HISIA ZANGU: Yusuf Manji, kutoka ufalme Jangwani mpaka pumzi za mwisho Florida

YUSUF Manji. Mtu na pesa zake. Amevuta pumzi zake za mwisho katika maisha haya ya dunia, Jumamosi, jijini Florida nchini Marekani. Nyuma yake ameacha historia ya kusisimua katika soka letu na maisha ya Watanzania wengi.

Tuanzie wapi kuhusu Manji? Hatujui sana katika maisha yake ya nyuma kabla hajaamua kuanza kuingiza pesa zake katika Klabu ya Yanga. Ndiyo. Tanzania mchezo wa soka huibua jina la mtu kwenda juu ghafla na kwa kasi hasa kama ukijiingiza katika siasa za Simba na Yanga.

Kulikuwa na matajiri wengi nchini ambao mpaka wanaondoka duniani hatukuwahi kuwajua kwa sura wala kujua kwamba walikuwa na pesa nyingi. Yusuf angeweza kuishia hukohuko kama asingejitumbukiza katika Klabu ya Yanga.

Akaanza kuleta wachezaji mafundi na uwezo mkubwa. Kina Donald Ngoma, kina Thabani Scara Kamusoko, kina Obrey Chirwa na wengineo. Kabla ya hapo Yanga walikuwa wanachangishana pesa za usajili kutoka kwa matajiri wao wa wakati huo. Kina Seif Magari, Ndama mtoto wa Ng’ombe, Abdallah Bin Kleib na zaidi ya wote ni Francis Mponjoli Kifukwe.

Manji akaichukua Yanga akaiweka mfukoni. Akazima migogoro ya wazee ambao ilikuwa maarufu wakati huo klabuni. Akakodi ndege iliyozunguka kuhamasisha maridhiano kati ya wazee wa Yanga Asili na Yanga Kampuni.

Ujio wa Manji Yanga ukaifanya ghafla Simba kuwa yatima. Wakati ule kundi la Friends of Simba lilionekana kuwa kundi la watu matajiri, lakini alipoingia Manji ghafla matajiri halisi wakajulikana. Manji Yanga na familia ya Bakhresa pale Azam.

Kwa misimu mitano mfululizo Simba walijikuta wakiangukia nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi. Labda ndani ya umaskini huu wa ghafla wakajikuta wakijiaminisha katika sera ambayo haiwezi kukubalika katika timu yoyote kubwa duniani. Sera ya kuanza kutumia vijana. Hapa ndipo wakaanza kuhangaika na kina Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude, Ramadhan Singano, Miraji Athuman na wengineo. Waliishia kuteseka. Timu kubwa zipo kwa ajili ya wachezaji wakubwa.

Yusuf akatia pesa hasa. Inashangaza kidogo. Wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia mchezo wa soka sio mapenzi yao makubwa. Huwezi kukuta tajiri wa Kihindi akimiliki timu ya soka katika daraja lolote lile katika nchi za England, Italia, Hispania, Ujerumani, Ufaransa na kwingineko.

Hata Afrika ni kitu ambacho kimetokea Tanzania tu. Hata hivyo Yusuf alijua kumwaga noti zake. Kuanzia kwa wachezaji hadi wanachama. Baadaye ghafla akaamua kuchukua Uenyekiti wa klabu. Nani angemzuia? Ni sawa sasa hivi Ghalib Said Mohamed akiamua kuwa rais wa Yanga. Nani atamzuia?

Baada ya kutamba kwa miaka kadhaa, siasa ndio zilikuja kummaliza Manji na Yanga yake. Akawa diwani pale Mbagala. Baadaye katika maisha yake akajikuta katika wakati mgumu wakati nchi ilipobadili utawala wa kiuongozi kutoka awamu ya nne kwenda awamu ya tano.

Manji akajikuta gerezani Keko kwa mashtaka ambayo wengi hatukuyaelewa. Yanga nao wakaanza kuishi kama wapo jela ingawa walikuwa uswahilini. Kuanzia hapo wakavaa vazi la njaa. Manji hakuwaachia misingi mizuri ya kuishi bila ya yeye.

Sijui kama ilikuwa bahati mbaya au ilipangwa lakini wakati Manji akiwa gerezani, Mohamed Dewji akajitokeza kuichukua Simba. Mpaka leo hatujui ni kwanini hakujitokeza kuichukua Simba wakati Manji akiwa bado anatumia pesa zake Yanga.

Kuanzia hapo Simba ikabadilisha sera zake ghafla. Ikavuna wachezaji wanne wazuri pale Azam. Aishi Manula, John Bocco, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe. Halafu wakachukua wachezaji mahiri wa kigeni wakiongozwa na Clatous Chotta Chama. Hapa ndipo Simba walikwenda kuchukua mataji manne ya Ligi Kuu mfululizo huku Yanga ikishika nafasi ya pili.

Bila ya Manji Yanga wangetambaje wakati walikuwa wanachangishana hadi nauli kwenda Mwanza na Mbeya? Nahodha Ibrahim Ajibu akatumika kama alama ya michango. Kocha Mwinyi Zahera naye akatumika kama kikokotoo cha michango.

Manji alipotoka ndani hakuwa yuleyule tena. Bahati nzuri Yanga ikaenda kuokolewa na GSM akimtumia kijana wake Injinia Hersi Said. Ni hili ndilo ambalo kwa kiasi kikubwa liliirudisha Yanga katika ushindani mpaka leo kiasi kwamba mpaka sasa wametwaa mataji matatu mfululizo ya ligi na wamefika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 kitu ambacho hata Manji alishindwa.

Hakukuwa na nafasi tena kwa Manji kurudi Yanga ingawa bado alikuwa na kundi dogo la wanachama ambao waliamini bado alikuwa na nafasi yake. Hata hivyo kundi kubwa lilikuwa limehamia kwa GSM wakiamini kwamba anapaswa kushukuriwa kutokana na kuikoa klabu yao katika fedheha ya michango.

Mpaka jana wakati mwili wake ukizikwa jijini Florida nchini Marekani, mashabiki wengi wa Yanga waliendelea kumheshimu Manji kutokana na ile miaka minne aliyowapa kiburi. Walimpenda kutokana na kuwa tajiri aliyetumia pesa hasa kwa ajili ya Yanga. Walimpenda kutokana na namna ambavyo aliwakomboa kutoka katika kucha za Friends of Simba.

Lakini walimheshimu pia kwa sababu aliondoka Yanga kwa sababu ambazo zilieleweka. Hakuwatupa bali alijikuta katika wakati mgumu nchini kiasi ambacho tunaambiwa alitoroka nchi. Ulikuwa mwisho mbaya kwa Yanga, lakini hakuna ambaye alimlaumu mwenzake kwa kuachana kwao.

Hatujui ugonjwa ambao umesababisha mauti yake na wala hatujui kama ugonjwa una uhusiano na matatizo aliyopitia akiwa nchini. Wakati ule akiwa jela alijikuta akilazwa mara kwa mara katika hospitali za Muhimbili na Agha Khan.

Related Posts