Arusha. Katika kukabiliana na taarifa zinazokinzana na zinazowachanganya wakulima kuhusu huduma za ugani, Serikali imeanza matumizi ya mfumo wa usajili na habari kidijitali, ili kuwawezesha wakulima kupata taarifa sahihi na za kuaminika.
Mifumo hiyo iliyotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) inalenga kuendeleza mabadiliko ya kilimo kidijitali kote nchini, ikishughulikia changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya kilimo.
Taarifa iliyotolewa na FAO imesema mfumo huo utasaidia kukabiliana na kuzagaa kwa huduma nyingi za ugani za kilimo kidijitali zinazotoa taarifa zinazokinzana.
“Mkanganyiko huu umewaacha wakulima wakihangaika kuhusu mbinu bora na pembejeo za mimea yao.”
“Maelezo muhimu kuhusu hali ya barabara, maeneo ya masoko na maeneo muhimu ya uzalishaji wa kilimo yalikuwa hayapatikani au yalikuwa yamepitwa na wakati,” imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfumo huo utakuwa na dashibodi ya kilimo, ikijumuisha ramani za kuona za mfumo wa habari za kijiografia (GIS), itakayoruhusu ufuatiliaji wa wakati halisi na uchambuzi wa data za kilimo.
Akizungumza baada ya kupokea mifumo hiyo kwa niaba ya Serikali jijini Arusha, Mkuu wa kitengo cha Tehama (ICT) katika Wizara ya Kilimo, Vailet Kazimoto amesisitiza jukumu la mfumo huo katika kuimarisha juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo cha kidijitali.
“Sasa tunahamia kutoka kilimo cha jadi kwenda kilimo kidijitali. Mfumo huu utasaidia kuunda msingi imara wa kuwahudumia wakulima wetu kwa njia ya kidijitali, hatimaye kuongeza uzalishaji,”amesema.
Awali akizungumzia mfumo huo, Meneja wa Mradi wa FAO kwa mpango wa Hand in Hand, Mponda Malozo, ameipongeza Serikali kwa kukifanya kilimo kuwa cha kidijitali.
“Tumeshuhudia nia ya Serikali na tunafurahi sana kuwa sehemu ya safari hii. Lengo letu ni kusaidia mabadiliko ya kilimo kidijitali ambayo yataboresha uzalishaji na maisha ya watu wa Tanzania,” ameeleza Malozo.
Ameongeza kuwa mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi ya teknolojia katika kutatua matatizo magumu na kuleta maendeleo na Tanzania ipo njiani kufikia sekta ya kilimo yenye tija zaidi, endelevu na yenye ustahimilivu.