Dar es Salaam. Wabunifu wamekuja na kifaa cha kukomesha udanganyifu wa wasimamizi wa mashamba ya samaki kwa kubuni kifaa cha kulishia samaki kitakachotoa taarifa kwa mmiliki ya muda na kiasi cha chakula walichopewa.
Ili kupatikana samaki kwa wingi ni lazima kuwe na kazi ya kupanda, kukuza na kuwatunza katika bwawa au uzio uliotengenezwa kwa vyuma, miti pamoja na nyavu, hivyo wabunifu wamekuja na kifaa cha kisasa kitakachosaidia kulisha samaki kwa wakati.
Kifaa hicho kitapeleka taarifa moja kwa moja kwa mmiliki kupitia ujumbe mfupi wa maneno utakaoleza kiasi cha chakula kilichowekwa na muda gani.
Mbunifu wa kifaa hicho, Livinus Paschalates wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amezungumza na Mwananchi katika maonyesho ya 48 ya Sabasaba kuwa kifaa hicho kitapunguza manung’uniko ya wafugaji ya kupata hasara kutokana na samaki kufa au kutofikia uzito hitajika.
“Hii itaondoa usumbufu wa kufika shambani mara kwa mara kujua taarifa za ulishaji wa samaki na mfugaji anaweza kuwa safarini na akapata kile anachopasa kufahamu akiwa mbali,” amesema.
Pia, amesema njia hiyo itasaidia kupunguza vifo vya samaki vinavyosababishwa na bakteria wanaozalishwa kwenye mikono wakati wa ulishaji.
“Kwa utafiti mdogo niliofanya, wapo wafugaji wakubwa waliopata hasara kwa sababu ya makosa ya ulishaji huku wengine wakiingiza imani potofu ikiwepo ya kutiliwa sumu au kufanyiwa ushirikina na kusababisha vifo vya samaki,” amesema Livinus.
Mtaalamu Mshauri wa ukuzaji viumbe maji, Mussa Said amesema kifaa hicho kitasaidia kuondoa uongo kwa wasimamizi wa samaki kwa kutokulisha kwa wakati kama ilivyowekwa kwenye kalenda.
“Kuna wakati mashamba boy wanatoa taarifa za uongo, anaweza kusema amelisha saa 10 kumbe muda huo amekwenda kuangalia mpira. Tunapopita kufanya tathmini ya samaki kwa miezi mitatu alitakiwa na gramu 200 ukifuatilia unakuta ana gramu 120,” amesema Said.
Amesema katika upimaji wa vitu vingine, unaweza kukuta kila kiti kipo sawa lakini taarifa za baadaye zikasema samaki hawakupatiwa chakula kwa wakati, hivyo kuwekwa kwa kifaa hicho kutasaidia ukuaji mzuri wa samaki.
Mfugaji wa samaki Kiluvya, Mahamoud Ismael amesema changamoto inayowakabili ni kutopatiwa taarifa za kweli za ukuaji wa samaki na wamejikuta wakiuza samaki kwa hasara tofauti na matarajio.
“Unafuga kwa kutumia gharama kubwa ya vyakula halafu tunauza kwa bei ya hasara kwa sababu samaki hawafikii kiwango hitajika kwenye soko, hivyo kifaa hiki kitasaidia kupata taarifa za ukweli na kuhamasisha wafugaji wa samaki kujitokeza kwa wingi,” amesema Ismael.
Katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2024/25 Serikali imesema itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ugani, uzalishaji wa vifaranga, kaguzi na uhamasishaji wa mbinu bora za uzalishaji na udhibiti wa magonjwa.