Israel yaendelea kukabiliana na wanamgambo wa Kipalestina – DW – 01.07.2024

Idadi hiyo ya vifo 37,900 inajumuisha karibu watu 23 waliopoteza maisha katika muda wa saa 24 zilizopita. Taarifa ya wizara ya afya ya Palestina inayodhibitiwa na Hamas imeongeza kuwa watu 87,060 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita hivyo mnamo Oktoba 7 mwaka jana.

Mashambulizi makali yameripotiwa katika Ukanda wa Gaza, ambapo vifaru vya Israel vilizidisha uvamizi katika kitongoji cha mashariki cha  Shejaia  kwa siku ya tano mfululizo, huku vikosi vingine vikisonga mbele zaidi kuelekea maeneo ya magharibi na hata kusini katika mji wa Rafah unaopakana na Misri. Israel imetangaza pia kifo cha askari wake mmoja huko Rafah, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

Picha ikionyesha mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel ikiharibu roketi zilizorushwa dhidi yake
Picha ikionyesha mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel ikiharibu roketi zilizorushwa dhidi yakePicha: Ayal Margolin/Xinhua/picture alliance

Hayo yakijiri, wanamgambo wa Kipalestina wa Islamic Jihad wanaoungwa mkono na Iran na ambao ni washirika wa Hamas, walivurumisha karibu roketi 20 kuelekea Israel. Islamic Jihad wamesema hiyo ni hatua ya kujibu kile walichokiita “uhalifu wa adui wa Kizayuni dhidi ya watu wetu wa Palestina”.

Soma pia: Baraza la Usalama lashindwa kupitisha azimio la kusitisha vita Gaza

Hata hivyo jeshi la Israel limesema mashambulizi hayo hayakuwa na madhara yoyote lakini yanaonyesha kuwa wanamgambo hao wanazo silaha za kutosha na kuwa bado ni tishio kwa taifa hilo.

Eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu na Israel limeshuhudia pia ghasia ambako kumeripotiwa vifo vya Wapalestina wawili katika mji wa Tulkarm. Vikosi vya Israel vimedai kuwa waliouliwa ni wanamgambo na kwamba eneo hilo waligundua maficho ya silaha kadhaa.

Israel yawaachilia huru wafungwa wa Kipalestina 

Kando ya  mashambulizi na makabiliano , Israel imewaachilia huru Wapalestina zaidi ya 50 waliokuwa wamezuiliwa nchini humo. Miongoni mwa walioachiliwa ni Mohammed Abu Salmiya, Mkurugenzi mkuu wa hospitali kubwa ya Gaza ya al-Shifaa.

Wapalestina wakisherehekea kuachiliwa kwa jamaa zao kutoka Israel
Wapalestina wakisherehekea kuachiliwa kwa jamaa zao kutoka IsraelPicha: Wahaj Bani Moufleh/Middle East Images/AFP/Getty Images

Salmiya amesema alipitia “mateso makali” kwa muda wote wa zaidi ya mizi saba alipokuwa amezuiliwa nchini Israel, kama anavyothibitisha Wael Diab Ahmad Mansour mfungwa mwingine aliyeachiliwa huru:

” Wakati wa uchunguzi tulikabiliwa na vitendo kadhaa vya mateso kama kupigwa, kumwagiwa maji ya moto, au maji ya baridi wakati wa majira ya baridi kali. Tulikuwa tunafungwa kwenye kiti na mara nyingi tunapigwa na shoti ya umeme, walikuwa wanaweza pia hata kutukojolea.”

Soma pia: Israel-Hamas wakubaliana kuachiwa mateka na wafungwa

Wafungwa wengine walioachiliwa wameelezea pia kuwa watu wengine waliuliwa wakati wakihojiwa na vikosi vya Israel huku wengine waking´olewa meno, kuvunjwa vidole, kunyimwa chakula na maji na mateso mengine ambayo wamesema yaliwaathiri na kuwadhalilishwa kimwili na kisaikolojia.

(Vyanzo: Mashirika)

Related Posts

en English sw Swahili