WATOTO wa mjini wanasema biashara asubuhi na jioni mahesabu, ndio kauli waliyoitumia Yanga kukamilisha dili la kiungo Clatous Chama ambaye ametua kwa mabingwa hao na tangu jana ndio gumzo mitandaoni na kwenye vijiwe vya michezo.
Chama amesaini mkataba wa miaka miwili na Yanga baada ya mkataba wake kumalizika na Simba akigoma kuongeza mwingine sababu kubwa ikitajwa kuwa ni masilahi pamoja na kejeli za hapa na pale.
Yanga haikuwa imepanga kumtambulisha jana kama ambavyo ilifanyika, lakini hatua hiyo ilitokana na matajiri hao kupokea simu kutoka kwa kiungo huyo kuwa Simba imepata uhakika amesaini upande wa pili.
Kila kilichokuwa kinaendelea usiku wa Jumapili baina ya Chama na viongozi wa Simba, alikuwa anakishusha kwa Yanga kama kilivyo na ndiye aliyewashauri waachie picha yake asubuhi kabla ya chai kama kitendo cha kuwanyamazisha Simba ambao anatafsiri hawakumheshimu.
Ukweli mwingine ni kwamba aliwaambia rafiki zake anataka kucheza Ligi ya Mabingwa na Yanga inaonyesha uelekeo wa kufika mbali.
Simba baada ya kupata taarifa hiyo matajiri wake kuanzia Juni 30 walirudi mezani wakihaha kumbakisha kiungo huyo kwa gharama yoyote wakimuwekea fedha mara mbili ya zile alizochukua Yanga, lakini ngoma ikadunda.
Yanga baada ya kupata taarifa hiyo na kujiridhisha ikaona hapana kabla ya watu hawajapata kifungua kinywa isambaze picha hizo akisaini ambazo ziliwatibua zaidi mabosi wa Simba.
Hata hivyo, Simba haikukata tamaa mpaka jana mchana baadhi ya vigogo waliendelea kusukuma kete ya mwisho kwa Chama wakimtaka akubali kusaini mkataba kisha wao wanajua namna gani watakwenda kumalizana na watani wao, lakini mambo yakadunda.
Saa chache baada ya Yanga kumtangaza Chama, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephanie Aziz KI aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram akimkaribisha.
Azizi Ki ndiye aliyeongoza mashambulizi kwa mabosi wa Yanga akiwataka kukisuka kikosi kwa kushusha wachezaji bora zaidi. Ikumbukwe pia Khalid Aucho aliwahi kunukuliwa msimu uliopita akisisitiza atamani kucheza na Chama kwenye timu yoyote kwani anajua sana na anafanya mchezo kuwa rahisi.
Kocha wa zamani wa Yanga, Nasredine Nabi aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa aina ya usajili ambao Yanga imeufanya sio taarifa njema kwa wapinzani wao kwenye ligi.
Nabi alisema usajili wa Chama utakwenda kuleta shida zaidi akiunganika na anaowakuta Aziz KI na Pacome.
“Nimeshtuka sana kusikia huu usajili wa Chama, nilidhani kwamba anaweza kubaki Simba kama ilivyokuwa nyuma, nadhani Yanga inakwenda kuwa na timu bora zaidi, hii siyo nzuri kwa timu pinzani,” alisema Nabi ambaye anaondoka FAR Rabat na kwenda kujiunga na miamba ya Afrika Kusini Kaizer Chiefs.
“Kila mtu anamjua Chama, ni mchezaji bora aliyezaliwa na kipaji kikubwa miguuni kwake, hapa unatakiwa kupima anakwenda kuiunganika na Aziz KI,Pacome na Maxi utaona namna timu hiyo itakavyokuwa na makali zaidi,”aliongeza Nabi.
Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii kuhusiana na usajili huu.