Mtendaji wa kijiji aliyehukumiwa kwa kupokea rushwa ya Sh20,000 akwaa kisiki

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo Moshi, imebariki adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela bila faini au faini ya Sh1.5 milioni kwa aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Sanyajuu wilayani Siha, Deogratias Moshiro aliyehukumiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh 20,000.Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, ilimuhukumu adhabu hiyo baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha aliomba na kupokea rushwa hiyo kutoka kwa Peter Mwenda, aliyekwenda ofisini kwake kuchukua barua kwa ajili ya kwenda kumdhamini kijana wake aliyekuwa akishikiliwa katika Kituo cha Polisi Sanya Juu.Alikata rufaa kupinga hukumu hiyo, lakini Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa Juni 26, 2024 na Jaji Adrian Kilimi, imebariki hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi.Jaji Kilimi katika hukumu hiyo amesema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, ameridhika kwamba mrufani (Deogratias) alitiwa hatiani na kuhukumiwa ipasavyo, hivyo akatupilia mbali rufaa yake.Rufaa hiyo ya jinai namba 68/2023 ilitokana na kesi ya jinai namba 31/2022 ambapo mrufani huyo alishtakiwa alidaiwa kutenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 15(1) (a) na (2) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 329 marejeo ya 2022.Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, kijana hiyo alikamatwa na askari Polisi Agosti 15, 2022 akituhumiwa kuchunga ng’ombe katika shamba la mtu, hivyo kutakiwa kuwasilisha barua za utambulisho kutoka kwa ofisi ya Mtendaji wa Kijiji, ili apewe dhamana.Mwenda baada ya kufika kwenye ofisi hiyo hakupata barua baada ya mtendaji huyo kutaka apewe kiasi hicho cha fedha ambacho hakuwa nacho, hivyo ilimlazimu kwenda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa msaada zaidi.Takukuru iliweka mtego kwa kumkabidhi Mwenda fedha hizo, kisha akaelekea ofisini kwa mrufani ambaye baada ya kupokea kiasi hicho cha fedha alimuandikia barua aliyoihitaji, kisha akakamatwa na maofisa wa taasisi hiyo akiwa na fedha hizo.Hivyo alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo.Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita na vielelezo vitano ambapo katika utetezi wake mrufani alikanusha kuomba fedha hizo na kudai zilitupwa mezani kwake na shahidi wa kwanza wa jamhuri, lakini Mahakama ya Hakimu Mkazi ilitupilia mbali utetezi wake huo, kumtia hatiani na kumbukumbu adhabu hiyo. RufaaDeogratias katika rufaa yake alitoa sababu  sita kupinga  hukumu hiyo, miongoni mwa sababu hizo ni kuwamahakama ya chini ilikosea kisheria kumtia hatiani na kumuhukumu kwa ushahidi wa upande wa mashtaka aliodai ulikuwa unakinzana.Sababu nyingine alidai kuwa mahakama ya chini ilikosea  kisheria kumtia hatiani na kumhukumu mrufani kwa kosa aliloshtakiwa bila kuzingatia ukiukwaji wa utaratibu wa kumkamata na kumsaka mrufani, mahakama hiyo kumtia hatiani bila ushahidi wa mashtaka kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka.Pia alidai kuwa mahakama ya chini ilikosea kisheria kumtia hatiani bila kuzingatia ushahidi wa mashtaka ambao ulishindwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka na kuwa mahakama hiyo haikuzingatia ushahidi wake alioutoa mahakamani hapo.Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Deogratias aliwakilishwa na wakili wa utetezi, Elia Kiwia huku mjibu rufaa aliwakilishwa na Wakili Framk Wambura.Wakili Kiwia alidai kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani mapema kwa sababu hakuna hatua za kinidhamu zilizochukuliwa kabla ya kumshtaki mrufani.Hivyo alidai kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Maadili na Maadili ya Utumishi wa Umma, rushwa inatajwa kuwa ni miongoni mwa vitendo visivyo vya kimaadili vinavyovutia kuchukuliwa hatua za kinidhamu.Pia alidai kwa mujibu wa Kanuni za Wilaya ya Siha (Kanuni za kudumu za halmashauri ya Siha) chini ya aya ya 35 masuala ya nidhamu kwa watumishi wa halmashauri yanatakiwa kushughulikiwa na halmashauri na kuomba kubatilisha shauri hilo na kumwachia huru mrufani.Vilevile, Wakili Kiwia alidai kuwa  ushahidi wa shahidi wa kwanza ulikuwa wa mashaka kwa sababu alisaini kwa jina la Peter, lakini iliandikwa Peteli kwa sababu hajui kusoma na alifundishwa na mjukuu wake.Alihitimisha kwamba mrufani hapaswi kutiwa hatiani kwa udhaifu wake wa kujitetea, bali kwa nguvu ya upande wa mashtaka, hivyo kasoro hizo zinapaswa kutatuliwa kwa manufaa ya mrufani, na kuomba mrufani aachiwe huru.Akijibu hija hizo, Wakili Wambura alidai uwa ilikuwa sahihi kesi hiyo kupelekwa mahakamani kwa sababu kosa lililokuwa linamkabili mrufani ni kosa la jinai na haliwezi kutatuliwa kwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.Kuhusu kuthibitishwa kwa kosa hilo, alidai kiwa ushahidi ulionyesha namna shahidi wa kwanza alivyowasiliana na mrufani kwa ajili ya barua ya utambulisho na mrufani kuomba Sh20,000 na Takukuru iliweka mtego na kuwa hakujatolewa ushahidi kuwa shahidi huyo hajui kusoma.Wakili Wambura alidai kuwa mahakama hiyo ilizingatia utetezi na ikajiridhisha kuwa mrufani alichukua fedha hizo kama rushwa, hivyo kuomba mahakama itupilie mbali rufaa hiyo. HukumuBaada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Kisanya katika hukumu hiyo amesema hakuna ushahidi kwenye rekodi kwamba kulikuwa na mashtaka yoyote ya kiutawala au ya madai ambayo yalianza kabla ya mrufani kushtakiwa kwa jinai.Jaji Kilimi amesema kuwa kwa mtazamo wake, fedha hizo Sh20,000 zilikutwa kwa mrufani baada ya kuwekewa mtego uliofanywa na maofisa wa Takukuru.Amefafanua kuwa katika kupima msingi wa mwenendo, akinukuu kesi ya mahakama ya rufani kuhusu uaminifu wa shahidi unaweza kuamuliwa hata  na mahakama ya rufaa ya pili wakati wa kuangalia matokeo ya uchunguzi wa maamuzi ya mahakama ya rufaa ya kwanza.Kuhusu madai ya mrufani kutishiwa wakati anatoa maelezo yake ya onyo, Jaji Kilimi amesema kwa maoni yake katika suala hilo kulikuwa na dosari kwa  mahakama ya awali kutokufanya kufanya uchunguzi au kesi ndani ya kesi ili kuthibitisha kama ilikua hiari au la, baada ya mrufani(mshtakiwa) kuyakana.”Baada ya kuangalia mwenendo na kuuchambua, naona utaratibu uliopitishwa na mahakama ya awali uliingia dosari, hivyo maelezo ya onyo yaliyokubaliwa kama kielelezo cha nne inafutwa kutoka kwenye rekodi ya mahakama ya awali, hivyo nakubali sababu hiyo, moja”amesema.Kuhusu hoja ikiwa utetezi wa mrufani ulizingatiwa, Jaji Kilimi amesema amezingatia hukumu ya mahakama ya awali si kwa  kueleza ushahidi wa mrufani, bali ameichambua katika kielelezo katika ukurasa wa 15 wa hukumu ya mahakama ya mwanzo iliyopigwa chapa na kuridhika kwamba utetezi ulizingatiwa kwa makini na mahakama ya awali ambapo alitupilia mbali hoja nyingine tano.”Kusuluhisha mtazamo wa utetezi wa mrufani katika kesi hiyo kama ulivyopatikana kwa haki na mahakama ya kesi, hiyo hiyo haikuleta shaka yoyote ambayo inaweza kuathiri ushahidi wa mashtaka,” amesema.Jaji amesema baada ya kupitia hoja zote sita za upande wa mrufani ameridhika kwamba mrufani alitiwa hatiani na kuhukumiwa ipasavyo na kuwa haoni sababu ya kubatilisha uamuzi wa mahakama ya awali, hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo.

Related Posts