EST waja na mwarobaini kuwadhibiti wachumi ‘makanjanja’

Dar es Salaam. Jumuiya ya Wachumi Tanzania (EST), imesema umefika wakati wachumi nchini wanapohitimu elimu ya juu, wanapaswa kufanya mtihani wa kupima ubobezi wao katika taaluma hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Julai 2, 2024 na mratibu wa jumuiya hiyo, Geofrey Mwambe, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la wanajumuiya wa uchumi linalotarajiwa kufanyika Julai 12, jijini Dar es Salaam.

Ili kufanikisha dhamira yao hiyo, wanatarajia kuishirikisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ili itoe ithibati ya mtihani huo.

Hatua hiyo itaifanya taaluma ya uchumi, ipitie mchakato kama wanaopitia mawakili, wahasibu na madaktari, ili kupata ithibati ya utaalamu wao.

Mwambe ambaye pia ni mbunge wa Masasi Mjini, amesema hatua hiyo itasaidia sio tu kuondoa wachumi makanjanja, bali kuwa na wachumi waliobobea katika taaluma hiyo, hivyo kuleta tija kwa taifa.

“Sasa hivi kuna baadhi ya watu wanasema wamesomea uchumi, lakini wape kazi inayohusu uchumi waambie wafanye hawana wanalolijua,” amesema Mwambe.

Frank Asheri, mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), amesema haoni umuhimu wa kuwa na mtihani huo kwa kuwa hata baadhi ya tasnia zenye mitihani hiyo bado zina ‘makanjanja’.

Saraphina Kamote, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema huko ni kurefushiana miaka ya kuendelea kusoma, ilihali hatuna uhakika wa wanachosomea kama watapata ajira au la.

Mchambuzi wa uchumi kutoka Chuo cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo, akitoa maoni yake kuhusu hilo, amesema hajui jambo hilo litaongeza thamani gani kwa wachumi.

“Inawezekana wanafanya hivi ili kupata fedha, lakini kinachotakiwa wangeanza kwanza na kuongeza nguvu ya jumuiya kujulikana, kuongeza idadi ya wanajumuiya kwani sio wachumi wote wapo katika jumuiya hiyo,” amesema Profesa huyo.

Badala yake ametaka viongozi wajikite kuhakikisha jumuiya imesimama na si kutaka kuleta ukiritimba na kuwasumbua watoto wa kimaskini kusoma tena na kulipia mitihani.

Akizungumzia kongamano hilo, Mwambe amesema wataalamu hao watajadili masuala yanayohusu uchumi na kupata fursa ya kuimarisha ujuzi wao na kujifunza mikakati ya kujumuisha utafiti wa hivi punde na mwelekeo mpya wa kiuchumi.

Lengo jingine amesema wachumi wa Tanzania, kutoka mataifa mengine na Diaspora watakuja na suluhisho madhubuti la mtangamano na changamoto za maendeleo zinazoikabili Tanzania.

“Kongamano linalenga kuzingatia, kujadili na kuchambua masuala ya maendeleo ya kisasa na kupendekeza suluhisho linalofaa.

“Wakati wa kongamano washiriki zaidi ya 300 watakaokuwepo watatoa mapendekezo ya wazi, ili kuisaidia Tanzania katika kuunda upya sera zetu za kiuchumi, ili kukabiliana na changamoto zilizopo za kijamii na kiuchumi,” amesema.

Matarajio yao baada ya kongamano hilo, Mwambe amesema ni uwepo wa mafunzo shirikishi kwa wanataaluma hao kila kunapopatikana fursa, huku likiwa limebeba kaulimbiu ya “Wajibu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Tanzania katika Maendeleo ya Uchumi wa Taifa”.

Related Posts