Mapya kesi ya kutekwa Kabendera, Vodacom yaitwa mahakamani

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salalam, imeitaka Kampuni ya huduma za mawasiliano ya simu za mkononi, Vodacom kufika mahakamani na kuwasilisha nyaraka inazotarajia kuzitumia katika kujitetea katika kesi ya madai iliyofunguliwa na wanahabari, Erick Kabendera dhidi yake.

Katika kesi hiyo, Kabendera anaoimba mahakama iiamuru kampuni hiyo imlipe fidia ya Dola za Marekani 10 milioni (sawa na Sh28 bilioni), akiituhumu kuwa ndio iliyofanikishwa kukamatwa kwake na polisi, tukio analoliita kutekwa na kisha kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, mwaka 2019.

Kabla ya kufungua kesi hiyo, Kabendera aliyejikita katika uandishi wa habari za uchunguzi, kupitia kwa Wakili Peter Madeleka aliiandikia barua kampuni hiyo akiitaka imlipe fidia ya Dola za Marekani 1 milioni (zaidi ya Sh2.5 bilioni), huku akiipa siku 14.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Vodacom Tanzania PLC, Zuweina Furaha alilithibitrishia Mwananchi kupokea barua hiyo na kueleza walikuwa wanaifanyia kazi.

“Tumepokea taarifa hiyo na tunaliangalia suala hilo na madai kupitia timu yetu ya wanasheria.” amesema Furaha.

Hata hivyo, wakili Madeleka ameleilieleza Mwananchi kuwa mteja wake amechukua uamuzi wa kufungua kesi hiyo mahakamani baada ya muda wa siku 14 walioipatia kampuni hiyo kumalizika, bila kampuni hiyo kufanyia kazi maelekezo hayo.

Wakili Madeleka amelieleza Mwananchi kuwa kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi na itatajwa kwa mara ya kwanza Julai 9, 2024.

Kwa mujibu wa hati ya wito wa mahakama kwa wadaawa (pande zote) kufika mahakamani, kesi hiyo namba 12799/2024 imepangwa kutajwa tarehe hiyo saa 2:30 asubuhi, huku ikiitaka kampuni hiyo kufika bila kukosa na kuwasilisha nyaraka zake inazotarajia kuzitumia katika utetezi wake.

“Fahamu kwamba kesi iliyotajwa hapo juu imepangwa kutajwa kikao cha mwisho cha kupanga usikilizwaji Julai 9, 2024, saa 2:30 asubuhi, mbele ya Jaji Maghimbi inasomesema hati hiyo ya wito na kuongeza;

“Unatakiwa kufika katika mahakama hii bila kukosa na lazima uwasilishe siku hiyo nyaraka zote ambazo unatarajia kuzitimia katika kesi yako,” imeeleza hati ya wito wa mahakama.

Katika kesi hiyo, Kabendera anadai kuwa kutokana na matukio hayo amepata madhara ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi, ya kijamii, maumivu ya kiakili na kimaono, hasara ya kutokufurahia maish, hasara ya maendeleo binafsi na hadhi yake katika jamii na kutokuaminiwa kitaaluma.

Hivyo, anaitaka kampuni hiyo imlipe Dola za Marekani 10 milioni (Sh28 bilioni) kama fidia ya hasara halisi na riba kwa kiwango cha mahakama (asilimia) kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kumaliza malipo yote.

Pia, anataka alipwe fidia ya hasara ya jumla kadri mahakama itakavyotathmini, gharama za kesi na nafuu nyingine kadri mahakama itakavyona inafaa.

Kwa mujibu wa hati ya madai katika kesi hiyo, Kabendera ameeleza matukio yaliyojiri katika simu yake kabla ya tukio la kukamatwa kwake, kuwa ilianza kupoteza mawasiliano na kumfanya ashindwe kupata huduma ya mawasiliano.

