Mbowe, Prof. Kitila ‘wavaana’

MITIZAMO ya kisiasa kuhusu ugumu wa mtu kuwa mwanachama wa chama cha upinzani hususani Chadema imewagonganisha Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Prof. Kitila Mkumbo baada ya ‘kuvaana’ hadharani. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Majibizano kati ya vigogo hao yamekuja siku moja baada ya aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa na Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Mchungaji Peter Msigwa kuhamia CCM.

Prof. Kitila Mkumbo

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter) jana Mbowe ameandika, kuwa chama cha upinzani hasa Chadema sio suala jepesi, linahitaji ujasiri wa namna ya pekee.

Mbowe amesema viongozi wengi wa upinzani na Watanzania wazalendo wa nchi hii wanapitia nyakati ngumu kutokana na uoga wa serikali ya CCM.

“Marehemu Mzee Lowassa alithubutu kuingia CHADEMA, japo baada ya muda alirudi CCM tunatambua ujasiri wa maamuzi yake.

“Kitu pekee kitakachoikoa Tanzania kutoka kwenye mikono ya watawala ni ujasiri na uthubutu wa mwananchi mmoja mmoja; tuanze sasa kulipigania taifa letu,” aliandika Mbowe.

Hata hivyo, muda mchache baada ya andiko hilo, Prof. Kitila ambaye pia ni mbunge wa Ubungo kupitia CCM, naye alijibu ujumbe wa Mbowe kwa kuandika;

“Makosa ya msingi na ya ki historia ya CDM ni mawili: 1. Kiburi cha kupendwa. 2. Kuamini makosa yao sio yao bali yanasababishwa na watu wengine nje ya CDM (externalization of your problem).

“Ujasiri wa maana kwa sasa ni kukubali kwamba makosa ni ya kwenu na kuanza kuyashughulikia. Pole sana Mr Chair,” amendika Prof. Kitila ambaye aliwahi kuwa kada wa Chadema kabla ya kufukuzwa ndani ya chama hicho kwa tuhuma za usaliti kisha kwenda kuwa mmoja wa waanzilishi wa ACT Wazalendo kabla ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu wizara ya maji kisha kuhamia CCM.

Related Posts