Viongozi wa dini Kenya waonya juu ya kuwateka nyara vijana – DW – 01.07.2024

Haya yanajiri baada ya ripoti zilizotolewa kuonesha zaidi ya vijana 34 hawajulikani walipo.

Viongozi wa kidini kutoka mjini Mombasa nchini Kenya wamekosoa vitendo vya mauaji na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha yaliyofanyika alhamisi wiki iliyopita.

Kundi la mashirika yanayopigania mageuzi katika kikosi cha polisi limetoa ripoti inayoonesha watu  34 walitekwa nyara wakati wa maandamano yaliyofanyika wiki iliyopita nchini Kenya.

Soma pia: Ruto: “Sina hatia” na vifo vya waandamanaji

Askofu Alphonce Baya kutoka kanisa la ACK Mombasa ameitaka serikali kuwaachilia huru vijana ambao kufikia sasa hawajulikani walipo tangu walipokamatwa wakati wanaandamana.

“Haya matukio ya utekaji nyara yanayoendelea yanafanyika kinyume na sheria, na taifa la kenya kwa sasa hatufai tena kushuhudia mambo kama hayo,tukumbuke rais ruto pamoja na deputy wake na serikali ya Kenya kwanza iliahidi kwamba mambo haya hayatafanyika tena”

Vijana wakishiriki maandamano ya kupinga mswada wa fedha mjini Nairobi
Vijana wakishiriki maandamano ya kupinga mswada wa fedha mjini NairobiPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Viongozi hao pia wametowa mwito wa kusitishwa kwa maandamano hayo yanayotarajiwa kuendelea kesho ili kudumisha amani nchini.Hii hapa sauti ya  Sheikh Mohamed Khalifa katibu mratibu wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini Kenya.

“Maafa yaliyotokea Githurai, Ongata Rongai, Nairobi, Homabay, Migori, Kisumu na Mombasa ni maafa makubwa,watu wamelala na business zao wameamka maskini watu wamelala na afya zao wameamka vilema,wengine maiti.Maadam rais amekubali ya kwamba ameondoa mswada tumpe nafasi akae na hao kwa sababu haya maandamano kwa sasa yanaelekea pabaya.”

Soma pia: HRW: Watu 30 wameuawa katika maandamano ya kuipinga serikali Kenya

Jana jioni Rais wa Kenya William Ruto aliulizwa maswali  na wanahabari, katika kipindi maalum kilichooneshwa kwenye televisheni na kwenye mahojiano hayo Rais alipinga kuhusika na mauaji ya waandamaji.

“Sina damu mikononi mwangu, rekodi niliyo nayo ya idadi ya watu waliokufa ni 19, rekodi hiyo imetoka kwa kwa vyombo vya usalama, inasikitisha na kama nchi inayoheshimu demokrasia vifo hivyo havifai kuwa sehemu ya mazungumzo yetu, mali ya thamani ya shilingi bilioni 2.4 imeharibiwa, ofisi ya jaji mkuu pia imeteketezwa moto, ofisi ya serikali ya kaunti ya Nairobi pia imechomwa, sehemu ya bunge imechomwa. Hio ndio hali ilivyo.”

Wananchi kwenye mitandao ya kijamii wameeleza kukasirishwa kwao na kauli ya Rais William Ruto ambaye wanasema hakujali kuhusu maisha ya wakaazi bali anajali  tu kuhusu mali zilizoharibiwa.

 

Related Posts