Akizungumza katika mahojiano na gazeti moja la nchini hapa mwishoni mwa wiki, kiongozi wa kundi la wabunge wa chama cha Christian Social Union, CSU Alexander Dobrindt, alisema baada ya zaidi ya miaka miwili ya vita wa Ukraine sasa wanapaswa kufuata kanuni ya kutafuta kazi nchini Ujerumani au warudi kwenye maeneo salama magharibi mwa Ukraine.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ilijibu katika mkutano wa habari wa kawaida wa serikali siku ya Jumatatu, ikisema hakuna maeneo salaama nchini Ukraine.
Ingawa madai hayo yamekanushwa mara kwa mara na watafiti, Dobrindt alirudia hoja kwamba mafao ya watu wasio na ajira – maarufu kama Bürgergeld, yalikuwa yakiwaghafilisha wa Ukraine kutafuta kazi.
Soma pia:UN yataka dola bilioni 4.2, msaada kwa Ukraine, 2024
Hoja hiyo pia ilitolewa huko nyuma na chama cha Christian Democratic Union, CDU, chama ndugu na CSU katika siasa za Ujerumani, na wiki iliyopita na chama kidogo zaidi kwenye serikali ya mseto ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, cha Free Democrats, FDP.
Katibu Mkuu wa FDP Bijan Djir-Sarai, aliliambia gazeti la Bild siku ya Jumatatu iliyopita, kwamba wakimbizi wapya wa kivita kutoka Ukraine hawapaswi tena kupokea fedha za raia, lakini pia hawapaswi kushughulikiwa chini ya sheria ya waomba hifadhi, hii ikiwa na lengo na kuwalaazimisha Waukraine kutafuta ajira.
Djir-Sarai aliongeza kwaba kuna uhaba mkubwa wa wafanyakazi kila mahala, ikiwemo kwenye sekta za migahawa, ujenzi na utoaji wa huduma, na kwamba hawapaswi kutumia tena fedha za walipakodi kufadhili ukosefu wa ajira, lakini badala yake wanahitaji kuhakikisha kwamba watu wanapata ajira.
Vyama vinavyotawala vyapinga hoja
Vyama vyote vilivyomo kwenye serikali ya mseto – chama cha kansela Scholz cha SPD, na kile cha watetezi wa mazingira cha Kijani, vimepinga wazo hilo na kulitaja kuwa la upopulisti.
Lakini pendekezo la FDP lilipata uungwaji mkono mara moja kutoka chama cha upinzani cha CDU, ambao wamekuwa washirika wa muungano na FDP katika serikali kadhaa zilizopita nchini Ujerumani.
Wasemaji wa serikali walitoa ufafanuzi mara moja na kusema msimamo wa FDP hauakisi ule wa Kansela Olaf Scholz, na kwamba hakuna mipango ya kubadilisha msaada unaotolewa kwa wakimbizi wa Ukraine, na kubainisha kuwa hata mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya walikubali wiki iliyopita tu kuongeza muda wa ulinzi maalum wa wakimbizi wa Ukraine hadi 2026.
Soma pia:Ujerumani yaridhia masharti magumu kwa wahamiaji na wakimbizi
Takriban watu milioni 1.3 wenye uraia wa Ukraine wanaishi Ujerumani, kulingana na takwimu za serikali za Machi 2024, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Shirikisho, karibu watu 260,000 kati yao ni wanaume wenye umri wa kati ya miaka 18 na 60.
Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Brandenburg Michael Stübgen, aliuambia mtandao wa habari wa RND, kuwa haileti mantiki kuzungumzia kuiunga mkono Ukraine kwa njia bora zaidi iwezekanavyo na wakati huo huo kuwalipa wa Ukraine waliotoroka nchi yao.
Kulingana na hadhi yao maalumu, wa Ukraine wanazuwiwa kupitia mchakato mrefu wa kuomba hifadhi baada ya kuwasili, wanakuwa huru kuchagua mahala pa kuishi, na inawapa haki ya mara moja ya kupokea mafao ya kijamii, elimu na kibali cha kazi.
Mafao ya msingi kwa wakimbizi wa Ukraine
Kulingana na wakala wa ajira wa serikali ya shirikisho, mnamo Machi 2024, zaidi ya Waukraine 700,000 walikuwa wakipokea fedha za mafao ya msingi kwa watu wanaotafuta kazi. Hii ilijumuisha watu 501,000 walioainishwa kuwa wenyewe uwezo wa kufanya kazi na 217,000 ambao hawakuwa na uwezo, hasa watoto.
Takribani wakimbizi 185,000 wa Ukraine waliajiriwa nchini Ujerumani na kulipa michango ya hifadhi ya jamii.
Mnamo Oktoba 2023 utafiti uliofanywa na Wakfu wa Friedrich Ebert ulibaini kuwa ujumuishaji wa wakimbizi wa Ukraine katika soko la ajira la Ujerumani ulikuwa nyuma ya ule wa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.
Soma pia:Steinmeier: Ujerumani imefikia ukomo wa kupokea wahamiaji
Wakati asilimia 18 tu ya wakimbizi wa Ukraine walipata kazi nchini Ujerumani, nchini Poland, Jamhuri ya Czech na Denmark idadi ilikuwa theluthi mbili au zaidi.
Nguvu kazi ya Ujerumani inayozidi kuzeeka inamaanisha kuwa nchi hiyo inazidi kutegemea wafanyakazi wa kigeni katika sekta kadhaa.
Lakini kinachowatatiza wakosoaji wengi ni kwamba wengi wa wakimbizi wa Ukraine ni wenye umri wa kupigana – ingawa ukweli ni kwamba wanaume wengi wa Ukraine hawataki kupigana.