Majiha katika nyakati za kudhihirisha umwamba wake

JULAI 20, mwaka huu bondia namba moja nchini ‘Tanzania One’ Fadhili Majiha maarufu Kiepe Nyani atapanda ulingoni kutetea Mkanda wa ubingwa wa Baraza la Ngumi Duniani kwa Tawi la Afrika ‘WBC Afrika’ ambalo limepangwa kufanyika katika Jiji la Mbeya.

Majiha atapanda ulingoni kwenye pambano hilo dhidi ya Sabelo Ngebinyana wa Afrika Kusini katika pambano litakalokuwa la raundi kumi kabla ya Abeid Zugo, Idd Pialali, Emmanueli Mwakyembe na Mubaraka Denso kuweka uzito kwa mapambano ya utangulizi.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Jiji la Mbeya kuandaa pambano kubwa la kimataifa ambalo litawakutanisha mabondia wenye rekodi kubwa nchini katika mchezo wa ngumi za kulipwa kama ilivyofanya mikoa mengine ya Ruvuma, Morogoro, Tanga, Arusha, Mtwara, Mwanza na Dar es Salaam.

Tayari Majiha ambaye amepangiwa kucheza pambano kuu siku hiyo ameshaweka rekodi ya kupanda ulingoni nje ya Mkoa wa Dar es Salaam baada ya mwaka jana kupigana katika Jiji la Mwanza ambapo kwake ilikuwa ni mara ya kwanza.

Bondia huyo namba moja ameingia kwenye orodha ya mabondia waliowahi kupanda ulingoni kwenye mapambano makubwa nchini kucheza nje ya mikoa mengine kama Twaha Kiduku anayeshikilia rekodi ya kupigana kwenye mikoa minne, Seleman Kidunda (Ruvuma), Ibrahim Class (Tanga), Hassan Mwakinyo (Tanga na Dodoma), Dullah Mbabe (Tanga na Dar es Salaam).

Kitendo cha mabondia hao kutengeneza rekodi kuusambaza mchezo huo kimekuwa kikijenga na kuibua mashabiki wapya kila uchwao ambapo awali walikuwa wakiwashuhudia mastaa hao wa ngumi kupitia runinga pekee.

Mwanaspoti linakuchambulia rekodi za mabondia watakaopanda ulingoni katika pambano hilo ambalo litafanyika chini ya promosheni ya Kemmon Sports inayoongozwa na promota Saada Kasonso.

Majiha vs Sabelo Ngebinyana

Ni pambano la kutetea ubingwa wa WBC Afrika ambalo litamkutanisha bondia namba moja Tanzania, Fadhili Majiha dhidi ya Sabelo Ngabiyana kutoka Afrika Kusini.

Bondia huyo namba moja nchini, atetea mkanda wa ubingwa huo baada ya kushinda Oktoba mwaka jana kufuatia kumtandika kwa pointi Bongani Mahlangu wa Afrika Kusini kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba.

Majiha licha ya kuwa bondia namba moja huku akiwa hatajwi sana lakini rekodi zake zimekuwa moto wa kuotea mbali akiwa na jumla ya mapambo 50 aliyocheza mpaka sasa ambayo sawa na raundi 317. Majiha ameshinda mapambano 32 kati ya hayo 15 akishinda kwa ‘Knockout’ yaani KO.

Bondia huyo aliyewahi kuweka rekodi ya kushika nafasi ya tano duniani kati ya mabondia 1068 wa uzani wake wa bantam, amepigwa mapambo 14, kati hayo ‘Knockout’ zipo tatu huku akitoka sare mara nne.

Majiha anayetumia mtindo wa ‘orthodox stance’ kutanguliza mguu wa kushoto na mkono wa kushoto mbele wakati wa kupigana, amekuwa na uwezo wa kushinda KO kwa asilimia 46.88%  huku akishika nafasi ya kwanza nchini kwa mabondia wote wa Tanzania na kwenye uzani wake wa bantam ambapo kuna jumla ya mabondia 56.

Lakini duniani, Majiha anakamata nafasi ya 15 katika mabondia 1068 huku hadhi yake ya  nyota ikiwa ni tatu na nusu licha ya kufika nne na nusu akiwa ni bondia wa kwanza nchini kufikia hadhi hiyo kabla ya kuporomoka.

Siyo jina geni hapa nchini na wala siyo bondia wa kumchukulia poa kabisa linapokuja suala la kuwania mkanda wowote wa ubingwa.

Bondia huyo kutoka katika ardhi ya Nelson Mandela ambayo iliwahi kutawaliwa na Makaburu, alishakuja Tanzania Februari mwaka jana na kumpiga Mtanzania, Tony Rashidi katika pambano la ubingwa wa ABU lakini kwenye mtandao wa rekodi iliwekwa sare huku ABU wakisisitiza Sabelo alimbonda Tony.

Lakini alirejea tena Desemba mwaka jana katika pambano ambalo halikuwa la ubingwa dhidi ya Oscar Richard ambapo alipoteza kwa pointi kabla ya Machi, mwaka huu kuja nchini kuwania mkanda wa ubingwa wa WBC Africa katika pambano ambalo lilimalizika kwa sare.