Pia, Kabendera ameelezea juhudi alizofanya kujua chanzo cha hali hiyo kwa kufanya mawasiliano na mwakilishi wa huduma kwa wateja na hata kutembelea ofisi za kampuni hiyo, lakini hakupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, hali hiyo ilianza Julai 27, 2019, saa 9:00 alasiri alipoiwasha simu yake ambayo alikuwa ameizima tangu jana yake usiku na kwamba ndipo alipobaini kuwa haikuwa na mtandao.

Hivyo aliazima simu nyingine akampigia mtoa huduma kwa mteja kujua mazingira yaliyosababisha kumkatia huduma katika simu yake bila kumjulisha kwanza.

Mwakilishi wa huduma kwa wateja wa Vodacom alimweleza kuwa namba yake ya simu ya Vodacom (+255767456796) ilikuwa na changamoto za kiufundi ambayo ilimhitaji kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja cha karibu kilichopo Tegeta.

Kabendera alimtaka mwakilishi huyo kuelezea tatizo ni nini kabla ya kwenda huko kituoni, lakini mwakilishi huyo alikataa akidai kuwa ni suala nyeti ambalo linamtaka aende binafsi kituoni hapo.

“Hata hivyo, (Kabendera alisita kwenda huko kituo cha huduma kwa wateja) kwa kuwa kulikuwa kina matukio kadhaa ya watu kutekwa ama kutiwa mbaroni walipokuwa wakitembelea kituo cha huduma kwa wateja tangu mwaka 2016,” inasomeka sehemu nyingine ya hati hiyo ya hiyo na kuongeza:

Inaendelea kueleza kuwa Jumatatu, Julai 29, 2019 saa 4:00 asubuhi, Kabendera alipiga tena simu ya huduma kwa wateja akimlalamikia kuwa alikuwa akihitaji kutoa fedha kwenye simu yake hiyo kwa ajili ya kumnunulia dawa mama yake aliyekuwa mgonjwa.

Mwakilishi wa Vodacom aliyemhudumia alimweleza kuwa asubiri kidogo, ili amuulize meneja wake na alirejea dakika chache baadaye na kumweleza kuwa kesi yake ilikuwa nyeti na kwamba ilikuwa juu ya uwezo wao kuitatua.

Badala yake walimshauri atembelee ofisi zao zilizoko Mliman City, asubuhi hiyo.

Hata hivyo saa 9:00 alasiri siku hiyohiyo Julai 29, ghafla simu yake ilianza kufanya kazi, kisha alipigiwa simu na mwakilishi wa Vodacom ambaye alimtaka (Kabendera) amwelezee tatizo lake na baada ya Kabendera kumwelezea kwa takribani dakika tatu, alikata simu akiahidi kumpigia baadaye kidogo.

Baada ya takribani dakika tatu Kabendera alipokea simu iliyopigwa kutoka huduma kwa wateja Vodacom ambayo aliipokea akabaini kuwa ilikuwa ni sauti ya mwanaume, ambaye alimtaka Kabendera aeleze mahali alikokuwa na kwamba simu hiyo ilikuwa ikwaruza kama vile ilikuwa inarekodiwa.

“Kabla ya simu hiyo kukatwa mteja wetu alimsikia huyo aliyempigia simu hiyo akinong’ona kuwa alikuwa nyumbani kwake na kuongeza kuwa sogea karibu na nyumba yake,” inasomeka sehemu nyingine ya hati hiyo ya madai.

Kwa mujibu wa hati hiyo, maelezo hayo yalimstua Kabendera na akakimbia sehemu ya juu ya nyumba yake ambako aliona magari kadhaa ambayo hakuyafahamu, karibu ya nyumba yake.

Kisha lilitokea gari lingine aina ya Toyota Alphard lililoegesha mbele ya magari hayo upande wa kulia mwa nyumba yake, halafu wakashuka watu wanne ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa Polisi, lakini walikataa kutoa utambulisho. Walimpiga pingu kumshikilia kizuizini kwa siku mbili.

Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa wakati wa mahojiano, maofisa wa polisi walifika katika chumba cha mahojiano wakiwa na karatasi zilizochapishwa kutoka katika kompyuta (printout) za akaunti pesa ya simu na za namba simu alizokuwa amezipiga kwa mwaka mzima.

Hivyo walimhoji lengo la kila muamala alioufanya kwa mwaka mzima nyuma yake na pia walimhoji uhusiano wake na watu aliokuwa amewasiliana nao miaka kadhaa.

Kabendera analalamika kuwa polisi na Serikali walitoa taarifa kadhaa zenye mgogoro kwa umma kuhusiana na ‘kutekwa’ kwake na kwamba walimtuhumu kwa kutokuwa raia na kumkashfu Rais (wa wakati huo) John Magufuli.

“Hatimaye alishtakiwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi na matokeo yake walimuweka chini ya ulinzi mkali katika mahabusu ya gereza la Segerea”, inasomeka hati hiyo ya madai na kusisitiza;

“Usikilizwaji wa kesi yake mahakamani uliahirishwa mara 12, huku upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi wa upelelezi”.

Pia inaeleza kuwa kutokana na hali hiyo aliamua kukiri makosa na kulipa fidia ya Sh273 milioni, ili atoke mahabusu na kwamba baada ya kuachiliwa marafiki na familia yake walimweleza kuwa walipigiwa simu na polisi wakiwaonya kutokumtembelea mahabusu, vinginevyo wangepata hatari.

Kabenderea baada ya kutiwa mbaroni nyumbani kwake Mbweni Julai 29, 2019, alishikiliwa kwa wiki nzima, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Agosti 5, 2019 akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Alisomewa mashtaka matatu ya kupanga na kushirikiana na mtandao wa kiuhalifu.

Mashtaka mengine yanayomkabili Kabendera ambaye kwa mujibu wa upande wa mashtaka, licha ya uandishi wa habari pia ni mfanyabiashara, ni la ukwepaji kodi zaidi ya Sh173 milioni na la utakatishaji fedha zaidi ya Sh173 milioni.

Alidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019, alitenda kosa la kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia maslahi.

Katika shtaka la pili la ukwepaji kodi, alidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 19, 2019, mshtakiwa huyo alishindwa kulipa kodi kiasi cha Sh173,247,047.02.

Katika shtaka la tatu la utakatishaji fedha, alidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019, maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, alitakatisha Sh173,247,047.02.

Alidaiwa kutenda kosa hilo, huku akijua kuwa fedha hizo ni mazao ya uhalifu wa kukwepa kodi na kushiriki kupanga uhalifu.

Hata hivyo, Kabendera aliachiliwa huru Februari 24, 2020 baada ya kufanya majadiliano kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ya kukiri makosa yaliyokuwa yanamkabili.

Alipoulizwa na Hakimu Agustine Rwizile kama iliingia katika makubaliano hayo kwa hiyari yake, alikiri hivyo kuwa ni hiyari yake na hakulazimishwa.

Kutokana na kukiri huko Mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh250,000 au kifungo cha miezi mitatu jela akishindwa faini kwa kosa la kwanza kukwepa kodi.

Pia, kwa kosa hilohilo mahakama hiyo ilimhukumu adhabu ya kulipa fidia ya hasara aliyoisababisha, yaani kiasi cha kodi aliyokwepa Sh173,247,047.02.

Kwa kosa la pili (utakatishaji) alimhukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh100 milioni kwa mujibu wa makubaliano baina yake na DPP na kwamba adhabu zote zinakwenda tofauti (haziendi kwa pamoja bali kila moja inajitegemea).

Kabendera alilipa faini Sh 100 milioni ambazo alikuwa ameshazilipa kabla ya makubaliano hayo kufikishwa mahakamani na pia alilipa Sh25,000, hivyo kuachiwa huru.

Related Posts