Mabomu ya machozi, mawe, moto Wakenya wakimkaidi Ruto – DW – 02.07.2024

Maandamano ya Jumanne yalianza katika hali ya furaha lakini yalizidi kuwa na vurugu kadiri siku ilivyosogea. Katika eneo la biashara katikati mwa jiji la Nairobi, polisi waliokuwa wamevalia helmeti na kubeba ngao na virungu vya mbao waliwakabili waandamanaji, huku mabomu ya machozi yakilipuka katikati mwa umati huo.

Kioski kilichomwa moto katikati ya barabara huku madaktari wakimhudumia kijana aliyelala kwenye njia ya wapita kwa miguu akiwa na damu mkononi. Vijana wengine walikamatwa na kurundikwa kwenye gari.

Nje ya mji mkuu, mamia ya waandamanaji waliandamana Mombasa, mji wa pili kwa ukubwa nchini Kenya, kwenye pwani ya Bahari ya Hindi. Walibeba makuti, wakapuliza pembe za plastiki na kupiga ngoma, wakiimba “Ruto lazima aende!”

Kenya | Maandamano Nairobi
Baada ya awali kuandamana kupinga muswada fedha wa mwaka 2024, maandamano yaligeuka na kudai kujiuzulu kwa Rais William Ruto.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Baadaye, kituo cha televisheni cha NTV Kenya kiliripoti kuwa watu wawili walipigwa risasi mjini Mombasa, na kuonyesha picha za magari yakiwaka moto.

Soma pia: Ruto: “Sina hatia” na vifo vya waandamanaji

Ruto, anayekabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa urais wake wa takriban miaka miwili, amenaswa kati ya matakwa ya wakopeshaji kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kupunguza nakisi, na idadi kubwa ya watu wanaoteseka kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Wanachama wa vuguvugu la maandamano, ambalo halina viongozi rasmi na ambao wengi hupanga mikakati yao kupitia mitandao ya kijamii, wamekataa wito wa Ruto wa mazungumzo – hata baada ya kuachana na mapendekezo yake ya nyongeza ya kodi.

“Watu wanakufa mitaani na kitu pekee anachoweza kuzungumzia ni pesa. Sisi sio pesa. Sisi ni watu. Sisi ni binadamu,” mwandamanaji Milan Waudo aliiambia Reuters mjini Mombasa. “Anahitaji kuwajali watu wake, kwa sababu ikiwa hawezi kuwajali watu wake basi hatumhitaji katika kiti hicho.”

Soma pia: Ruto auondoa kabisa muswada wa fedha 2024

Maandamano mengine yalifanyika Kisumu, Nakuru, Kajiado, Migori, Mlolongo na Rongo, kulingana na picha zilizotangazwa kwenye televisheni ya Kenya. Katika mji wa kusini magharibi wa Migori, waandamanaji walichoma moto matairi.

Tume ya taifa ya haki za binadamu ya Kenya (KNHCR) imesema Wakenya 39 wameuawa katika maandamano na makabiliano na polisi tangu Juni 18. Vingi ya vifo hivyo vilitokea Juni 25 wakati maafisa walipofyatua risasi karibu na bunge ambapo baadhi ya waandamanaji walijaribu kuvamia jengo hilo kuzuia wabunge kupigia muswada wa nyongeza ya kodi.

Waandamanaji Kenya ´wamkalia kooni´ Rais Ruto

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

‘Siku nzuri’

“Tumedhamiria kumshinikiza rais ajiuzulu,” alisema Ojango Omondi, mwanaharakati jijini Nairobi. “Tunatumai maandamano ya amani na idadi ndogo ya majeruhi, kama watakuwepo.” Mamlaka ziliomba utulivu.

“Ni siku nzuri ya kuchagua uzalendo. Siku nzuri ya kuchagua amani, utulivu na utukufu wa utaifa wetu,” mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu Gerald Bitok aliandika kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne, akiongeza kwa Kiswahili: “Vurugu si uzalendo.”

Baadhi ya wanaharakati waliokuwa wameitisha maandamano hayo walichukizwa na machafuko hayo. “Majambazi wamejipenyeza,” Hanifa Adan, mwanaharakati na ripota wa gazeti la Eastleigh Voice, aliandika kwenye X, akifuatisha ujumbe wake na emojis zilizovunjika moyo.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, mshindi wa pili katika chaguzi nne zilizopita za urais, aliunga mkono waandamanaji ingawa walitoa wito kwa wanasiasa kujiepusha na maandamano yao.

“Vijana wameipa nchi yetu fursa yake ya mwisho,” chama cha Odinga cha ODM kilisema katika taarifa. “Ama tuitumie fursa hii na kuogelea nayo kwa kutekeleza madai yao yote, au tuipuuze na kuizamisha nchi kabisa.”

Kenya | Hotuba ya Rais William Ruto baada ya maandamano
Licha ya Rais Ruto kusalimu amri na kuondoa sheria ya fedha iliyozusha machafuko, maandamano yameendelea Kenya kumshinikiza aachie madaraka.Picha: James Wakibia/SOPA Images via ZUMA Press/picture alliance

Soma pia: Mahakama ya Kenya yaidhinisha kutuma jeshi huku vijana waandamanaji wakitafakari hatua inayofuata

Maandamano hayo, ambayo yalianza kama ghadhabu ya mtandaoni kuhusu ongezeko la karibu dola bilioni 2.7 za kodi katika mswada wa fedha uliopendekezwa, yamekua na kuwa harakati ya kitaifa dhidi ya ufisadi na utawala mbovu.

Ruto ameagiza wizara ya fedha kubuni mbinu za kubana matumizi ili kuziba pengo la bajeti lililoachwa na uondoaji wa mipango ya kodi, na kuongeza pia kwamba kuna haja ya kukopa zaidi.

Mwanaharakati mkongwe wa kupambana na ufisadi John Githongo aliiambia Reuters kuwa wakati Ruto alikuwa amehutubia taifa na vyombo vya habari, “hakuna dalili kwamba anataka kuchukua hatua” kuhusu matakwa ya waandamanaji, ikiwa ni pamoja na kuwafuta kazi maafisa wabadhirifu.

“Hakujawa na dalili zozote za serikali kwamba watachukulia kwa uzito wito wa kushughulikia ufisadi,” alisema.

Maandamano hayo yalikuwa ya amani hadi Juni 25, wakati baadhi ya waandamanaji walipovamia bunge kwa muda na kuwasha moto sehemu yake, na kuilaazimu polisi kufyatua risasi za moto.

Ruto ametetea vitendo vya polisi na kulaumu ghasia hizo kwa “wahalifu” ambao walikuwa wamejipenyeza kwenye maandamano hayo.

Waandamanaji Kenya wavamia majengo ya Bunge la Taifa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Chanzo: RTRE

Related Posts