Dar es Salaam. Mwaka mpya wa fedha wa 2024/25 ukianza, wananchi wamelalamika kuongezeka makato ya kodi ya majengo kuanzia Julai Mosi 2024.
Hata hivyo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema ongezeko hilo ni malipo ya deni walilopaswa kukatwa Julai, 2023.
Kwa mujibu wa shirika hilo, kodi ya jengo kwa nyumba za kawaida imesalia Sh1,500 kwa mwezi na ghorofa ni Sh7,500 tangu mabadiliko ya Julai mwaka jana.
Ufafanuzi wa Tanesco umetolewa wakati ambao, wananchi kupitia mitandao ya kijamii wanalalamikia ongezeko la Sh500 katika makato ya kodi hiyo inayolipwa kupitia ununuzi wa umeme (Luku).
Kabla ya ufafanuzi kutolewa, waliolalamika walieleza Serikali imeongeza kodi ya majengo kutoka Sh1,500 hadi Sh2,000 kwa nyumba za kawaida.
Waliolalamika wameelezwa kukatwa Sh2,000 waliponunua umeme, hivyo kueleza kodi kuongezwa kimyakimya.
Tanesco kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma, imetoa ufafanuzi leo Julai 2, ikisema hakuna kodi ya jengo iliyoongezeka.
“Tunapenda kuufahamisha umma kwamba, hakuna ongezeko lolote lililofanyika kwenye viwango vya kodi ya majengo nchini isipokuwa ni madeni ya nyuma yaliyotakiwa kulipwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Tanesco, baada ya mabadiliko ya kodi hiyo yaliyotangazwa Julai 26, 2023 kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500 kwa nyumba za kawaida na Sh5,000 hadi Sh7,500 kwa nyumba za ghorofa, ilimaanisha mteja aliyenunua umeme kati ya Julai Mosi hadi 25, mwaka jana (kabla ya mabadiliko ya viwango vya kodi kuanza) alilipa kiwango cha zamani, yaani Sh1,000 na hivyo kuwa na baki ya deni la Sh500 ambayo alitakiwa kulipa.
Tanesco imesema kwa kuwa madeni ya fedha hizo hayakulipwa kwa baadhi ya wateja, kinachotokea sasa ambao ni mwaka mpya wa fedha 2024/25 ni kwa mteja kukatwa kiwango ambacho hakikulipwa.
“Makato ya madeni hayo yatafanyika kwa mara moja tu na yanatakiwa kulipwa kwa pamoja wakati mteja akifanya manunuzi ya umeme kwa mara ya kwanza kuanzia Julai 2024,” imeeleza.
Shirika hilo limesema baada ya Julai, mteja ataendelea kulipia viwango vya kawaida kulingana na aina ya nyumba anayoishi.
Matumizi ya shilingi badala ya dola
Katika hatua nyingine, baadhi ya taasisi na wakala za Serikali zimeanza kutekeleza agizo la Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba la malipo yote yanayofanyika nchini yafanywe kwa Shilingi ya Tanzania badala ya Dola ya Marekani.
“Kuanzia Julai Mosi, 2024 naelekeza wadau wote wa ndani, taasisi za umma, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa na watu wote waliopo nchini Tanzania wenye tabia ya kuweka bei kwenye huduma au kuuza bidhaa kwa fedha za kigeni kuacha mara moja na kuhakikisha bei za bidhaa na huduma hizo zinatangazwa na kulipwa kwa Shilingi ya Tanzania,” alisema Dk Mwigulu alipowasilisha bajeti ya Serikali bungeni Juni 13, 2024.
Kutokana na maelekezo hayo, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), zimetoa tangazo kwa wadau wote wa utalii kuhakikisha wanafanya na kupokea malipo kwa Shilingi.
Akizungumzia tangazo hilo, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli za Kitalii Tanzania (HAT), Kennedy Mollel amekiri hatua hiyo ina tija katika kuongeza thamani ya shilingi.
Hata hivyo, amesema katika sekta ya utalii inapaswa kuangaliwa vinginevyo akieleza kulikuwa na kiasi maalumu cha dola kinachotozwa kwa kampuni za kitalii na ziliwekwa kwa mujibu wa sheria.
Mabadiliko yaliyofanyika amesema yanamaanisha mamlaka zitaendelea kuhesabu kinachotozwa kwa dola, lakini kampuni ya kitalii itapaswa kulipa kiasi hicho kwa shilingi.
“Hii maana yake, mteja akinilipa kwa dola kutoka nje, mimi nitatakiwa kulipa tozo kwa shilingi, ikitokea thamani ya dola imepanda nitalazimika kulipa zaidi, ikitokea imeshuka Serikali itapata hasara,” amesema.
“Ilipokuwa inatozwa kwa dola kama ni 60 maana yake utalipa kiasi hicho tu hakibadiliki, lakini ukitakiwa kuilipa hiyo kwa shilingi, leo itapungua, kesho itapanda kutokana na thamani ya dola ya siku husika, kwa sekta binafsi tutaumia,” amesema.
