Wabongo, Wakenya wakabana magari | Mwanaspoti

ITAKUWA ni mchuano mkali kati ya madereva wa Tanzania na Kenya katika mwezi huu wakati harakati za kuwaleta nchini washiriki kutoka Mombasa zikifikia hatua ya kuridhisha.

Kwa mujibu wa waandaji kutoka Klabu ya Mount Usambara, kuna mchakato wa kuwaleta Tanga madereva bingwa kutoka Mombasa nchini Kenya na kwa mujibu wa mwenyekiti wa klabu hiyo, Hussein Moor, ujio wa madereva hao utathibitishwa  mapema juma hili.

“Tuko katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato wa kuwadhamini madereva watatu, na majina yao na aina za magari watakayoyatumia vitawekwa bayana mapema juma hili,” alisema Moor na kusisitiza kuwa tarehe ya mashindano ni Julai 20 na 21 mwaka huu.

Akiendelea, Moor alisema umbali wa njia kuu ya mashindano ni kilomita 155  na madereva na magari yao watachuana katika maeneo yenye vivutio vya utalii vya maeneo ya Pongwe, Mkanyageni na Mlamleni.

Miongoni mwa madereva waongozaji (naviagtors) watakaozinogesha mbio za magari mwaka huu ni Mzambia David Sihoka ambaye ni mmoja wa magwiji wa  daraja la juu barani Afrika.

Sihoka, ambaye amekuwa akimuongoza dereva Muna Singh wa Zambia kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, safari hii atakuwa na dereva kutoka Arusha, Gurpal Sandhu wakiendesha gari aina ya Mitsubishi Evo 10, akiwa ni mzoefu sana wa barabara za Tanzania.

Kwa mujibu wa Moor, Kuwepo kwa madereva vinara wa mbio za magari kutazidisha ushindani.

Related Posts