MBIO zilizopita za nchini Austria zilisisimua vilivyo wapenzi wa mashindano ya magari duniani (Formula 1) kutokana na kilichotokea kati ya madereva Max Verstappen na Lando Norris.
Wakiwa wanafukuzana kwenye mbio sita za nyuma, wawili hao waliiingia kwenye vita ya kuwania ushindi wa mbio za Austria, na vita baina yao ilikwenda hadi mwishoni kabisa ilipobaki mizunguko minane ya mwisho walipogongana kwenye harakati za kuzuiana kupitana.
Verstappen alikuwa anaongoza mbele ya Norris kama ilivyotokea kwenye mbio sita baina yao ambazo tano alishinda Verstappen, nafasi ya pili akishika Norris na moja akishinda Norris.
Safari hii ulitokea upinzani kiasi cha Verstappen kumzibia Norris asimpite na kusababisha msuguano uliosababisha tairi zao zipasuke na kumfanya Norris ashindwe kuendelea na mbio hizo.
Verstappen naye aliishia kushika nafasi ya tano nyuma ya Lewis Hamilton wa Mercedes kwenye nafasi ya nne, huku George Russell akinufaika kutoka kuwa nafasi ya tatu hadi kuibuka mshindi wa mbio kwa mara ya pili kwenye historia yake. Upinzani uliojitokeza baina ya Norris wa McLaren na Verstappen wa Red Bull, umenogesha vita ya mbio hizo ambao mashabiki na wafuatiliaji wamefurahishwa na kilichotokea kikikumbusha mbio za miaka kadhaa nyuma kulipokuwa na matukio kama hayo kwa madereva wanaokuwa wanapambania ushindi.