Kwa mujibu wa Mollel, mpango huo ni mzuri lakini kwenye baadhi ya sekta kama ya utalii inahitaji kuangaliwa kwa umakini, kujua nani ataumia na nani atanufaika.
Ili kuwepo ufanisi katika mpango huo, amependekeza Wizara ya Maliasili na Utalii iweke kiwango elekezi cha tozo kwa shilingi ili kusiwe na mabadiliko.
“Tukisema iwe Sh150,000 maana yake kila kampuni itapaswa kulipa kiwango hicho, yaani tusitoze kwa mtindo wa dola, lakini malipo yafanywe kwa shilingi, tozo zitambulike kwa shilingi na zitozwe kwa shilingi,” amesema.
Pendekezo lingine ni kudhibitiwa kwa malipo ya dola taslimu, badala yake tozo hizo ziendelee kutozwa kwa fedha hiyo lakini lazima zilipwe kielektroniki.
“Tukifanya hivi maana yake tutaendelea kudhibiti matumizi ya dola kwa njia ya taslimu, italipwa kwa mtandao na hakuna atakayetoa kuitumia,” amesema.
Mhadhiri wa Utawala wa Biashara wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk David Amani amelitazama suala hilo kwa pande mbili, akigusia tija katika kuongeza dola nchini na kuimarisha thamani ya shilingi.
Kwa upande wa pili, ameeleza linaweza kusababisha changamoto ya michakato mingi kwa baadhi ya biashara kama ya utalii.
Kuhusu tija, amesema matumizi ya shilingi yatafanya mtu yeyote anayekuja na fedha ya kigeni apewe fedha ya Tanzania, hivyo kutakuwa na kiwango kikubwa cha fedha ya kigeni nchini.
Hatua hiyo, amesema itaongeza thamani ya shilingi na kusisimua uchumi wa nchi.
“Hatua hii itaondoa changamoto ya uhaba wa dola, tutakuwa na hifadhi kubwa ya dola na thamani ya shilingi itakuwa kubwa na hatimaye uchumi utaimarika,” amesema.
Kwa upande mwingine, amesema kutakuwa na changamoto hasa kwenye biashara kama za utalii, kwa kumwongezea mtalii mchakato wa kubadilisha fedha ndipo aingie nchini.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa ubadilishaji fedha wenye ufanisi ili mteja kutoka nje asione usumbufu wa kupata huduma.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Timoth Lyanga amesema hatua hiyo inaongeza heshima ya fedha ya Tanzania na inakuza thamani yake.
Madhara ya kuendelea kutumia dola nchini, amesema ni kuinyong’onyesha shilingi na hatimaye inakosa thamani na hadhi ilhali ipo kwenye nchi yake.
Baada ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25, wamiliki wa viwanda vya mvinyo wamesema ongezeko la ushuru kwenye ethani utadhorotesha kilimo cha zabibu.
Ongezeko la kodi hiyo lilipendekezwa na Dk Mwigulu katika bajeti akisema kila lita ya ethani itatozwa ushuru wa Sh7,000 kwa zile zenye kilevi cha asilimia 80 au zaidi inayotoka nje ya nchi.
Pia alipendekeza kutozwa ushuru wa Sh5,000 kwa kila lita ya Un-denatured Ethyl Alcohol yenye kilevi cha asilimia 80 au zaidi inayozalishwa ndani ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha kusindika mvinyo cha Alko Vintages, Archard Kato amesema kupanda kwa ushuru huo ni kuongeza changamoto kwa wasindikaji.
Changamoto nyingine amesema ni kupanda kwa bei ya dola ambako kumeongeza gharama za uzalishaji wa mvinyo. Amesema wanauza bei ya wakati dola ikiwa Sh2,100.
Kato amesema kupandisha ushuru katika ethani, ni kurudisha nyuma kilimo cha zabibu kwa sababu uwezo wa kuuza utakuwa mdogo na hawatakuwa na uwezo wa kushindana na mvinyo kutoka nje.
“Hatutaweza kuchukua zabibu nyingi kutoka kwa wakulima. Hili jambo inawezekana watu wasilione. Kama mkakati wa Serikali ni kuendeleza zabibu basi sera zetu zisipingane na nia tuliyokuwa nayo,” amesema.
Waziri wa Mipango na Uwezeshaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumzia hilo, amesema hatua ya Serikali kupitisha kodi katika ethanol imelenga wanaozalisha vinywaji vikali nchini ambao watu wanapofanya manunuzi hurudishiwa kodi hiyo.
“Ndio maana Serikali iko kila siku na Bunge linakaa mara kwa mara kwa hiyo tunaipokea, tutaichakata na huko mbele tutarekebisha vizuri tu,” amesema Profesa Kitila aliyetembelea kiwanda hicho.
Nyongeza na Sharon Sauwa (Dodoma)