Mwanachama wa Chadema adaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Handeni

Handeni. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati matukio ya baadhi ya wananchi kupotea kwa madai ya kutekwa na watu wasiojulikana.

Amesema bila hatua kuchukuliwa, inaweza kusababisha machafuko siku zijazo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika jana Jumapili, Juni 30, 2024 katika viwanja vya Handeni Square wilayani Handeni, mkoani Tanga, Lema amesema wamepata taarifa za kupotea kwa mwanachama wa chama hicho, Kombo Mbwana, tangu Jumamosi ya Juni 29, 2024 na hajaonekana mpaka sasa.

Hivyo, Lema amesema Serikali inapaswa kulifanyia kazi suala hilo kwa haraka, kwa sababu familia za wahusika zinateseka na ni matukio yasiyokubalika ndani ya jamii.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku chache tangu kuripotiwa kutoweka kwa Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa jijini Dar es Salaam na kupatikana Juni 27 katika pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha mwilini, alionekana katika video fupi iliyosambaa katika mitandao ya kijamii akiomba msaada wa kupelekwa hospitali huku akivuja damu na kulalamikia maumivu makali kutokana na kipigo.

Kijana huyo kwa sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam na ripoti ya awali ya vipimo imeonyesha amepata mpasuko wa taya zilizosagika, huku baadhi ya mifupa ikionekana na mipasuko midogo.

Akiendelea kuzungumza katika mkutano huyo, Lema amesisitiza kuwa matukio ya wananchi kutekwa hayaleti taswira nzuri kwa Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Tunaitaka Serikali ichukue hatua hraka na za madhubuti, ili kuepusha machafuko yatayosababishwa na hali hii,” amesema.

Ameonya kuwa siasa isiwe sababu ya wananchi kutekwa na kupotea, badala yake watu washindane kwa hoja na kuendelea na maisha yao kwa amani.

“Nimuombe Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan), haya mambo ya watu kupotea Serikali yake iweke mkakati wa kuyakomesha. Yasichukuliwe kirahisi, yatakuja kuchafua nchi. Yatatengeneza waasi na watu wataanza kujitoa mhanga, ache kutengeneza kizazi cha hasira ambacho siku kikiamua kulipa kisasi kutakuwa na hali mbaya,” amesema Lema.

Naye Katibu wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Kombo Matulu amedai ofisi yake kupokea taarifa za mwanachama wao kupotea na wamefuatilia sehemu mbalimbali, lakini hawajapata majibu kuhusu mahali alipo.

Amesema wanahitaji kujua Kombo yuko wapi, na nani, na nini kimemsababisha kupotea ili familia ipate amani.

Mama asimulia mwanawe alivyotekwa

Mwananchi imezungumza na mama mzazi wa Kombo, Hellena Joseph aliyesema Jumamosi, Juni 29, 2024, alienda nyumbani kwa Kombo asubuhi kumsalimia, lakini akapewa taarifa na mkewe kuwa Kombo hayupo.

Anasema mkewe alimwambia kuna watu walifika nyumbani hapo wakidai lile eneo wanaloishi ni la kwao, hivyo wakamchukua kwa nguvu na kuondoka naye.

“Aniliambia katika mabishano hayo, walimchukua kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari, kuondoka naye,” amesimulia mama huyo.

Hellena amesema tangu siku hiyo wamemtafuta bila mafanikio, licha ya kutoa taarifa polisi.

Jana usiku, Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi kwa simu ili alizungumzie hilo, lakini simu ilipokelewa na msaidizi wake akidai yupo kwenye kikao.

Hata hivyo, baada ya kutafutwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando, amekiri kuwapo kwa tukio hilo na linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya dola na taarifa zitatolewa.

“Ni kweli taarifa za kutekwa kwa Kombo tunazo na tayari Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi,” amesema Msando.

Ameihakikishia familia ya Kombo kuwa Serikali inaendelea kufuatilia tukio hilo na kwamba suala hilo lisitumike kisiasa kwa sababu huo ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine.

Matukio yaliyowahi kutokea

Mapema mwaka huu, Mwananchi liliripoti mfululizo wa matukio ya watu kudaiwa kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha yaliyotokea kwa nyakati tofauti.

Miongoni mwa matukio hayo, baadhi yaliibuka katika mikutano ya hadhara iliyokuwa ikifanywa na aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda. Katika ziara hiyo Makonda alikumbana na kero za watu kutekwa na kupotea kwa nyakati tofauti.

Hata hivyo, kumbukumbu zinaonyesha matukio ya aina hii yalianza kuibuka mwaka 2021 na kuendelea na kuleta taharuki kwa familia husika na wananchi ambao wanahoji, Jeshi la Polisi lenye dhamana ya ulinzi wa wananchi na mali zao linayadhibiti vipi.

Miongoni mwa matukio hayo ni la kutekwa kwa aliyekuwa mfanyabiashara na fundi simu eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, Innocent Elias Liveti (34) maarufu Macheni. Liveti likuwa amekaa mbele ya duka lake lililopo Mtaa wa Narung’ombe, walitokea watu wawili waliovalia kofia na kuingia naye ndani ya gari na kuondoka naye.

Tukio lingine ni la kutekwa kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, aliyekuwa akimiliki kampuni ya Mziba Empire Investment Ltd yenye ofisi zake Mikocheni, Dar es Salaam. Mziba alitekwa na watu wawili waliofika ofisini kwake saa 2 usiku Desemba 7, 2023 wakijitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi. 

Matukio hayo yalitanguliwa na kutoweka kwa Charles Wetinyi, aliyedaiwa kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi eneo la Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara Oktoba 23, 2023. 

Pia, Wilson Damas alitoweka tangu kampeni za uchaguzi mwaka 2020 sasa ni zaidi ya miaka mitatu hajulikani pamoja na Richard Kayanda, wote wakazi wa Nyandoto Tarime, Mkoa wa Mara.

Wengine waliopotea kwa pamoja Desemba 26, 2021 ni waliokuwa mafundi simu na wafanyabiashara katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam waliodaiwa kutekwa na watu waliokuwa wamevaa sare za polisi.

Vijana hao ni pamoja na Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe na siku ya mwisho mmoja wao alituma ujumbe wa mfupi wa simu ukieleza wamekamatwa maeneo hayo wakiwa kwenye gari IST nyeusi na wanapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Related Posts