Akiandika katika ukurasa wake wa kijamii wa X uliojulikana kama Twitter zamani, Zakir Jalaly afisa mkuu katika wizara ya mambo ya nchi za nje wa Afghanistan, amesema watajaribu kuishinikiza Jumuiya ya Kimataifa kuiondolea nchi yao vikwazo vya kiuchumi.
Taarifa yake inafuatia ile ya msemaji wa serikali ya Afghanistan Zahibulla Mujahid, aliyeuliza katika ufunguzi wa mkutano huo hapo jana ni kwanini Afghanistan inaandamwa kwa vikwazo vya pamoja, akihoji pia iwapo vikwazo hivyo vinastahili kuwepo nchini humo hasa baada ya miongo kadhaa ya vita na ukosefu wa usalama, uliosababishwa na uvamizi wa mataifa ya kigeni na kuingiliwa kwa mambo yake ya ndani.
UN yaitaka Taliban kuondoa ‘sheria kandamizi’ dhidi ya wanawake
Kuondoa vikwazo hivyo vya kiuchumi, kuachia fedha zinazozuiliwa na kutolewa kwa njia mbadala kwa wakulima wa taifa hilo hasa wale waliokuwa wanategemea kilimo cha mmea wa Poppy,unatumika kutengeneza mihadarati ni miongoni mwa matakwa ya kundi hilo. Mkutano huo wa faragha unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na serikali ya Taliban, unawajumuisha kwa mara ya kwanza wajumbe wa Taliban tangu walipochukua madaraka mwaka 2021.
Mkutano huo uliofunguliwa na Mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo, ulijaribu pia kuyajadili mengi yanayoonekana kuwa changamoto Afghanistan kama masuala ya haki za binaadamu, haki za wanawake na ujumuishwaji wa makundi yote ya kisiasa katika serikali. Lakini Zabihullah Mujahid ametahadharisha kwamba masuala ya ndani ya Afghanistan hayapaswi kuwekwa katika meza ya mazungumzo.
Bado kuna wasiwasi juu ya uimarishaji wa haki za wanawake
Taliban imekataa makundi kadhaa kushiriki ikiwemo wanawake ikisisitiza kuwa kundi hilo ndio muakilishi pekee wa mikutano ya kimataifa ili kudhibiti uingiliaji wa kigeni katika masuala yake.
Hata hivyo baadae hii leo Rosemary DiCarlo amepangiwa kukutana na makundi ya wanaharakati wa Afghanistan. Mkuu huyo wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa amesema lengo la mkutano huo wa Qatar ni kuwa na Afghanistan iliyo thabiti na iliyo na amani na itakayojumuishwa katika masuala ya kimataifa na kufanikisha pia ahadi zake za kuimarisha haki za binaadamu hasa haki za wanawake na wasichana.
Taliban yakosolewa kwa kuwatenga wanawake katika mazungumzo na UN
Tangu kundi hilo lilipochukua madaraka mwaka 2021, limekataa miito ya kuundwa kwa serikali ya pamoja, na kuhakikisha haki za wanawake kupata elimu na kufanya kazi zinaheshimiwa. Kutokana na hayo hakuna hata nchi moja hadi sasa iliyoitambua serikali hiyo ya Taliban iliyopo katika bara Asia.
Fedha zake hadi sasa zimezuiliwa katika mataifa ya Magharibi na wakuu wa kundi hilo bado wapo katika orodha ya watu wanaohitajika na serikali ya Marekani. Lakini matukio ya hivi karibuni ya Marekani kulegeza vikwazo vya usafiri kwa baadhi ya viongozi wa kundi hilo, na Umoja wa Ulaya kutangaza msaada wa kibinaadamu kwa taifa hilo, inaashiria kulegea kwa msimamo wa Jumuiya ya Kimataifa dhidi ya Afghanistan.
Ujerumani inapanga kuwarejesha wanadiplomasia wake Kabul
Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa serikali ya Taliban Hamdullah Fitrat, amekaribisha hatua ya wanadiplomasia kurejea mjini Kabul akisema serikali itatoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha lengo hilo. Fitrat amesema hatua hiyo itaongeza ushirikiano wa kisiasa na mahusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Hatua hii inatokana na taarifa ya hivi maajuzi ya msemaji wa ofisi ya sera za kigeni wa chama cha Social Democratic Party (SPD) Nils Schmid akipendekeza mabadiliko ya kisera kwa Taliban kama chama tawala nchini Afghanistan, akisema haiingii akilini kwa Taliban kuachia madaraka hivi karibuni.
Mwaka mmoja wa Taliban madarakani
Hata hivyo Berlin imekuwa kidogo na mashaka juu ya mahusiano yake na kundi hilo kufuati wasiwasi kuhusiana na masuala ya haki za binaadamu na haki za wanawake na wasichana. Ujerumani ilifunga ubalozi wake mjini Kabul mwaka 2021 baada ya kundi hilo kuchukua madaraka.
dpa