PUMZI YA MOTO: ‘Sumu’ ya Dube ilipoondoka na Kipre

WIKI iliyopita ilikuwa ya moto kwenye harakati za uhamisho kwa wachezaji kwa upande wa klabu ya Azam ya Chamazi Dar es Salaam.

Sakata la muda mrefu la Prince Dube lilikamilika baada ya mchezaji huyo raia wa Zinbabwe kutii amri na kulipa ‘pesa za watu’ kama walivyokubaliana kwenye mkataba.

Lakini wiki hiyo hiyo Azam FC tena walimpoteza winga wao hatari kutoka Ivory Coast, Kipre Jr. aliyeuzwa kuelekea MC Alger ya Algeria.

Katika biashara hizi mbili Azam FC wameingiza zaidi ya Sh 1 Bilioni za kitanzania, kwa hiyo unaweza kusema wamefanikiwa kiuchumi.

Lakini wakati huo huo wamepoteza wachezaji wao muhimu sana kikosini, hiyo ni hasara kiufundi.

Sote tunajua kilichotokea kwa Dube, lakini hatujui vizuri kuhusu Kipre Jr. Mtu anaweza akadhani mchezaji huyo aliyemaliza msimu wa 2023/24 akiwa na mabao 9 na pası 9 za mabao, ameuzwa kama biashara ya kawaida ya wachezaji, hapana.

Kipre Jr, amelazimishwa kuuzwa na aliandika barua ya kuitaka klabu ipokee ofa yoyote itakayokuja kwa sababu hataki tena kubakia Azam.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Azam ni kwamba Kipre Jr. alikataa kuongeza mkataba wake na Azam FC ambao utaisha 2025.

Ilimbukwe kwamba Kipre Jr alijiunga na Azam mwaka 2022 akisaini mkataba wa miaka mitatu.

Katikati ya msimu huu, Kipre Jr alifuatwa na Azam kwa ajili ya kuongeza mkataba akiwekewa ofa mara mbili ya maslahi aliyokuwa akipata – akakataa kusaini akisema anasubiri msimu uishe kwanza.

Azam hawakukubaliana na hilo, wakamuita mama yake mzazi ambaye ndiye aliyetumika kumshawishi hata wakati wanamsajili mwaka 2022.

Mama akaja na kukutana na matajiri, lakini akasema yeye kama mama hawezi kumshinikiza mwanaye, kama anasema atasaini mwisho mwa msimu basi ivutwe subira.

Hapo kengele ya hatari na tahadhari ikalia kwenye vichwa vya viongozi wa Azam kwamba chochote kinaweza kutokea… acha wajiandae.

Ndipo wakamsaini Franck Tiesse, raia wa Ivory Coast aliyekuwa nahodha wa Stade Malien ya Mali.

Tiesse na Kipre walicheza pamoja nchini kwao kwenye klabu ya Sol FC, na Kipre alikuwa akimsubiri Tiesse nje.

Msimu ukaisha na wachezaji wakaenda likizo, wakiwa huko, Kipre akaandika barua kuitaarifu Azam  kwamba hatosaini mkataba mpya, ni aidha wapokee ofa itakayokuja au arudi kumalizia mwaka wake mmoja uliobaki halafu aondoke bure.

Azam wakaona mambo yamekuwa makubwa, wakakubali ofa na kumuacha mchezaji aondoke.

Prince Dube na Kipre Jr, walikuwa wanakaa chumba kimoja wakiwa kambini pale Chamazi kwneye hostel zao.

Hii ikiwafanya wawe karibu sana wakiongea vitu vingi kama binadamu wengine walivyo.

Yawezekana ukaribu wao ulimfanya Dube afunguke vitu vingi kwake na kumtia sumu. Ukisikiliza maneno aliyoyaongea Dube baada ya kuondoka Azam utagundua kwamba alikuwa na mengi sana moyoni.

