Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo amekata rufaa katika kamati ya rufaa ya chama hicho, kupinga uchaguzi uliofanyika, akidai kutoridhika na matokeo.
Mbali na kutoridhika na matokeo, Doyo ameituhumu kamati ya uchaguzi pamoja na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hamad Rashid Mohamed, kwa kukiuka katiba na kanuni za chama hicho.
Juni 29, 2024, chama hicho kilifanya uchaguzi mkuu wa nne na baadhi ya viongozi wamemaliza muda wao wa kipindi cha miaka 10, kwa mujibu wa katiba akiwemo aliyekuwa mwenyekiti Hamad Rashid Mohamed.
Katika uchaguzi huo, Shabani Itutu aliibuka mshindi kwa nafasi ya Mwenyekiti Taifa kwa kupata kura 121 dhidi ya Doyo aliyepata 70, huku kura moja ikiharibika. Kura zilizopigwa zilikuwa 192.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu Julai mosi 2024, jijini Dar es Salaam, Doyo amesema amekata rufaa kwa mujibu wa kanuni za chama za mwaka 2019 kanuni ndogo ya tatu, inayozungumia haki ya rufaa ambayo itatolewa kwa mgombea.
“Sheria hii inamtaka atakayekata rufaa kuwasilisha kusudio ndani ya saa 24 baada ya uchaguzi na baadaye rufaa yenyewe ambayo yote tumeshayafanya,” amesema Doyo.
Kwa mujibu wa Doyo, sababu ya kukata rufaa ni kuwa mkutano wa uchaguzi kuongozwa na mwenyekiti anayemaliza muda wake, Hamad Rashid Mohamed badala ya wajumbe kumchagua mwenyekiti wa muda.
Sababu nyingine ni mwenyekiti wa muda baada ya kupatikana ataendesha uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa kudumu na baada ya hapo, atamkabidhi kiti kwa ajili ya uchaguzi wa makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar.
“Hapa katiba ilivunjwa, mwenyekiti anayemaliza muda wake aliongoza kikao kile kinyume na katiba, na hata alipopatikana hakumkabidhi kiti kuendelea na majukumu yake,” amesema Doyo.
Aidha, Doyo amesema sababu nyingine ni msimamizi kutowapa nafasi wapigakura, kinyume na kifungu na kwa kuwasimamia na kuwaelekeza nani wakumpigia kura.
“Tunapiga matokeo yote ya uchaguzi pamoja na uendeshaji wake na utangazaji wa matokeo, yalifanyika mbele ya Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa,” amesema.
Katiba ya ADC toleo la mwaka 2019 ibara ya 37 ngazi ya Taifa kifungu cha (xii) kinaeleza Mkutano Mkuu wa Taifa wa Uchaguzi utaongozwa na Mwenyekiti wa muda hadi pale uchaguzi utakapokuwa umefanyika na Mwenyekiti wa chama ngazi ya Taifa kuchaguliwa.
Mwenyekiti wa muda atakabidhi jukumu la kuongoza mkutano kwa Mwenyekiti wa Taifa aliyechaguliwa baada ya jina la mwenyekiti huyo kutangazwa.
Kifungu cha (xii) kinaeleza kuwa Mkutano Mkuu wa Taifa utamchagua Mwenyekiti wa Taifa ambaye atakuwa pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya Taifa, Kamati Tendaji Taifa.
Kauli ya Hamad Rashid, Kamati ya uchaguzi
Alipotafutwa mwenyekiti ambaye amemaliza muda wake, Rashid kuhusiana na tuhuma hizo amesema hazina ukweli wowote, kwa kuwa yeye alikuwa anamaliza muda wake, hivyo alipaswa kumkabidhi mwenyekiti mpya.
Kuhusu suala la kura kuongezeka na kutoa rushwa amesema, orodha iliyotumika kwa kura Doyo akiwa katibu mkuu ndiyo aliyoiandaa, na kuwakabidhi kwa kamati ya uchaguzi.
“Doyo asome katiba vizuri, mimi nilikuwa sigombei tena nilikuwa namaliza muda wangu na nilipaswa kukabidhi mshindi atakayeshinda kwa kuwa alitumia fedha nyingi kugawa rushwa ndio maana, lakini uchaguzi ulienda vizuri,”amesema Hamad Rashid.
Kwa upande wa Katibu wa kamati ya uchaguzi, Innocent Siriwa, amesema kwa kuwa rufaa imeshawasilishwa na chama kina uongozi mpya, hawawezi kuzungumza lolote hadi pale watakapoijibu.
Alipotafutwa Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ali Ahmed, amesema kama yapo malalamiko yameshawasilishwa ofisini, wanasubiri ili wayashughulikie.