Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania limetangaza ongezeko la safari za treni ya kisasa (SGR) zitakazohusisha kuanza kwa treni mpya ya mwendo kasi (Express train) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro bila kusimama vituo vya kati.
Ratiba iliyotolewa inaonyesha kutakuwa safari nane kwa siku na treni hizo zitakuwa zinapishana kwa takribani dakika 20 kati ya treni ya kawaida na ile ya mwendokasi.
Ongezeko la safari hizo limekuja ikiwa siku 16 zimepita tangu kuanza kwa safari za treni hiyo ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo zilikuwa safari nne kwa siku.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRC leo Jumatatu Julai mosi, 2024, kupitia kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Jamila Mbarouk mabadiliko hayo yataanza rasmi Julai 5, 2024.
“Ongezeko la safari litahusisha kuanza kwa treni mpya ya haraka (express train), ambayo itakuwa inafanya safari kati ya Dar es Salam hadi Morogoro bila kusimama vituo vya kati,” amesema.
Amesema treni ya haraka itakuwa inaondoka Dar es Salaam kuanzia saa 12:20 asubuhi na saa1:30 usiku, wakati huo treni ya kawaida itakuwa inaondoka Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi na saa 10:00 Jioni.
“Treni ya kawaida itakuwa inaondoka Morogoro saa3:50 asubuhi na saa 10:20 jioni. Abiria wanashauriwa kukata tiketi kwa njia ya mtandao au madirisha ya tiketi yaliyopo ndani ya vituo vya treni hiyo saa mbili kabla ya muda wa safari, ili kuepuka msongamano,” amesema.