Unguja. Licha ya fursa zinazopatikana katika sekta ya utalii na Uchumi wa Buluu, bado jamii haijaweza kuzifikia kutokana na uelewa mdogo na hofu ya uthubutu.
Kutokana na changamoto hiyo, Chuo cha Utawala wa Umma (Ipa) kimeanza mpango wa kuwapeleka wataalamu chuoni hapo kuwapa elimu ya maeneo hayo wanafunzi ili kuwaandaa kuwa mabalozi katika jamii kuhusu suala hilo.
Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi wa Ipa, Dk Salum Rashid Moh’d amesema wamebaini bado kuna pengo kubwa hivyo elimu zaidi inahitajika ili kuiwezesha jamii kuzifikia fursa zinazopatikana katika sekta hizo ambazo zinaweza kutoa ajira na kuwa mkombozi kwa vijana wengi.
Akizungumza katika mhadhara uliowashirikisha wanafunzi wa fani ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na biashara chuoni hapo jana Juni 30, 2024, Dk Salum amesema sekta hizo zimejumuisha aina nyingi za biashara.
Miongoni mwa biashara hizo ni pamoja na kilimo, uvuvi na utoaji wa huduma za utalii kwa wageni hivyo mikakati zaidi inahitajika katika kuzifikia na kuzichangamkia fursa hizo kwani utekelezaji wake unaendana na sera ya Taifa ya uchumi wa bluu.
“Hizi sekta zina fursa nyingi ambazo ni mkombozi lakini bado jamii haijaweza kuzifikia kwa sababu bado elimu ni ndogo kwa hiyo ipo haja sasa elimu hii ikaifikia jamii ili watumie fursa hizi kujikomboa kimaisha,” amesema Dk Salum.
Naye Mkurugenzi Idara ya Utawala wa biashara, Mahmoud Makame amesema wameamua kutafuta wataalamu wa utalii ili kuwaelekeza wanafunzi fursa zilizopo katika sekta hiyo na namna nzuri ya kuziendea.
“Hapa ni kuwajenga wanafunzi baada ya kuhitimu masomo yao wajiwezeshe kiuchumi kwa kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira serikalini,” amesema Makame.
Kwa upande wake, mtaalamu wa utalii kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Ilias Rajab Nassor alisema katika sekta hiyo kuna fursa nyingi zikiwemo za kutembeza wageni, kuwahudumia wanapokuwa kwenye hoteli na kuwatafsiria lugha.
Mmoja wa wanafunzi hao, Latifa Hassan Babar amesema hawakuwa na uelewa kuhusu fursa hizo na kushauri mpango huo uendelee hata katika maeneo mengine, kwani utawasaidia vijana wengi kupata uelewa wa kuchangamkia fursa hizo.
“Mara nyingi vijana tukimaliza elimu ya juu tunasubiri kuajiriwa ama serikalini au sekta binafsi kumbe kuna mbinu nyingi za kupata ajira ikiwa ni pamoja katika sekta hizi,” amesema.
Mwanafunzi mwingine Harith Abdalla amesema, “uthubutu unatuponza wanafunzi wengi lakini tunapojengewa uwezo kwa njia hii wengi tunaamka na inakuwa rahisi kuziendea fursa hizi badala ya kuzunguka na bahasha kutwa nzima kuomba kazi.”