RC Batilda azicharukia taasisi za Serikali zinazodaiwa bili za maji

Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, balozi Batilda Burian, ameziagiza taasisi zote za Serikali zinazodaiwa bili za maji na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) na mamlaka nyingine kulipa madeni hayo mara moja.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya mfumo wa Maji Information System, (Majils) kwa  Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) leo Jumanne Julai 2, 2024, mkuu huyo wa mkoa amesema wote wanaodaiwa wapelele makadirio yao Ruwasa kuangalia wanalipa vipi.

Amesema kama kuna watumishi ambao kwa taratibu za kazi zao wanalipiwa bili za maji kwenye maeneo wanayoishi lakini wamehamia nje ya maeneo hayo ya kazi, wanatakiwa kulipa maduhuli hayo.

“Wapo wafanyakazi walikuwa wanaishi kwenye nyumba za kambi za majeshi, sasa wamehamia mahali pengine na wameacha bili za maji hazijalipwa, wanatakiwa kuzilipa, wanapaswa kukaa na waajiri wao wakubaliane fedha hizo wakatanaje,” amesema.

Hata hivyo, Burian amesema agizo hilo halizigusi taasisi zinazopatiwa huduma za maji kisheria, ila wengine wote ambao wapo nje ya misamaha hiyo maalum, wafike kwenye ofisi za mamlaka ya maji na wakadiliwe madeni yao na kuyalipa.

Balozi Batilda amesisitiza kwamba fedha hizo ndio zinakwenza kuisaidia mamlaka ya maji mkoani humo kujiendesha.

Hivyo, amesisitiza ni lazima taasisi zote za serikali kuzingatia ulipaji wa bili za maji kwa wakati.

Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Tanga, Upendo Lugongo amesema kuna taasisi za serikali zinadaiwa bili za maji kwa muda mrefu.

“Kwa kuwa madeni ni mengi, bado tunaendelea kusaka hesabu kamili na tunachoendelea nacho sasa ni kukusanya madeni,” amesema Lugongo.

Amesema mfumo wa Majils sasa utawezesha kukusanywa kwa bili za maji kwa urahisi, kwa sababu zote zitasomwa kielektroniki, hivyo kila mhusika taarifa zake zitakuwa kwenye mfumo huo na itakuwa rahisi kukusanywa.

“Taasisi za maeneo ya kijijini nyingi zilikuwa hazilipii huduma ya maji, hivyo hatuna madeni rasmi ya taasisi hizo ambazo ni za vijijini. Kupitia mfumo huu zimeingizwa katika mifumo ya ulipiaji bili na zitaweza sasa kama zina madeni yataonekana humo na kulipwa,” amesema Upendo.

Emanuel Shoo kutoka CBWSOs wilayani Lushoto amesema mfumo wa Majils ni mwarobaini wa ukusanyaji bili.

“Awali ilikuwa lazima mtoa huduma afike kwa mteja, ila huu mfumo wa kielektroniki, bili zitatumwa kwa ujumbe mfupi,” amesema.

Amesema hata bili za maji zilizolipwa kupitia mfumo huo zitaonekana moja kwa moja kwenye mfumo huo wa CBWSO.

Kwa kupitia mfumo huo wa CBWSO, kiasi cha Sh7 milioni kimekusanywa ndani ya siku mbili tangu kuanza kwa mwaka wa fedha wa serikali 2024/2025 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkoa wa Tanga.

Related Posts