TETESI ZA USAJILI BONGO: Sangana asakwa Yanga, Yakubu kutua Coastal Union

UONGOZI wa Yanga umeanza kumfuatilia kiungo raia wa DR Congo, Onoya Sangana Charve anayekipiga AS Maniema.

Nyota huyo aliyejiunga na Maniema Julai 28, 2022 akiachana na OC Renaissance du Congo anamudu kiungo mshambuliaji na uzuiaji. Yanga inamtaka akaungane na Maxi Nzengeli.

COASTAL Union ‘Wagosi wa Kaya’ wameanza mazungumzo na beki wa kati wa Stade Malien ya Mali, Issah Yakubu.

Coastal inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao inamtazama Issah kama mbadala sahihi wa Lameck Lawi aliyejiunga na Simba, japo Rayon Sports na APR za Rwanda zinadaiwa kumtaka pia.

SINGIDA Black Stars, iko mbioni kukamilisha uhamisho wa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), Seleman Mwalimu anayeichezea KVZ.

Nyota huyo wa zamani wa Fountain Gate msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Zanzibar alikofunga mabao 20 na kuasisti saba katika michezo 27 anatajwa kuzitosa Dodoma Jiji na Kagera Sugar.                                 

PAMBA Jiji imeanza mazungumzo ya kumpata nyota mshambuliaji wa Gor Mahia Mkenya, Benson Omala kwa msimu ujao. Mwakilishi wa mfungaji bora wa Kenya msimu uliopita akifunga mabao 19, inaelezwa tayari wamefanya mawasiliano na viongozi wa Pamba ili kumpata nyota huyo aliyewindwa misimu kadhaa na Azam na Simba.

MAAFANDE wa Tanzania Prisons, wameanza mazungumzo ya kupata saini ya winga, Haruna Chanongo ambaye ni mchezaji huru. Chanongo aliyewahi kutamba na Simba, Stand Utd, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting, amemaliza mkataba Pamba Jiji aliyoipandisha Ligi Ku. Mabosi wa Pamba pia wanapambana kuhakikisha anabaki.                 

DODOMA Jiji iko mbioni kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa nyota wa Mashujaa FC, Reliants Lusajo baada ya mkataba wake kumalizika katika kikosi cha maafande wa mkoani Kigoma. Nyota huyo aliyefunga mabao manane msimu wa Ligi Kuu Bara uliopita alikuwa na mkataba wa miezi sita na Mashujaa na hakuna mazungumzo mapya ya kumuongezea mwingine.

KLABU ya JKT Tanzania huenda isiendelee na beki wa kati wa kikosi hicho, Wema Sadoki baada ya mazungumzo ya mkataba mpya kugonga mwamba. Nyota huyo wa zamani wa Ihefu SC na Alliance FC inaelezwa kwamba huenda akaondoka ili kupisha sura mpya ndani ya kikosi hicho, huku Tanzania Prisons nayo ikitajwa kwamba inamnyemelea pia saini yake.

Related Posts