Mbowe: Serikali iwadhibiti tembo wanaoingia makazi ya watu

Muheza. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amezitaka mamlaka zinazohusika kusimamia na kudhibiti wanyamapori nchini, kuchukua hatua za kuwadhibiti tembo wanaoingia kwenye makazi ya wananchi katika Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga.

Akizungumza na wananchi wilayani humo, ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya hadhara leo Julai 2, 2024 kwenye kampeni yao ya operesheni +255, Mbowe amesema amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa eneo la Maramba, wilayani Mkinga kuwa tembo wanasumbua.

Amesema lazima uwepo udhibiti wa wanyamapori kwa kuweka uzio utakaolinda wanyama, lakini muda huohuo kuwalinda na wananchi, pia uharibifu unaofanywa na wanyamapori hao.

Mbowe ameongeza kuwa vijiji vingi nchini vinavyopakana na hifadhi za taifa, kuna vilio vya kuvamiwa na wanyamapori na kupata madhara kwa muda mrefu, aeetolea mfano nchini Kenya ambako hifadhi zake zimewekewa mazingira mazuri na wanyama hawatoki.

“Nimetoka Maramba tembo wanaua wananchi, wanasema tembo hao wanatoka Mkomazi na Tsavyo Kenya wanakuja Tanzania, wanaua raia,” amesema Mbowe.

Awali kwenye kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema -Zanzibar, Salim Mwalimu ameishauri Serikali kuangalia jinsi ya kuboresha sekta ya utalii, ili itoe vijana wengi kutoka Tanzania, kwani kwa sasa ni wachache.

Amesema vijana wengi wa Tanzania wanashindwa na wenzao kutoka nchi jirani kama Kenya kwenye ushindani wa soko la ajira kwenye mambo ya utalii na changamoto kubwa ni kutofahamu vizuri baadhi ya lugha za kigeni, ikiwemo Kiingereza kwa fasaha.

Hivyo, ameishauri Serikali kuangalia katika kuboresha mitaala ya elimu waboreshe pia kwenye sekta ya utalii, ili vijana wapate elimu itakayowaweza kuingia kwenye soko la ajira, hasa masuala ya kuhudumia watalii.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yosepher Komba amewataka wanachama wa chama hicho wilaya ya Muheza kufanya siasa safi na kuachana na misuguano, hasa mambo ya kung’oleana bendera za vyama vyao.

Chadema kipo kwenye ziara maalumu ya operesheni +255 katika Kanda ya Kaskazini kwenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo kwa mkoa wa Tanga wamefanya mikutano kwenye wilaya ya Kilindi, Handeni, Pangani, Mkinga, Tanga na Muheza.

Related Posts