Gen Z waliamsha tena, barabara zafungwa

Dar es Salaam. Waandamanaji wa Gen Z wamerudi barabarani sasa wakiwa na kaulimbiu waliyoipa jina kamata maeneo yote dhidi ya utawala wa Rais William Ruto, yaani ‘Occupy everywhere protests against President William Ruto’s regime’

Maandamano nchini humo yamekuwa ya kila wiki, yakitanguliwa na yale ya kukataa muswada wa fedha kwa mwaka2024 ambao Rais Ruto amekataa kuusaini na kuurejesha bungeni.

Hatua hiyo ya Rais Ruto ilitokana na matakwa ya waandamanaji waliopaza sauti kukataa muswada huo waliodai unaongeza ugumu wa maisha.

Rais Ruto katika hatua yake ya kuleta umoja nchini humo, aliwaita vijana hao kwa ajili ya mazungumzo, lakini hawajasitisha maandamano hayo.

Jumapili iliyopita, Ruto alisema yupo tayari kuzungumza na vijana hao ana kwa ana au kwa njia ya mjadala wa mtandao wa X (zamani Twiter).

Maandamano ya leo Jumanne, Julai 2, 2024 yameshika hatamu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo eneo la Kaunti ya Kakamega ambako makundi ya vijana wakionekana kwenye maandamano.

Idadi hiyo ya waandamanaji ni kubwa katika kaunti hiyo, ikilinganishwa na waandamanaji wa kaunti ya Voi.

Nairobi CBD hali ni tofauti, Jeshi la Polisi limelazimika kutumia bomu la kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliojumuika kwenye makutano ya barabara ya Kenyatta na Moi.

Pia, eneo la barabara linalofahamika kama Wainyaki halipitiki kutokana na maandamano na Jeshi la Polisi linakabiliana na waandamanaji kupitia gesi ya kutoa machozi.

Kwa upande wa Mombasa, maandamano tayari yameshika hatamu kwa idadi kubwa ya waandamaji na polisi wakiwataka kuepuka kufanya uharibifu wa mali.

Kaunti ya Homa Bay waandamanaji wamefunga barabara, huku waandamanaji wa eneo la Kisumu wakiandamana kuelekea barabara ya Kenyatta na makutano ya barabara ya Oginga Odinga.

Wakati hayo yakijiri katika baadhi ya kaunti, yapo maneo ambayo maandamano bado hayajaripotiwa, ikiwemo Turkana, Siaya.

Habari kwa msaada wa Mtandao wa Daily Nation.

Related Posts