Songwe. Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ileje, Mkoani Songwe, kimesema kitawafikisha kwenye vikao vya maadili ya chama hicho makada wanaojipitisha kwa lengo la kutaka nafasi za ubunge na udiwani kabla ya wakati.
Makada hao watafikishwa kwenye vikao vya kamati ya maadili kwa utaratibu utakaohusisha upokeaji wa tuhuma dhidi yao wanaokiuka miongozo ya chama hicho, ikiwepo kuanza kampeni mapema.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mwenezi wa CCM wilayani humo, Maoni Mbuba wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo leo Jumatatu Julai mosi, 2024, kikiwa ni kikao cha kawaida cha kikatiba.
Mbuba amesema hayo baada ya kuwepo tetesi za kuwepo kwa baadhi ya makada wanaojipitisha kwenye kata kwa lengo la kujitangazia nia ya kugombea nafasi za ubunge na udiwani, kitendo ambacho kinalenga kuwaharibia na kufifisha utendaji kazi wa viongozi waliopo madarakani.
Amesema kujipitisha kwa makada hao kutasababisha kukigawa chama na kuweka makundi ambayo hayana tija ndani ya chama na taifa letu kwa ujumla kwa kuwaletea maendeleo Watanzania.
“Tuwape nafasi viongozi waliochaguliwa hadi muda wao utakapofika ukomo, na kama chama tutahakikisha kuwafikisha kwenye kamati ya maadili makada wote wanaokiuka katiba ya chama kuhusu kanuni za uchaguzi,” amesema Mbuba.
“Viongozi wa vijiji, udiwani na wabunge wanaotokana na CCM ni viongozi halali kwa sasa mpaka muda wao utakapofika, ikiwa ni mwaka huu kuchagua viongozi ngazi ya vijiji na madiwani pamoja na wabunge na Rais mpaka Uchaguzi Mkuu mwaka 2025,” ameongeza.
Mbunge wa Ileje na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya Msongwe amewataka wanachama na wananchi wa Ileje kuwapuuza makada wanaojipitisha kwa lengo la kutaka nafasi za uongozi kabla ya muda, bali washikamane na viongozi waliopo madarakani kuleta maendeleo.
Msongwe amesema, “Tuwapuuze watu wanaojipitisha kutengeneza chuki dhidi ya viongozi, hivyo tunakipongeza chama kwa kuliona hili kwa lengo la kuleta utulivu ndani ya chama.
“Tutahakikisha tunawaletea wananchi maendeleo bila kujali watu wasiowatakia mema viongozi waliopo madarakani. Tunachowaomba wananchi na wanachama wote mtuombee kama tulivyoaminiwa kukaa madarakani miaka mitano na tutahakikisha maendeleo yanawafikia wananchi.”
Katibu wa CCM kata ya Ibaba, Sadamu Mwasinyanga, amesema kuna baadhi ya makada kuzunguka kwenye kata zao bila viongozi kuwa na taarifa, hivyo kuwaomba viongozi wa chama wilaya kuwapa meno kwa lengo la kuwachukulia hatua makada wasio watiifu.
Amesema kuna utitiri wa makada wakipita kwenye kata wakitangaza nia ya kugombea nafasi za ubunge na udiwani.
“Je, kabla ya muda inaruhusiwa? Kwa nini chama kisiwashughulikie kama si hivyo mtupe mamlaka sisi viongozi wa kata kuwawajibisha,” amesema Mwasinyanga.