Dar es Salaam. Baada ya mwenyekiti na mfadhili wa zamani wa Yanga Yusuf Manji kufariki Jumamosi iliyopita, aliyekuwa mwanasheria wa timu hiyo, Onesmo Mpinzile ameeleza mengi kumhusu mfanyabiashara huyo.
Manji alifariki akiwa hospitalini Florida nchini Marekani ikiwa ni miezi miwili tangu alipofanya mahojiano marefu na Mwananchi Digital akiwa jijini Dar es Salaam ambapo alihudhuria mchezo wa Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo mtoto wa marehemu Mehbub Manji, alilitumia Mwananchi inasema kuwa mfanyabiashara huyo atazikwa leo saa tisa na kama familia wanashukuru kwa jinsi ambavyo Watanzania wameendelea kuombeleza kifo hicho.
Akizungumzia msiba huo kwa majonzi, mwanasheria huyo ambaye alifanya kazi kwa muda mrefu na Manji, alisema anakumbuka mambo mengi sana ambayo walifanya wakiwa pamoja Yanga.
Mwanasheria huyo ambaye alianza kufanya kazi na Manji tangu akiwa mfadhili wa timu hiyo na baadaye mwenyekiti anasema kiongozi huyo amefariki huku moyo wake ukiwa Yanga.
“Nilianza kufanya kazi na Manji kama mwanasheria wa Yanga na yeye akiwa mfadhili na mwenyekiti wa timu hiyo lakini kati ya kesi au migogoro ya kimpira ambayo niliwahi kufanya naye kwa karibu mojawapo ni mgogoro wa udhamini wa Azam ambao Yanga ilikataa kupokea milioni 100.
“Hoja ya mwenyekiti wakati ule ilikuwa ni Azam nao wana timu kwenye ligi kuu halafu wanadhamini ligi hiyohiyo lakini terms za mikataba haikuwa vile alivyokuwa anataka iwe, nakumbuka tulifungua kesi Mahakama Kuu dhidi ya TFF, Azam na Bodi ya Ligi, hata hivyo kesi hiyo ilifunguliwa na ikaendelea hadi alipoondoka madarakani,” alisema Mpinzile ambaye muda mwingine alikuwa akiongozana na Manji uwanjani.
Hata hivyo, anasema aliwahi pia kufungua kesi kuhusu wachezaji watatu kwenye Ligi Kuu Bara, Bernard Morisson, Mrisho Ngassa, Emanuel Okwi kutokana na usajili wa wachezaji hao.
“Ukichana na ishu ya Azam lakini niliwahi pia kusimamia sakata usajili wa Emanuel Okwi, Yanga, Simba, Simba, Yanga ni sakata ambalo wakati huo lilkuwa na mvuto wa aina yake na mimi nilisimama nikiwa Katibu wa Kamati ya Nidhamu Yanga.
“Lingine lilikuwa sakata la Bernard Morrison, la mara ya kwanza wakati anakwenda Simba akitokea Yanga na Mrisho Ngassa wakati anaondoka Yanga pamoja na mambo mengine,” alisema Mwanasheria huyo maarufu nchini.
Mpinzile anasema mara kwa mara Manji alikuwa akifika hapa nchini lazima amtafute waende wote uwanjani kutazama mechi za Yanga na akiwa Marekani lazima apige simu kuuliza kuhusu Yanga.
“Kwa kweli nilikuwa namfahamu sana na ni mtu ambaye nilikuwa nawasiliana naye mpaka hivi karibuni na hata alipokuwa Marekani alikuwa ananipigia simu kuniuliza Yanga inaendeleaje, naweza kusema moyo wake ulikuwa Yanga.
“Naweza kusema kuwa tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake aliotoa haswa katika klabu ya Yanga, mimi kwa kweli ni shabiki na nimekuwa mwanasheria wake na kila mara nimekuwa nikiamini kuwa kwenye jambo lolote alikuwa mbele zaidi ya wengine,” alimalizia.
Mashabiki wa Yanga watamkumbuka Manji kwa mafanikio makubwa akiwa madarakani ambapo alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne 2012/2013 na mara tatu mfululizo 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017.
Pia alifanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Kagame 2012 likiwa ndiyo kombe la mwisho la michuano hiyo kwa Yanga.
Akiwa na Yanga kipindi chote timu ilifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ingawa haikufanya vizuri sana lakini kipindi chake chote cha uongozi Simba hawakutwa ubingwa wa Bara, anakumbukwa na mashabiki wa timu hiyo kama mmoja kati ya viongozi wenye mafanikio makubwa zaidi Jangwani lakini akiwa mmoja kati ya watu walioleta mapinduzi ya soka Tanzania.
Manji ambaye aliingia madarakani siku chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0 na Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Mei 6, 2012 alifanya kazi kubwa kipindi cha uongozi ikiwamo kuhakikisha anavunja makundi mawili makubwa yaliyokuwa yanapingana ndani ya timu hiyo moja likiitwa Yanga Asili na lingine Yanga Kampuni.
Mwenyekiti huyo aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017 baada ya kukwaruzana na wazee wa timu hiyo akiwemo marehemu Yahaya Akilimali, anakumbukwa kwa kufanikiwa kuwasajili wachezaji wakubwa kama Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Emannuel Okwi, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa na Donald Ngoma kwenye kikosi chake.
Mbali na wachezaji mahiri ambao walisajiliwa, Manji pia aliajiri makocha kadhaa wakubwa wakiwemo Konstadin Papic, Milutin Sredojevic ‘Micho’, Sam Timbe, Ernest Brandts, Marcio Maximo, George Lwandamina na Tom Santifiet na kuleta mabadiliko makubwa katika soka la Tanzania.