Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia Kijana Shadrack Yusuph Chaula [24] Msanii wa Sanaa ya uchoraji, Mkazi wa Kijiji cha Ntokela, Wilaya ya Rungwe mkoa wa Mbeya kwa kitendo cha kuchoma moto picha ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 02, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi [SACP] Benjamin Kuzaga ameeleza kuwa Juni 30, 2024 huko Kijiji cha Ntokela, Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya Mtuhumiwa alijirekodi video fupi na kuituma katika mitandao ya kijamii ikionesha kutamka maneno makali ya kumkashifu Mhe.Rais na kisha kuchoma moto picha inayomuonesha Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, mara baada ya kuona taarifa hiyo inayosambaa mitandaoni Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifuatilia na kumkamata Mtuhumiwa huyo kwa kitendo hicho ili kufanya mahojiano kujua kwa nini ameamua kufanya hivyo.
Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na taratibu za kiupelelezi zinaendelea kukamilishwa, Jalada la kesi limeandaliwa na kufikishwa Ofisi ya Mashitaka ili baada ya hatua hiyo aweze kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma kwa kitendo alichokifanya kwani ni kinyume na Uungwana, utamaduni na Maadili ya Kitanzania.
#KonceptTvUpdates