Wanafunzi UDSM wagundua kifaa cha kudhibiti joto kwa vifaranga vya kuku

Dar es Salaam. Wafugaji wa kuku wako mbioni kuondokana na hasara wanayoipata kwa vifaranga vyao kufa kutokana na baridi au joto lililozidi kiwango kinachohitajika. 

Hiyo ni baada ya wanafunzi sita wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kubuni kifaa kinachoweza kudhibiti joto linalohitajika kwa vifaranga katika umri tofauti.

Kifaa hicho pia kinaweza kudhibiti na kuweka hali ya hewa inayohitajika katika miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika haraka kama matunda na mbogamboga.

Hayo yameelezwa katika viwanja vya maonyesho ya 48 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam, (DITF) na Mhandisi wa maabara wa chuo hicho, ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Adriano Kamoye alipokuwa akizungumza na Mwananchi, leo Jumatatu, Juni 1, 2024.

Kamoye amesema mfumo huo umebuniwa ili kuwasaidia wafugaji kuondokana na taabu wanayoipata katika utunzaji wa vifaranga hasa katika siku za awali, zinazohitaji uangalizi zaidi.

“Katika siku za awali kuna kiwango cha joto kinachohitajika kwa vifaranga, ambacho hakitakiwi kuzidi sana au kupungua sana, na si joto tu hata baridi,” amesema Kamoye.

Amesema baadhi ya wafugaji hulazimika kuweka majiko ya moto ndani ya mabanda ili kazalisha joto kwa vifaranga au taa zinazozalisha joto lakini wakati mwingine ni vigumu kuwapo uhakika wa kile kinachofanyika.

Amesema wakati mwingine hujisahau hadi moto kuzima, jambo linalofanya vifaranga vipigwe na baridi hadi kufa au umeme kukatika kwa muda mrefu.

“Sasa kifaa hiki kitakuwa ni suluhisho kwani kitamwezesha mfugaji kujua nini kinahitajika kwa wakati huo,” amesema Kamoye.

Akielezea namna kinavyofanya kazi, Kamoye amesema ipo sehemu inayoonyesha joto lililopo ndani ya chumba husika na kiwango cha joto kinachohitajika kulingana na kuku waliopo.

Ikiwa joto ni kali na linalohitajika ni kiwango cha chini, mfugaji anaweza kulishusha kwa kutumia kitufe maalumu ili kuhakikisha mifugo yake inakuwa salama.

“Lakini kuna kujisahau, ili kuondoa usumbufu unaweza kuuseti katika mfumo wa kujiendesha wenyewe kwa kupandisha au kushusha kiwango kulingana na wakati husika. Kama joto liko juu ya kiwango ndani ya banda ili kushushwa kufikia kiwango kinachohitajika ubaridi utazalishwa na mfumo huu ili kupooza eneo husika,” amesema Makoye.

Kinyume chake ikiwa kuna baridi ndani ya banda, mfumo huo utazalisha joto hadi kufikia kiwango kinachohitajika kwa wakati huo na njia hiyo hiyo pia inayotumika katika usafirishaji bidhaa zinazoharibika.

Kwa sasa kifaa hicho kipo katika hatua za mwisho za majaribio kabla ya kuanza kufanyiwa maboresho zaidi.

Mmoja wa wafugaji waliozungumza na Mwananchi, Francisca Msangi amesema uwepo wa kitu kama hicho utakuwa mkombozi kwa wafugaji wengi nchini.

“Kama kuna kitu kinachohangaisha wafugaji basi ni kujua kiwango cha joto kinachohitajika kwa kuku kwa wakati fulani, huwa tunahangaika na majiko, taa, sasa kuna wakati ukifika hata hizo taa unatakiwa uzipunguze lakini hujui ufanye kwa kiasi gani, tunachokifanya ni kama kuweka chumvi kwenye chakula tunapotumia makisio,” amesema Francisca.

Linus Livinus yeye amekumbuka hasara ya vifaranga 500 aliyowahi kuipata baada ya mvua kunyesha kwa muda mrefu na kusababisha baridi kali.

“Mabanda yangu yako umbalu kidogo na ninapoishi, siku hiyo nilihudumia kuku nikahakikisha kila kitu kipo sawa nikarudi nyumbani, ilipofika saa nne usiku mvua kubwa ilianza kunyesha, nilikosa usingizi, ilipokuja kupungua nilikimbilia bandani na kukuta kuku wameishiwa nguvu, nilijaribu ninaloweza kufanya ila nilikiwa nimechelewa,” amesema Livinus.

Related Posts