Rais Samia Suluhu Hassan amemteua aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Japan Kidata kuwa Mshauri wa Rais, Ofisi ya Rais – Ikulu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka, imesema nafasi ya Kidata imechukuliwa na Yusuph Juma Mwenda.
Kabla ya uteuzi huo, Mwenda alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Pia Rais Samia amemteua Dk. Selemani Saidi Jafo kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Kabła ya uteuzi huu, Dk. Jafo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Aidha, Dk. Ashatu Kachwamba Kijaji aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Mabadiliko hayo yamekuja siku chache baada ya kuwepo mgomo wa wafanyabiashara kutoka mikoa zaidi ya 10 nchini ikiongozwa na wa soko la Kariakoo waliofunga maduka yao kwa siku tatu mfululizo kutokana na matumizi ya kudai kodi kwa nguvu yaliyokuwa yanatumiwa na TRA.
Wafanyabiashara hao waliituhumu TRA kutumia kikosi kazi kudai kodi kwa nguvu, kufunga akaunti za baadhi ya wafanyabiashara hali iliyochochea mgomo huo.
Pia Gazeti la MwanaHALISI lilifichua siri za mgogoro huo kuwa ni hatua ya baadhi ya vigogo serikalini na TRA, kuamua kuwakamua wafanyabiashara, ili kutetea nafasi zao.
Miongoni mwa waliotajwa kushinikiza kukamuliwa kwa wafanyabiashara hao, ni pamoja na Kidata, anayedaiwa kuongezewa mkataba wa kuwapo katika mamlaka hiyo.
Wakati mgomo huo ukipamba moto tarehe 26 Juni mwaka huu Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa amepigiwa simu na Rais Samia na kumhakikishia ameagiza mfumo wa utozaji kodi urekebishwe.
Rais Samia pia aliwaahidi wafanyabiashara hao kuwa hadi kufikia tarehe 8 Agosti mwaka huu atakuwa ameinyoosha bandari ya Dar es Salaam na kuweka mazingira rafiki ya biashara, mgomo wa wafanyabiashara umeendelea kupamba moto katika mikoa nane.
Wakati Rais Samia akiahidi hayo kwa wafanyabishara, nap mabalozi wa Marekani, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden, na Ujerumani waliomba kikao na Serikali ya Tanzania kutokana na wawekezaji wa nchi hizo waliowekeza nchini, kubambikiwa kodi za kipindi cha miaka 15 iliyopita pamoja na kufungiwa akaunti na TRA.
Mabalozi hao walilalamikia mazingira yasiyoridhisha ya uwekezaji nchini kutokana na nguvu kupita kiasi iliyotumiwa na TRA kufunga akaunti za baadhi ya kampuni za wawekezaji hao.
Tayari Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameshawakubalia mabalozi hao kuhusu kikao hicho ambacho hata hivyo haijaelezwa ni lini watakutana na mawaziri husika.
Katika uteuzi huo, pia Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Mhandisi Yahya lsmail Samamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini. Kabla ya uteuzi huu, Mhandisi Samamba alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.
Mhandisi Samamba anachukua nafasi ya Kheri Abdul Mahimbali ambaye atapangiwa kazi nyingine.