Unguja. Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) limeingia makubaliano na taasisi sita kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupata huduma hiyo popote kidijitali, kwa lengo la kuleta ufanisi na kuwaondolea wateja usumbufu.
Akizungumza kwenye hafla ya kufikia makubaliano hayo leo Jumapili, Juni 30, 2024, Meneja wa shirika hilo, Haji Mohammed Haji amesema mbali na kuwaondolea wananchi usumbufu na kuwapunguzia gharama, pia hatua hiyo italeta ufansi kwa shirika.
Amesema jambo hilo litawapunguzia gharama za uendeshaji katika kuuza umeme kwani hadi sasa wana vituo vinane pekee vya kuuzia umeme vinavyotumia mfumo wa pesa taslimu.
Amesema katika kukabiliana na hilo, ndio sababu iliyowafanya kuingia makubaliano hayo kwani hilo litapanua wigo wa uuzaji umeme na kuwapunguzia mzigo wao.
“Katika mfumo huo shirika linaingia gharama katika ukusanyaji mapato kwani lazima ifikapo jioni tupite katika vituo hivyo kukusanya fedha na kuziweka makao makuu kabla ya kuzipeleka benki,” amesema Haji
Mashirika yaliyoinga makubaliano kuuza umeme ni benki ya NMB, CRDB, TigoZantel, NBC, TTCL na PBZ.
Meneja huyo amesema vituo vinavyotumika kuuzia umeme sasa vitafungwa kuanzia Julai na vitabaki vituo viwili vilivyopo makao makuu ya Zeco Guliono, Unguja na Chakechake, Pemba.
Kwa mujibu wa Haji, mfumo wa ukusanyaji wa mapato uliopo utaongezewa hifadhi zaidi ili mtu yeyote asiweze kuingia na kujipatia umeme bila ya kufanya malipo sahihi.
Kwa hivyo, kila mwenye mita atapatiwa tarakimu tatu zitakazobadilisha mfumo wa zamani na kuweka mfumo wa sasa na hilo litawasaidia kuongeza mapato.
Pia, amesema makubaliano hayo yatapunguza gharama za umeme kwani kila tokeni moja inauzwa Sh266 lakini baada ya kuingia makubaliano hayo inatarajiwa kupungua kutokana na ushindani utakaokuwapo kwenye mashirika hayo.
Hata hivyo, hakutaja itapungua kwa kiasi gani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi uendeshaji kampuni ya TigoZantel, Arnold Ngarashi amesema makubaliano hayo yanaonyesha ukuaji wa maendeleo ya sekta nishati visiwani humo kwani matumizi yake ni makubwa.
“TigoPesa kupitia mfumo wa kununua umeme tumefanya maboresho makubwa kama vile kupata tokeni iliyopotea, kuanzisha huduma ya mawakala wetu kuuza umeme na tuna wateja asilimia 80 kisiwani hapa,” amesema Ngarashi.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwani inawarahisishia wananchi kupata huduma hiyo kwa ufanisi.
Mkurugenzi wa Biashara Benki ya Watu wa Tanzania (PBZ), Eddie Muhina amesema jambo ambalo limewavutia kuingia makubaliano na shirika hilo ni gharama nafuu zilizowekwa, hivyo wataitumia fursa hiyo kusambaza huduma kwa wananchi.
Mmoja wa watumiaji wa umeme, Husna Hemed amepongeza hatua hiyo akisema itaondoa usumbufu kwani mwananchi atakuwa na uamuzi kupata huduma hiyo kupitia njia anayotaka, badala ya kwenda kupanga foleni kwenye vituo vya umeme.