DIRISHA la usajili kwa wachezaji huru (free agents) lipo wazi kwa sasa kwenye Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), ambapo wachezaji wanatoka timu moja na kwenda nyingine na hata zaidi ya timu moja kupitia mabadilishano.
Usajili unaosubiriwa zaidi ni ule wa Klay Thompson ‘Killer’ kujiunga na Los Angeles Lakers ya LeBron James ambaye inaelezwa kuwa yupo tayari kupunguza mshahara ili tu timu hiyo imchukue Klay aitumikie kutokea Golden State Warriors.
Hadi sasa usajili ambao umezua gumzo kubwa ni ule wa staa Paul George ‘PG13’ aliyevunja kiapo cha kustaafia Los Angeles Clippers na kuhamia Philadelphia 7ers kwenda kutengeneza utatu mpya katika ligi.
PG13 anaungana na Joel Embiid na Tyrese Maxey kuipatia Sixers utatu utakaoipa nafasi kusaka taji la NBA msimu ujao kutokana na ubora wa mastaa hao.
Staa huyo ameondoka Clippers wakati ambao mwenzake James Harden anaendelea kubaki na Kawhi Leonard, huku hatima ya Russell Westbrook ikiwa haijafahamika kutokana na mpango wa timu hiyo kutaka kufanya biashara na timu nyingine.