Rais Samia apangua mawaziri wawili, vigogo TRA na ZRA

Tanga. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali ikiwemo mawaziri na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Uteuzi huo umetangazwa usiku wa leo Jumanne, Julai 2, 2024 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.

Balozi Kusiluka amesema Rais Samia amemteua Dk Seleman Jafo kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Awali, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Pia, Rais Samia amemteua Dk Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano na Mazingira) akitoka kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Kwa maneno mengine, Jafo ambaye ni Mbunge wa Kisarawe Mko wa Pwani na Kijaji, Mbunge wa Kondoa mkoani Dodoma wamebadilishana wizara.

Katika uteuzi huo, Rais Samia ameigusa TRA ambayo Juni 24, 2024 Mwananchi Digital liliripoti uwepo waanadiliko ya watendaji ndani ya mamlaka hiyo.

Msingi wa mabadiliko hayo ni malalamiko ya wafanyakazi dhidi ya TRA juu ya kamatakamata ya wafanyabiashara na wateja wao hali iliyosababisha mgomo uliodumu kwa takribani siku nne.

Mgomo huo ulianza Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kusambaa mikoa ya Mbeya, Dodoma, Iringa, Kigoma, Ruvuma, Morogoro, Kagera na Mwanza.

Miongoni mwa malalamiko ya wafanyabiashara ni kurejeshwa kimya kimya kwa kikosi kazi cha kudai kodi ambacho kimetajwa kuwabughudhi wafanyabiashara.

Hata hivyo, inaelezwa huenda si maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa watendaji wa juu ndani ya mamlaka hiyo, lakini kwa kuwa ni jambo lililokemewa mara kadhaa halikupaswa kuachwa lifanyike.

Katika uteuzi huo, Balozi Kusiluka amesema Rais Samia amemteua Yusuph Mwenda kuwa Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo akichukua nafasi ya Alphayo Kidata ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Ikulu.

Kabla ya uteuzi huo, Mwenda alikuwa  Mkuu wa Mamlaka za Mapato Zanzibar (ZRA).

Aliwahi kuwa diwani wa Mikocheni na meya wa Kinondoni, Dar es Salaam kuanzia mwaka 2010/ 2015, wakati akihudmu umeya alikuwa pia mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Machi Mosi, 2022 Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alimteua  Mwenda kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), akichukua nafasi ya Salum Yussuf Ali aliyetenguliwa. Baadaye ZRB ilibadilishwa na kuwa ZRA.

Desemba 29, 2022  katika kilele cha sherehe za mlipa kodi, 2021/22, Dk Mwinyi alimpongeza  Mwenda kwa kazi nzuri akisema ZRB imekuwa na mwelekeo mzuri katika ukusanyaji wa mapato tofauti na vipindi vilivyopita.

Kidata ambaye amepelekwa Ikulu

aliteuliwa na Rais Samia  kuwa Kamishna Mkuu wa TRA Aprili 4, 2021 akirejea katika nafasi hiyo baada ya kuondolewa na Hayati John Magufuli Machi 25, 2017.

Baada ya kutenguliwa Kidata aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Ikulu, nafasi aliohudumu hadi Januari 10, 2018 alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, nafasi alioitumikia kwa miezi 10. Alirejeshwa nchini na kuvuliwa hadhi ya Ubalozi na Rais wa wakati huo, Magufuli.

Septemba 20, 2019 Hayati Magufuli alimteua Kidata kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, nafasi aliohudumu hadi mwaka 2021.

Aidha, Kidata amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Katika uteuzi mwingine alioufanya Rais Samia ni wa Yahaya Samamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini. Awali alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.

Samamba anachukua nafasi ya Khero Mahimbali ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Related Posts