Katavi. Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mariam Sagini amesema wanawake wengi wamesahau jukumu lao kubwa la kuzaa na kulea familia kwa sababu ya vikundi vya kijamii vikiwamo vya vikoba.
Amesema hali hiyo inachangia kuporomoka kwa maadili ya watoto na vijana nchini.
Akizungumza katika Kikao cha Baraza la UWT Mkoa wa Katavi leo Jumapili, Juni 30, 2024, Sagini amesema baadhi ya kina mama wameacha majukumu yao ya kifamilia baada ya kujiunga na vikundi vya kijamii (vikoba).
Amesema, “baadhi ya wanawake hivi ninavyoongea hapa, walishaachana na waume zao kwa sababu ya uzembe wa kuhudumia familia na wanasahau pia walichoagizwa na Mungu na wengine wamo kwenye ndoa, lakini wameshindwa kujipa muda wa kulea watoto wao katika maadili, jambo ambalo ni hatari kwa familia,” amesema.
Hata hivyo, amesema ili kutengeneza viongozi bora watakaokuja kuongoza Chama cha Mapinduzi na jumuiya zake baadaye, watoto wanapaswa kuandaliwa sasa kama walivyoandaliwa wazazi wao.
Amesisitiza kuwa mama wa familia ndiye msingi mkubwa wa kutengeneza familia bora, akiyumba katika malezi ya watoto, ndiyo Taifa linashuhudia kizazi kisicho na maadili kikiendelea kutamalaki nchini.
Aidha, amesema hali ilivyo sasa ya mmomonyoko wa maadili hususan kwa watoto na vijana, kuna haja ya kukitafakari kizazi cha tatu kutoka sasa kitakuwaje.
“Kama tunaendelea kuwa na watoto ambao hawajalelewa kwa misingi ya maadili, tujue hawa ndio wazazi na viongozi wa kesho,” amesema kiongozi huyo.
Amesema katika hilo, wanawake hawawezi kukwepa lawama kwa sababu wengi wanajisahau linapokuja jukumu la nani anayepaswa kumlea mtoto akakua vema kwa misingi inayokubalika na jamii.
“Wengi wetu tupo bize na vikoba na tulioingia kwenye ulingo wa siasa pia tumesahau majukumu yetu ya kuzaa na kulea familia katika maadili,” amesema Sagini.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Katavi, Fotunata Kabeja amemshukuru Sagini kwa ushauri na kusema, “tunalizingatia na tunahimiza sana kina mama wenzetu kutengeneza familia bora. Kwa Katavi, kina mama ni waelewa na wanasimamia watoto vizuri japo changamoto hazikosekani.”
Wakati huohuo, Sagini amekabidhi simu janja nne kwa UWT Mkoa wa Katavi ili kusaidia kasi ya usajili wa wanachama wapya na kuimarisha umoja huo kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na mkuu mwakani.
Katibu wa UWT mkoani humo, Edina Buzima amesema simu hizo zitawasaidia kuongeza kasi ya kusajili wanachama kwenye umoja wao.
“Tulikuwa tunateseka sana kusajili wanachama na kufanya mkoa wetu kuwa nyuma katika uandikishaji. Sasa naamini hatua hiyo itafanyika kwa kasi zaidi na ufanisi mkubwa,” amesema Buzima.