KILA unapovuta picha ya uwepo wa Clatous Chama, Maxi Nzengeli, Stephen Aziz KI, Prince Dube na Pacôme Zouzoua unachoona ni ushindi tu.
Unachoona kingine ni mtu kupigwa tano kila siku. Unachoona ni safari ya Yanga kwenda kushinda kila mechi. Unachoona ni Yanga kwenda fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Unachoona ni Yanga kushinda mechi zote za Dabi. Unachoona ni Yanga kupiga pasi 700 kila mechi.
Ni raha juu ya raha duniani. Unaweza kuiona Yanga kama Manchester City. Unaweza kuiona Yanga ni kama Real Madrid. Kwa bahati mbaya mpira haupo kwenye njia hiyo. Mpira ni mchezo wa ajabu sana. Pengine mpira ndiyo mchezo usiotabirika kabisa. Unaweza usiamini mechi yako pale Yanga itakapofungwa na Pamba Jiji FC. Utabaki mdomo wazi pale Yanga itakapotolewa hatua za awali kabisa za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mpira ni zaidi ya tuujuavyo. Una matokeo mengi tusiyotarajia. Unaleta furaha na machungu mengi ndani ya dakika 90. Mpira ungekuwa unatabirika kirahisi, watu wa kubeti na kamari kwa ujumla wote wangekuwa matajiri.
Mpira ungekuwa unatabiriki hakuna ambaye angeumizwa na matokeo tena. Kwa sasa ni fahari ya macho kuyaona majina kama Pacome, Aziz KI, Maxi na Chama kwenye timu moja. Furaha yake haielezeki. Matarajio yake ni makubwa mno. Imani kwa Kocha Miguel Gamondi ni kubwa mno na kila mpira wanaogusa kwa sasa Yanga watu wanataka burudani. Kila mechi watu wanatarajia goli nyingi. Hapa ndipo Gamondi anaingia mtegoni. Hapa ndipo mpira huwa unatupa picha tofauti kabisa na tuliyokuwa nayo hapo awali.
Baada ya Yanga kumtangaza Chama na uwepo wa habari za uhakika kabisa juu ya Prince Dube kujiunga na mabingwa hao wa Jangwani, mpira unarudi sasa kwa Gamondi.
Matumaini ya mashabiki na wapenzi wa Jangwani ni kuona mpira mwingi msimu ujao. Picha kubwa vichwani mwao. Wanawaza ni mataji yote. Imani yao ni kuiona fainali ya Klabu Bingwa Afrika. Imani yao ni kuona watu wakifungwa mabao matano karibu kila mechi. Ukishakuwa na wachezaji wenye majina makubwa kama Yanga ya msimu ujao kazi kubwa inabaki kwa kocha. Mzigo mkubwa unabaki kwake. Yanga itachambuliwa msimu ujao pengine kuliko timu yotote.
Tayari timu inakwenda msimu wa nne ikiwa na mataji yote makubwa nchini. Kukosa kikombe chochote msimu ujao itakuwa ni anguko la Gamondi. Viongozi wa Yanga ni kama tayari wamejivua gamba. Kila mmoja anaona ni kama shughuli imekwisha na sasa wanasubiri mpira mwingi kutoka kwa Gamondi.
Baada ya kushinda mataji yote makubwa kwa msimu wa tatu mfululizo ndani watu wanataka kuona hatua kubwa kwenye soka la Afrika zikipigwa. Wananchi hawataridhika kuishia robo fainali tena.
Wakati PSG pale Ufaransa imewaleta Kylian Mbappe, Neymar JR na Lionel Messi kila mtu aliamimi safari ya PSG kwenda kutwaa ubingwa wa Ulaya imewadia, lakini haikuwa hivyo. Unaweza ukawaleta mastaa wote kundini, lakini suala la kufikia malengo makubwa likahitaji muda.
Bahati mbaya ni moja tu ya mpira wa Tanzania, hakuna uvumilivu. Hakuna mwenye subira. Viongozi wanataka matokeo mazuri. Mashabiki ndiyo usiseme. Pamoja na kazi nzuri sana ya Gamondi, lakini hakuna ambaye atamvumilia Yanga hii ikishindwa kufikia malengo msimu ujao. Ni rahisi sana kwa timu kama hii kumfukuza kocha.
