Nyumba 76 za watumishi wa afya, zitakavyoboresha utoaji huduma

Unguja. Familia 76 zimepata makazi karibu na Hospitali ya Rufaa ya Abdalla Mzee, Kusini Pemba hatua inayotajwa kuongeza ufanisi wa kutoa huduma katika hospitali hiyo baada ya kuwaepusha wataalamu kutembea masafa marefu kwenda kutoa huduma.

Nyumba hizo 76 zenye gharama ya Sh16.481 bilioni zimejengwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na kuikabidhi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Itakumbukwa mwaka 1969, China ndio ilijenga na kuizindua hospitali hiyo kwa mara ya kwanza huku wakiendelea kuipatia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) msaada wa madaktari wa fani mbalimbali na vifaa vya huduma za afya kwa zaidi ya miaka 54 sasa.

Akizungumza leo Jumatatu, Juni Julai Mosi, 2024 wakati wa kuzindua nyumba hizo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hatua hii ya kujenga makazi ya wafanyakazi karibu na hospitali ili kuwapunguzia masafa na kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi, ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali anayoiongoza.

Amesema China kuwajengea nyumba hizi chini ya mkandarasi kampuni ya Zhengtai Group, ni uthibitisho mwingine wa kuendeleza urafiki na uhusiano mwema uliopo baina ya nchi hizo mbili.

“Fedha hizo zimetumika katika kujenga nyumba nne za ghorofa. Nyumba hizi zitahudumia familia 76 zikijumuisha nyumba 52 za chumba kimoja kimoja kinachojitegemea na nyumba 24 za vyumba viwili viwili vinavyojitegemea,” amesema Dk Mwinyi

Amesema, “tuna kila sababu ya kuishukuru na kuipongeza Serikali ya watu wa China kwa kuunga mkono vipaumbele muhimu vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hususan katika sekta hii ya afya.”

Dk Mwinyi amesema ni mategemeo ya Serikali makazi hayo yatatoa fursa kwa wafanyakazi hao kupata hifadhi na muda mzuri wa kupumzika badala ya kufikiria usafiri wa kwenda na kurudi umbali mrefu.

Kiongozi huyo wa nchi amesema kipindi kifupi kijacho, wataweka mawe ya msingi katika ujenzi wa nyumba nyingine za wafanyakazi kwa upande wa Pemba zikijumuisha hospitali za Kinyasini iliyopo Wilaya ya Wete, ya Vitongoji kwa wilaya ya Chakechake na Hospitali ya Micheweni.

Kwa upande wa Unguja, Serikali inajenga nyumba za wafanyakazi katika Hospitali ya  Kitogani iliyopo  Wilaya ya Kusini, Hospitali ya Mwera Pongwe, Wilaya ya Kati na Hospitali ya Pangatupu kwa Wilaya ya Kaskazini B.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, baada ya kukamilika miradi hii, watakuwa wameondokana kwa kiasi kikubwa tatizo la kukosekana kwa makazi ya watumishi wa afya, kunakosababisha kuzorota kwa utoaji wa huduma kwa wakati katika hospitali hizo.

“Natoa wito kwa uongozi wa Wizara ya Afya na kwa wafanyakazi watakaoishi katika nyumba hizi kuhakikisha zinatunzwa kwa kuzingatia  kuwa gharama zilizotumika kujenga majengo haya ni kubwa.

Naye Waziri wa Afya, Ahmed Mazrui amesema Watahakikisha wanasimamia nyumba hizo ili ziweze kutumika kwa muda mrefu, jambo litakalosaidia kuboresha huduma za afya kisiwani humo.

Related Posts