BIL 1.9 ZIMETUMIKA MATENGENEZO BARABARA ZILIZOATHIRIWA NA EL-NINO MKOANI SHINYANGA-ENG JOEL

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt samia Suluhu Hassan imetoa fedha shilingi Bilioni 1.9 kwa ajili ya kushughulikia barabara zilizoathiriwa na Mafuriko/mvua za Elnino kwa Mkoa wa Shinyanga.

Fedha hizo zimetumika kuhakikisha kuwa miundombinu yote ya barabara iliyoathirika na wananchi kushindwa kutoka eneo moja kwenda jingine inapitika kwa haraka kama ambavyo serikali ilikusudia.

Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya miradi ya barabara inayoendelea na matengenezo mbalimbali Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania-RANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Samwel Mwambungu amesema kati ya fedha hizo shilingi Milioni 930 zimetumika kurejesha miundombinu ya barabara katika eneo la Kijiji cha Ngaya Burige kwenye barabara ya Mwakitolyo Kahama – Burige – Mwakitolyo – Solwa Yenye urefu wa Kilomita 80.

Pia amesema Milioni 243 zimetumika kurejesha miundombinu katika maeneo ya vijiji vya Lunguya, Kalagwa, Izengwabahala na Ilogi Barabara ya Buyange – Busoka/Kahama – Kakola yenye urefu wa kilomita 73.

Eng Joel amezitaja barabara zingine kuwa ni pamoja na Milioni 127 zilizotumika katika vijiji vya Bunambiyu, Mwapalalu na Itongoitale vilivyoathirika katika Barabara ya Itongoitale – Bunambiyu – Mwapalalu yenye urefu wa kilomita 33.8. Sambamba na Milioni 600 zilizotumika kwa ajili ya kurejesha mawasiliano katika maeneo ya Mwabomba na Ulowa kwenye Barabara ya Mwabomba – Bugomba A – Ulowa – Igombe River yenye urefu wa Kilomita 98.

Katika hatua nyingine Mhandisi Joel ameitaja miradi mbalimbali iliyofanyiwa upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami ambayo ni pamoja na Barabara ya Kolandoto – Mwangongo km 53; (Kuunganisha Mkoa wa Simiyu).

Pia Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina umefanywa na umekwisha kamilika katika barabara ya Kolandoto – Lalago, yenye urefu wa Kilomita 54 ambapo hata hivyo Utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utaanza mwaka wa fedha 2024/25 na umetengewa Shilingi Bilioni 1.0 kwa ajili ya maandalizi ya Ujenzi.

Miradi mingine ni kukamilika kwa asilimia 100 ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara ya Salawe – Old Shinyanga (Sehemu ya Solwa – Old Shinyanga) urefu wa Kilomita 64.66 Mpakani na Mwanza.

Mhandisi Joel amezitaja barabara zingine zilizofanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kuwa ni barabara ya Nyandekwa – Uyogo – Ng’hwande (km 55), kukamilika kwa asilimia 100 Upembuzi Yakinifu wa Ujenzi wa barabara ya Mpanda – Kaliua – Ulyankulu – Uyogo – Nyamilangano – Nyandekwa – Kahama ambayo kwa mwaka wa Fedha 2024/25 imetengewa Fedha Shilingi Milioni 350 kwa ajili ya maandalizi ya Ujenzi.

Pia kukamilika kwa usanifu katika Barabara ya Shinyanga Bubiki (km 35) ambapo Serikali itatekeleza ujenzi wake kwa kilomita zote 35 baada ya kupata fedha. Kwa mwaka wa Fedha 2024/25 imetengewa Fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1.0 kwa ajili ya kujenga km 1.2 kwa kiwango cha lami.

Nyingine ni kukamilika kwa usanifu wa Barabara ya Kahama – Solwa (Km 76.69) ambapo Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara yote baada ya kupata fedha. Kwa sasa serikali inakamilsha ujenzi wa vipande vya lami (jumla Km 1.4) katika miji ya Ngaya na Burige.

Mhandisi Joel ameitaja barabara nyingine iliyofanyiwa usanifu kuwa ni Barabara ya Kahama – Tulole – Muhulidede (Km 39.96) ambayo kwa mwaka wa Fedha 2024/25 imetengewa shilingi Milioni 650 kwa ajili ya kukamilisha usanifu na manadalizi ya Ujenzi.

Serikali imekuwa ikitoa jumla ya Shilingi Bilioni 10.69 kila mwaka kuhakikisha Kilomita 1177.74 zinahudumiwa ili ziweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka.

Related Posts