Musoma. Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Manispaa ya Musoma mkoani Mara, wamefunga milango ya kuingia sokoni hapo, wakishinikiza kuondolewa kwa wafanyabiashara ndogondogo ‘machinga’ wanaofanya shughuli zao kuzunguka soko hilo.
Wafanyabiashara hao wamegoma kuingia sokoni wakidai mazingira ya kufanya biashara sio rafiki.
Wakizungumza wakiwa nje ya soko hilo leo, Jumatatu, Julai mosi, 2024, wamesema hawatafungua milango ya kuingia sokoni hapo hadi maombi yao yatakapofanyiwa kazi.
Milango mitatu ya kuingia sokoni humo imefungwa kuanzia saa 2 asubuhi, huku kukiwa hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia ndani ya soko.
Mfanyabiashara Enock Samson amesema wanashindwa kufanya biashara kutokana na machinga kuzunguka soko hilo, huku bidhaa wanazouza ni sawa na biashara zinazouzwa ndani ya soko.
“Hakuna mtu anataka kuingia sokoni kununua mboga mboga, matunda, nyanya, vitunguu kwa sababu wenzetu wapo getini na mamlaka husika zinaona,” amesema Samson.
Amesema uwepo wa machinga hao nje ya soko kunawasababishia wao kukosa wateja, hivyo ni vema Serikali ikatenga maeneo maalumu mbali na eneo la soko kwa ajili ya machinga hao.
Mfanyabiashara mwingine, Ally Kansolele amesema mazingira magumu ya biashara yanawafanya washindwe kufanya biashara na kufunga vibanda vyao.
“Watu wamekopa wanatarajia, sasa hayo marejesho utayapataje wakati hakuna wateja, wateja wote wanauziwa nje,” amesema Kasonsole.
“Wateja wenye magari hawawezi kuingia sokoni kwa sababu wakipaki wanatakiwa kulipia ushuru Sh1,000 wakati wakifika kwa machinga wananunua vitu wakiwa kwenye magari,” ameongeza Zubeda Mafuru.
Ameeleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakiiomba mamlaka husika kuwatengenezea mazingira rafiki kwa ajili ya wao kufanya biashara, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.
“Sisi tunalipa ushuru, tunalipia vibanda na huduma zingine, wenzetu machinga hawalipi chochote, hivi hapo kuna usawa? Utaratibu ufanyike, aidha nasi tutoke nje ya soko tuweke vitu vyetu barabarani au wao waingie sokoni tuwe na mazingira sawa ya kufanya biashara,” amesema.
Baadhi ya machinga wamesema wanalazimika kupanga bidhaa zao katika eneo hilo kwa lengo la kutafuta wateja na si kuwazuia wenzao wa sokoni kuuza.
“Tunatafuta riziki, sio kwamba tumekuja kuwaharibia hapa na ukumbuke sote tunachukulia mzigo sehemu moja, kwa hiyo hapa tupo kwa lengo la kuwatafuta wateja na hakuna mteja anazuiliwa kuingia sokoni,” amesema Emmanuel John.
Kuhusu eneo la maegesho lenye umbali wa takriban mita 800 kutoka Soko Kuu ambalo limetengwa kwa ajili ya machinga, wamedai eneo hilo sio rafiki, huku wakidai liko mbali na watu.
“Pale kuna baa, unakuta mtu anatoka kunywa pombe huko anakuja kufanya fujo kwenye biashara, lakini pia kule hakuna wateja. Sisi ni machinga, tunapaswa kuwafuata wateja na sio wateja kutufuata,” amesema Eliya Marwa.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema amepokea taarifa za mgomo huo na ameahidi kufika eneo la soko kuzungumza na wafanyabiashara hao.
Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa taarifa zaidi.