Na kuna uwezekano mkubwa sana hayo mengi pia alimmezesha Kipre na kumchafua roho kabisa.

Hii ni kwa sababu baada tu ya Dube kuondoka, Azam ndiyo walianza harakati za kutaka kumuongezea mkataba Kipre, na akakataa.

Na kauli yake ya kwamba “pokeeni ofa itakayokuja” ina maana kwamba tayari mchezaji huyo alishaongea na ile klabu na kukubaliana nayo.

Haya mambo huwa hayaji ghafla…huja kidogo kidogo.

Kwa heshima ambayo Kipre Jr. alikuwa akipewa na Azam, yeye na familia yake nyumbani Ivory Coast, usingetemea abadilike ghafla vile.

Licha ya kupewa heshima kubwa sana, lakini Dube hakuaona kama Azam inamtendea haki kama nyota wake mkubwa zaidi.

Ujio wa watu kama Ali Ahamada na taarifa za kwamba analipwa pesa nyingi zaidi yake, zilimuuma.

Mbaya zaidi yeye ambaye ndiyo alama ya klabu alipangiwa nyumba Chamazi halafu Ahamada akapangiwa Masaki, na akapewa Range la kutembelea.

Hii akashindwa kuvumilia, akaomba apangiwe nyumba nyingine maeneo ‘mjini’, mwenyewe akachagua Tabata.

Akapangiwa hiyo nyumba na kuwekewa kila kitu ndani. Kwa hiyo Dube akawa na nyumba mbili, ile ya Chamazi na Tabata.

Angalau hasira za Dube kwa Ahamada zikapungua kidogo.

Lakini kwenye dirisha dogo la Januari, akaja Franklin Navarro, na baadaye Yeison Fuentes Mendoza.

Ikasemekana kwamba hawa nao wamelipwa pesa nyingi sana, wamepangiwa nyumba Masaki na wamepewa gari la kutembelea.

Hapa mambo yakamfika rohoni Dube, akashindwa kuvumilia – akaandika barua ya kuondoka kwenda kwa watu watakaompa heshima anayodhani anastahili.

Sasa wakati haya yote yanatokea, Dube anakaa chumba kimoja na Kipre Jr unadhani hawakuwa wakiyajadili?

Kipre naye kama staa wa Azam alipangiwa nyumba Chamazi, na wala hakupewa gari.

Naye kama binadamu lazima hii sumu ya Dube ilimuingia, ikaanza kumtesa moyoni.

Akafikiri kwa kina na kuona jambo pekee la kumpa amani ni kuondoka tu akapate heshima sehemu nyingine.

Na hata pale Azam waliopomfuata kutaka kumuongezea mkataba, yawezekana tayari nafsi yake ilishafura kwa hasira na tayari alishafanya maamuzi.

Hata hivyo, mwisho wa siku Azam imepata hela ambazo wanaweza kuzitumia kupata wachezaji wengine watakaoitoa klabu hapo ilipo na kwenda mbele.

Mpira wa kulipwa ni mchezo wa kibepari unaangalia zaidi biashara.

Wasifu wa mchezaji una maana kubwa sana katika kuamua thamani yake.

Dube alijiunga na Azam akiwa na wasifu mdogo sana. Ni Azam ndiyo imemkuzia wasifu wake. Na hii ni hata Kipre Jr. pia.

Ni tofauti na Ali Ahamada, na wale wacolombia. Wote wamekuja kama wachezaji wa daraja la juu.

Dube na Kipre huko wanakoenda sasa ndiyo watakutana na heshima kama ambayo kina Ali Ahamada na wacolombia waliipata Azam FC.

Hata huko pia, kuna wachezaji ambao roho zitawauma kuona wao wanapewa hiyo heshima.

Mwisho wa siku Azam FC imepata hela. Wachezaji wamepata maisha. Na klabu zao mpya zimepata wachezaji.Acha maisha yaendelee.

Related Posts