KUNA kila dalili ya Mtanzania Madina Iddi kushinda taji la ubingwa wa wazi la mashindano ya kimataifa ya gofu mjini Lusaka Zambia mwaka huu.
Akiwa ni mchezaji kutoka klabu ya Gymkhana ya Arusha, Madina aliwaacha mbali sana wapinzani wake kutoka Zambia, Kenya, Uganda na Botswana, kwa jumla ya mikwaju tisa hadi mwisho wa raundi ya pili.
Dada Mtanzania huyo alianza kwa kuongoza mashimo 18 ya kwanza kwa mikwaju 78 kabla ya kuandika mikwaju 80 siku ya pili na hivyo kupata jumla ya mikwaju 158.
Madina amemuacha aliyekuwa mpinzani wake wa karibu siku ya kwanza, Esther Wemba wa Zambia kwa jumla mikwaju 12.
Wemba aliyeanza na mikwaju 81 siku ya kwanza, alirudi na mikwaju 89 siku ya pili na hivyo kuishia na mikwaju 170 hadi Jumamosi jioni.
Mzambia mwengine aliyekuwa karibu na Madina, lakini akaachwa nyuma hadi Jumamosi jioni ni Martha Matyola ambaye alipiga jumla ya mikwaju 167 na hivyo kuwa katika nafasi ya pili, baada ya kuwa na mikwaju 9 nyuma ya Madina Iddi.
Vilevile kutoka Zambia ni Gracious Mwenda ambaye alikuwa na jumla ya mikwaju 182, akiwa nyuma ya Mtanzania kwa mikwaju 24.
Lakini mambo hayakuwa mazuri kwa Aalaa Somji na Ayne Magombe, Watanzania wengine walioshiriki mashindano ya mwaka huu nchini Zambia.
Magombe alipiga jumla ya mikwaju 182 wakati Somji akileta jumla ya mikwaju 185 katika jumla ya mashimo 36 ya siku mbili za mashindano hayo.
Siku ya kwanza Magombe alijitahidi kwa mikwaju 89 kabla kutengeneza mikwaju 93 siku ya pili wakati Somji alianza na 90 siku ya kwanza kabla ya kupiga mikwaju 95 siku ya pili.
Haya ni mashindano ya siku tatu.