Polisi Mbeya yamkamata msanii anayedaiwa kuchoma picha ya Rais Samia

Mbeya. Msanii wa sanaa ya uchoraji, Shadrack Chaula (24) amejikuta akiingia matatani baada ya kujirekodi video fupi akitoa maneno makali dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan na kisha kuchoma picha ya kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ameliambia Mwananchi Digital leo Jumanne Julai 2, 2024 kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 30, 2024 katika Kijiji cha Ntokela kilichopo Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.

“Mtuhumiwa ni msanii wa sanaa za uchoraji katika Kijiji cha Ntokela, Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe, alitenda kosa la kuchoma picha inayomwonyesha Rais Samia Suluhu Hassan, kitendo ambacho ni kinyume cha taratibu za nchi na fedheha,” amesema.

Kamanda Kuzaga amechukua hatua hiyo, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kuona video hiyo mitandaoni na kutoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Baada ya kusambaa kwa kipande kifupi cha video kikimuonyesha mtuhumiwa akitoa maneno makali dhidi ya Rais na kuchoma picha yake, tulianza kufuatilia na kumkamata,” amesema.

Kuzaga amesema kwa sasa Jeshi la Polisi linaendelea na mahojiano na mtuhumiwa, kujua sababu za kufanya kitendo hicho huku taratibu za kiupelelezi zikiendelea.

“Jalada la kesi linaandaliwa na kufikishwa Ofisi ya Mashtaka kwa hatua zaidi, ili mtuhumiwa afikishwe kujibu tuhuma kwa kosa alilofanya, kwani ni kinyume cha utamaduni na maadili ya Mtanzania.

“Baada ya upelelezi, ni lazima mtuhumiwa afikishwe mahakamani kwa makosa ya kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan na kutoa maneno makali kupitia video fupi aliyojirekodi na kusambaza mitandaoni,” amesema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Homera alilaani vikali kitendo hicho.

Akitoa maoni yake kuhusu tukio hilo, mkazi wa Jakalanda jijini Mbeya, Salma Ally amesema kitendo hicho si cha kuvumiliwa na viongozi ngazi ya mkoa na watu wa intelijensia, amewataka wamhoji vizuri mtuhumiwa, kwani huenda akawa na kundi kubwa nyuma yake.

“Hili ni zito kwa kweli, huyo kijana amejiamini nini kupata muda wa kukaa kujirekodi video ya kejeli dhidi ya kiongozi mkuu wa nchi? Isitoshe amechoma picha ya Rais, tunaomba hatua zaidi zichukuliwe, ili kukomesha tabia hiyo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimelaani vikali kitendo hicho na kutaka vyombo vya dola vishughulikie suala hilo haraka.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa (Nec), Ndele Mwaselela amesema kitendo hicho hakivumiliki hata kidogo na kwamba aliyetenda kosa hilo asitie dosari kwa vijana wa Mbeya.

“Tumeona kwenye mitandao ya kijamij kijana akiwa amejirekodi video fupi ikitoa maneno ya kejeli dhidi ya Rais Samia na haikutosha akachukua picha na kuichoma moto bila  hofu ya Mungu,” amesema Mwaselela.

Amesema kama chama wanalaani kitendo hicho, lakini isitafsiriwe kama vijana wote wa Mbeya wanaweza kutenda kosa hilo, bali achukuliwe yeye kama yeye kwa mujibu wa sheria.

“Tumeelekeza vyombo vya dola vichukue hatua kwa sababu video hiyo imemkashfu na kumdhalilisha Rais na kuibua taharuki ambayo haina sababu yoyote kwa jamii na viongozi,” amesema.

Mwaselela amesema umefika wakati wana Mbeya kutoiga mikumbo na kuachana na tabia za kukashfu viongozi wa kitaifa kwa kujenga hofu ya Mungu nakulitaka Jeshi la Polisi liwadhibiti watu kama hao.

Related Posts