Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata kuwa Mshauri wa Rais, Ikulu nafasi inayomuondoa katika nafasi yake ya awali.
Kidata anaondolewa TRA ikiwa ni wiki moja ipite tangu mgomo wa wafanyabiashara nchi nzima ufanyike wakilalamikia utitiri wa kodi unaotozwa na TRA.
Aidha, Rais Samia amemteua aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Yusuph Juma Mwenda kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwenda anateuliwa kushika wadhifa huo akichukua mikona ya Alphayo Kidata aliyehamishiwa kuwa Mshauri wa Rais, Ofisi ya Rais Ikulu.
Kidata aliteuliwa na Rais Samia kuwa Kamishna wa TRA Aprili 4, 2021 akirejea katika nafasi hiyo baada ya kuondolewa na Hayati John Magufuli Machi 25, 2017.
Baada ya kutenguliwa Kidata aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Ikulu, nafasi aliohudumu hadi Januari 10, 2018 alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, nafasi alioitumikia kwa miezi 10.
Septemba 20, 2019 Hayati Magufuli alimteua Kidata kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, nafasi aliohudumu hadi mwaka 2021.
Miongoni mwa jambo linalomsubiri katika nafasi hiyo mpya, ni utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara wanaoulalamikia.
Yusuf Mwenda aliwahi kuwa diwani wa Mikocheni na Meya wa Kinondoni kuanzia mwaka 2010/ 2015, wakati akihudumu umeya alikuwa pia mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Machi Mosi, 2022 Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alimteua Mwenda kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), akichukua nafasi ya Salum Yussuf Ali aliyetenguliwa.
Desemba 29, 2022 katika kilele cha sherehe za mlipakodi, 2021/22, Dk Mwinyi alimpongeza Mwenda kwa kazi nzuri akisema ZRB imekuwa na mwelekeo mzuri katika ukusanyaji wa mapato tofauti na vipindi vilivyopita.
Endelea kufuatilia Mwananchi.