Sabelo mpaka sasa amecheza jumla ya mapambano 25 ambayo sawa na raundi 165 akiwa ameshinda 15 kati ya hayo 11 ni kwa KO, amepigwa mara nane kati ya hizo mara mbili ni KO na sare mbili.

Bondia huyo ambaye rekodi yake inaonyesha kwa sasa ameshapanda ulingoni na vigogo katika uzani wa supa bantam ambapo uwezo wake wa kushinda kwa KO upo juu zaidi ya Fadhili Majiha kwani amepewa asilimia 73.33% huku hadhi yake ya nyota ikiwa mbili.

Sabelo katika viwango vya nafasi anashika namba 104 katika mabondia 1318 duniani wakati nchini kwao anakamata nafasi ya tatu kati ya mabondia 41.

Mubaraka Denso vs George Kandulo

Bingwa wa mkanda wa Taifa wa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC), Mubaraka Denso atakuwa na kibarua cha kuwania mkanda wa Chama cha Muungano wa Ngumi Afrika ‘ABU’ dhidi ya George Kandulo wa Malawi.

Denso ambaye ni ingizo jipya katika ngumi akiwa chini ya Kemmon Sports Promotion, ana rekodi ya kucheza mapambano sita sawa na raundi 35 ikiwa kila raundi ina wastani wa dakika tatu. Atapanda ulingoni kuwania mkanda wa ubingwa huo katika uzani wa fly huku pambano hilo likitarajiwa kuwa la raundi kumi.

Bondia huyo ameshinda mapambano yake yote matano kati ya hayo mawili ni kwa KO na hajawahi kupigwa zaidi ya kutoka sare moja mapema mwaka huu dhidi ya Abdul Kubira.

Denso ambaye amepewa asilimia 40 pekee za kushinda KO, anatumia mtindo wa orthodox ambapo kwa sasa hadhi yake ni nyota moja na nusu kwa mujibu wa rekodi yake katika mchezo huo.

Bondia huyo mzaliwa wa Dodoma ambaye ametimiza miaka 18, anakamata nafasi ya kwanza nchini katika mabondia 33 wa uzani wa fly wakati duniani akiwa ni 103 kati ya mabondia 733.

Mzaliwa wa Malawi lakini amekita kambi na maisha yake nchini Afrika Kusini, ndiye mpinzani wa Mubaraka Denso katika pambano ambalo litapigwa katika Jiji la Mbeya.

Kandulo mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 19 sawa na raundi 93, ameshinda sita kati ya hayo mawili ni kwa KO na amechezea kichapo mara 12 kati hizo mbili ni kwa KO huku akiwa ametoka sare moja.

Bondia huyo uwezo wake wa kupiga KO ni asilimia 66.67% akishikilia rekodi ya kuwa bondia pekee kwenye uzani wake huku duniani akiwa ni 83 katika mabondia 268 pamoja na kupewa hadhi ya nyota moja

Idd Pialali vs Kiaku Ngoy

Unakumbuka mwaka 2022 Idd Pialali alivyotandikwa kichwa na Mfaume Mfaume na kusababisha pambano kuisha katika raundi ya kwanza bila ya kupatikana mshindi ‘no contest’ pale Arusha? Sasa jamaa amepewa mtihani mwingine mgumu.

Pialali ambaye ameshinda ubingwa wa mabara  wa UBO, PST na WBF anatarajia kuwa na vita kali ya aina yake Julai 20 katika Jiji la Mbeya dhidi ya Kiaku Ngoy kutoka DR Congo.

Pialali kutoka mitaa ya Manzese mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 45 sawa na raundi 226, atapanda ulingoni kwenye pambano la utangulizi litakalopigwa kwa raundi nane uzani wa Walter.

Bondia huyo mpaka sasa ameshinda jumla ya mapambano 32 kati ya hayo 22 ni KO na amepigwa mara kumi kati ya hizo saba ni kwa KO huku akitoka sare moja.

Mtanzania huyo anayetumia mtindo wa orthodox  stance katika kupigana, anaweza kushinda KO kwa asilimia 68.75 huku akiwa nafasi ya nane katika mabondia 44 wa uzani wake wakati duniani akiwa ni 462 katika mabondia 2275, hadhi ya nyota moja.

Mpinzani wa Pialali, anakamata nafasi ya tatu katika mabondia 16 wa uzani wa Walter na 717 duniani katika mabondia 2275.

Mbali ya kushinda mapambano manne katika mapambano sita aliyocheza hana KO na amepigwa mara mbili ambapo mapambano yote amekusanya raundi 30 pekee mpaka sasa.

Bondia huyo atakayeonyeshana kazi na Pialali anamiliki hadhi ya nyota moja kama ilivyo kwa mpinzani wake ambaye haitAkuwa mara ya kwanza kucheza dhidi ya mabondia wa DR Congo.

Mabondia wengine watakaouwasha moto katika Jiji la Mbeya ni Abeid Zugo, Emmanueli Mwakyembe na Kelvin Ngedere atakayezichapa na Ajemi Amani.

Related Posts