Serikali yasisitizwa kuwachunguza viongozi wa dini kabla ya kuwasajili

Dar es Salaam. Chama cha Wanawake Wahubiri wa Injili (WWI) kimetaka kabla Serikali haijatoa kibali cha kuwasajili viongozi wa dini, ijiridhishe iwapo wana wito wa kumtumikia Mungu.

Akizungumza leo Jumapili, Julai 30, 2024 Mkurugenzi wa WWI Jimbo la Temeke, Stella Mabuga amesema,

“Serikali kama itatoa vibali kwa viongozi wa dini kwa kuwachunguza na kuwathibitisha wenye wito wa Mungu, tunaamini matukio ya kulitia doa kanisa au taasisi za dini kwa namna yoyote ile hayatakuwepo.”

Stella amewahamasisha wanawake wawatie moyo wachungaji, waepuke matukio yanayochafua makanisa.

Kinyume na kufanya hivyo, amesema familia zitakosa maadili akitolea mfano watoto wengi kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Naye, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la EAGT,  Calvari Kongowe Privatus Kakweche amesema chama cha WWI kimekuwa kikiwahamasisha wanawake wamche Mungu na kusimamia familia zao.

Amesema baadhi ya familia zipo nje ya maadili hivyo mwanamke anaposimama inasaidia jamii kuwa na watu wema wenye hofu ya Mungu.

“Familia isipokuwa na maadili mema inasababisha watoto kujihusisha na vitendo viovu ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya, wizi, ushoga jambo ambalo linasababisha Taifa kuwa na kizazi kisichokuwa na maadili,” amesema Kakweche.

Related Posts