Kamusi, misamiati wanafunzi wenye mahitaji maalumu zaja

Musoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iko katika mchakato wa kuandaa kamusi ya lugha ya alama ya vifaa vya ufundi kwa ajili ya masomo kwa watu wenye mahitaji maalumu.

Pia, wizara hiyo inatarajia kuandaa kamusi na misamiati kama mwongozo wa kufundishia masomo ya sayansi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu nchini.

Hayo yamesemwa leo, Jumatatu Julai Mosi, 2024 mjini Musoma na Ofisa Mwandamizi Idara ya Elimu Maalumu kutoka wizara hiyo, Selemani Chamshama kwenye mafunzo kuhusu mahitaji maalumu na elimu jumuishi kwa watumishi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT).

Chamshama amesema kutokana na utafiti uliofanywa na wizara hiyo, wamebaini wanafunzi wengi wenye mahitaji maalumu wanaacha masomo ya sayansi na ufundi kutokana na sababu nyingi, miongoni mwao ni upungufu wa nyenzo za kufundishia, ikiwemo kamusi na misamiati ya lugha za alama kwa masomo hayo.

“Wapo wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambao wana vipaji na matamanio ya kusoma masomo ya sayansi na ufundi, ili watimize ndoto zao za kuwa watu fulani huko mbeleni, lakini wanashindwa. Tunaamini hii itakuwa ni suluhisho la changamoto hiyo,” amesema Chamshama.

Amesema mchakato huo utakamilika ndani ya mwaka huu wa fedha na utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha kama sehemu ya maboresho ya sekta ya elimu yanayofanywa na serikali.

Amefafanua kuwa itakuwa ni ajabu Serikali kuingiza elimu ya amali katika mitalaa yake, wakati haina nyenzo za kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Hata hivyo, Chamshama amesema anaamini baada ya nyezo hizo kukamilika, wanafunzi wengi wenye mahitaji maalumu watasoma zaidi mafunzo ya amali kuliko elimu ya kawaida.

Msimamizi wa elimu jumuishi na mahitaji maalumu katika mradi wa uboreshaji elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi chuo cha MJNUAT, Dk Joel Matiku, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanafunzi wote wanaodahiliwa chuoni hapo kupata huduma sawa, sahihi na kwa wakati.

“Kama mnavyojua, chuo chetu tayari tumeanza kudahili wanafunzi na tunatarajia kudahili hadi wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Kwa hiyo, kupitia mafunzo haya tuna uhakika kila mwanafunzi atapata huduma sahihi, ikiwemo ya masomo bila kikwazo,” amesema.

Amesisitiza kuwa elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu ni muhimu na ni haki yao ya msingi, hivyo hakuna sababu ya kumuacha mtu nyuma kutokana na hali yake.

Mhadhiri wa chuo hicho, Dk Erasto Focus amesema mafunzo hayo ya siku nne yatawasaidia kupata ujuzi na uelewa juu ya namna ya kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Tunaomba haya mafunzo yawe ya mara kwa mara, kwani kwa muda mrefu kundi hili la watu wenye mahitaji maalumu limeachwa nyuma, hivyo ni vema tukaenda nalo sambamba, kwani wana haki kama walivyo watu wengine,” amesema.

Related Posts