Presha ya kufanya vizuri itakuwa ni kubwa pengine kuliko hata uhalisia. Kila mtu anatamani kuona nani anaanza na nani anaanzia benchi.
Moja kati ya maeneo ambayo Yanga wanapaswa pia kuongeza nguvu ni eneo la kiungo mkabaji. Mimi sio shabiki mkubwa wa Khalid Aucho, lakini amefanya kazi kubwa sana. Aucho ametumika sana. Kila anapokosekana Yanga inapungua ubora. Ni vyema kuongeza nguvu eneo hilo ili kujipanga kivita mapema. Ndoto za wana Yanga ni kuona Pacome, Chama, Aziz KI na Maxi wakianza kwenye kikosi.
Kila kijiwe cha soka nchini kinasubiri kuona namna ambavyo Gamondi anavyokwenda kutengeneza timu. Heshima yote aliyotengeneza na Yanga kipimo chake kikubwa kipo msimu huu. Kufungwa mechi mbili tu kunaweza kuharibu kila kitu. Huu ndiyo wakati rahisi sana wa kumfukuza Gamondi. Anatakiwa kushinda mechi. Anatakiwa kutoa burudani. Anatakiwa kushinda sio kwa kubahatisha.
Wananchi wanaamini huu ndiyo muda wa kuupiga mwingi. Gamondi ndiye mtu mwenye shughuli nzito kuliko yetote. Wananchi hawana subira. Wananchi hawataki utani na timu yao. Mambo ya kufungwa Siku ya Wananchi sidhani kama wanayataka tena. Wananchi hawataki kushinda tu, bali wanataka waupige mwingi pia.
Kwa namna ninavyowajua Wananchi huu ndiyo wakati wa Gamondi kutimuliwa kirahisi. Mpira wakati mwingine sio tu jambo la kuwa na wachezaji wakubwa. Mpira sio jambo tu la kuwa na wachezaji wengi maarufu na wenye ushawishi. Ni muunganiko wa mambo mengi. Nasubiri kuwaona Wananchi. Nasubiri kuona muunganiko wa timu. Nasubiri kuona hatima ya Gamondi. Kiukweli, Wananchi wameamua kufanya kufuru awamu hii. Kocha amepewa kila silaha ni yeye tu kuongoza kikosi cha mauaji.
Hakukuwa na haja kwa Simba kutumia nguvu kubwa kumbakisha Chama. Wakati mwingine kumpoteza mtu kama huyu kunatoa nafasi kwa timu kutengeneza watu wapya. Chama ameitumikia Simba kwa mafanikio makubwa. Ni vyema kumuacha aende kutimiza ndoto zake upande wa pili. Simba hawana haja ya kumtafuta mbadala wa chama, wanapswa kutengeneza timu mpya yenye wapambanaji wapya. Kazi ya kutengeneza timu sio rahisi lakini kwa ukubwa wa Simba hakuna linaloshindikana. Simba wamepitia nyakati kama hizi mara nyingi katika historia ya soka letu na bado waliendelea kusimama imara. Aliwahi kuondoka Juma Kasseja na Simba ikabaki imara. Aliondoka Emmanuel Okwi, Simba ikabaki. Aliondoka Kelvin Yondani na bado Simba ikabaki. Ni kawaida kwenye maisha ya soka ingawa haiondoi ukweli kuwa Yanga wamelamba dume. Pamoja na kuwa wamempata Yanga akiwa anaelekea ukingoni, lakini bado naamini Chama ana maarifa mengi sana uwanjani.
Nasubiri kwa hamu kuona namna atakavyoingia kwenye mfumo wa Gamondi ambao ndani yake kuna Aziz KI, Maxi na Pacome. Patamu sana Jangwani msimu ujao. Presha kubwa ni kwa Gamondi, lakini mashabiki wanategemea makubwa.
Gamondi ana kazı ngumu ya kuwaridhisha mashabiki msimu ujao. Makocha watakuwa wengi msimu ujao. Ni lazima achange vyema karata zake. Wananchi wanataka ushindi na udambwindambwi!