Dar es Salaam. Wakati wananchi mbalimbali wakiendelea kumchangia Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeungana na wadau hao kufanikisha matibabu ya Sativa aliyelazwa Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam.
Sativa anayedaiwa kutoweka Juni 23 na kupatikana Juni 27, 2024 katika pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha mwilini, anaendelea na matibabu Aga Khan yaliyoanza usiku wa Juni 30, 2024.
Ripoti ya awali ya vipimo inaonyesha Sativa amepata mpasuko wa taya zilizosagika, huku baadhi ya mifupa ya ikionekana na mipasuko midogo.
Kwa mujibu wa mwendeshaji wa harambee ya kufanikisha matitabu ya Sativa kupitia mitandao ya kijamii, tangu Juni 27, 2024 wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh10 milioni zilizochangwa na wadau mbalimbali.
Leo Jumatatu Julai mosi, 2024, Mratibu wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa amemtembelea Sativa katika Hospitali ya Aga Khan na kusema taasisi hiyo ipo bega kwa bega katika kufanikisha matibabu yake wakishirikiana na wadau wengine.
Ole Ngurumwa amesema jitihada za kunusuru maisha ya Sativa zinaendelea vema, huku akiwashukuru Watanzania kwa kuonyesha moyo wa ukarimu wa kupaza sauti kwa watu wanaodaiwa kutoweka au kutekwa, ili kuhakikisha wanapatikana.
“THRDC tumekuwa tunawasaidia watu mbalimbali, tumefuatilia suala la Sativa tangu alivyopotea, kuna nyingi za kufuatilia kuna wengine walipaza sauti, lakini sisi tulitumia njia nyingine na matatibu yake tunahusika kwa namna moja au nyingine.
“Tunataka kuhakikisha Sativa anapata matibabu sahihi yenye ubora iwe ndani au nje ya nchi, THRDC kazi yetu tunahusika katika hilo. Kama Watanzania wanaendelea kuchanga ni jambo jema fedha hizo zitamsaidia katika shughuli nyingine kumbuka kwa muda mrefu atakuwa kitandani kujitibu,” amesema.
Kwa mujibu wa Ole Ngurumwa, amezungumza na Sativa aliyemueleza kuumia zaidi maeneo ya kichwa alikopigwa risasi ya shingo iliyotokea katika shavu la kushoto.
“Uchunguzi wa awali wa madaktari umeonyesha maeneo hayo yamesagika na itamlazimu kufanyiwa upasuaji mkubwa, ili kurekebisha maeneo yaliumizwa na risasi. Tunaomba Watanzania kuwa na subira wakati tukiendelea kumuuguza Sativa,” amesema Sativa.
Sativa anayejishughulisha na biashara ya miamala ya fedha na michezo ya kubahatisha, alifikishwa Aga Khan usiku wa kuamkia jana Juni 30, 2024 akitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikofikia awali akitokea mikoa ya Dodoma na Katavi.
Baada ya kupatikana kwa Sativa Juni 27 alipekelewa kituo cha Afya Mpimbwe, kisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa huduma za kwanza, huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani akitangaza kuanza uchunguzi dhidi ya tukio hilo.
Jana Jumapili Juni 30, 2024 mratibu wa matibabu ya Sativa, Martin Masese maarufu ‘MMM’ amesema ripoti ya awali ya vipimo walioelezwa na madaktari imeonyesha kuwa ndugu yao ameonekana kuwa na alama za michubuko ya panga katika mikono yake.
“Alikuwa anapigwa mabapa ya mapanga, sasa kuna moja lilimpata katika mikono yake, lakini tunashukuru timu za madaktari wote waliompa huduma ya kwanza hadi tulipofikia hapa,” amesema.
“Hivi ni vipimo na matokeo ya awali, lakini atafanyiwa vipimo vingine vikubwa, ili kujua kila alipoumia au anaposikia maumivu, hatimaye apate matibabu ya uhakika, tunamshukuru Mungu hali yake inaendelea kuimarika kila kukicha,” amesema Masese.