Sababu wanafunzi kufanyiana mitihani vyuo vikuu

Si tukio la kawaida kwa walio wengi, lakini limetokea na pengine yamekuwa yakitokea matokeo mengi ya aina hiyo, lakini hayaripotiwi.

Si habari njema kwa kuwa linatia doa sekta ya elimu nchini. Ni tukio la uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kuwakamata watu 17 wakijaribu kuwafanyia mitihani wanafunzi wa chuo hicho.

Waliokamatwa ilielezwa walikuwa na vitambulisho vya kughushi na tiketi ya ukumbi wa mitihani.

Kwa mujibu wa OUT, watuhumiwa hao walikamatwa kuanzia Juni 18, 2024 katika vituo vya mitihani vya Ilala na Kinondoni na sasa wapo mikononi mwa vyombo vya dola.

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda , chuo kilianza mitihani Juni 3 hadi 24, huku wanafunzi 10,417 wakifanya mitihani katika vituo 53, ambavyo vimesambaa nchi nzima.

“Katika kipindi cha wiki tatu za mitihani, kwa umakini wa mifumo yetu, wasimamizi wa mitihani waliwakamata mamluki wapatao 17, hususan katika vituo vya Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam. Matukio mengi yalibainika kuanzia Juni 18,” alisema.

Alisema kitendo cha watu hao kughushi vitambulisho vya chuo na tiketi ya ukumbi wa mitihani ni vitendo vya jinai, hivyo sheria itachukua mkondo wake.

Alifafanua kuwa waliokamatwa siyo wa chuo hicho, bali ni kutoka vyuo vingine na wengine ni wafanyakazi katika fani walizosomea.

Kufuatia sakata hilo la aina yake sio tu kwa chuo hicho bali katika sekta nzima ya elimu, Mwananchi limefanya uchunguzi mdogo na kubaini kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa wanafunzi wa vyuio vikuu kufanyiana mitihani.

Lakini sio tu wanafunzi, uchunguzi utokanao na maoni ya baadhi ya wadau umebaini kuwa upo uwezekano hata wa watu wa nje wasio wanafunzi kufanya mitihani kama ilivyokuwa kwa baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa OUT.

Mwalimu mstaafu, Bakari Kheri anasema kwa mazingira aliyoyaona akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliposoma kwa miaka minne, kuna mianya mikubwa inayoweza kutumiwa na wanafunzi kufanyiana mitihani au hata watu wa nje kujifanya wanafunzi.

‘Mimi nimesoma ualimu, ni moja ya fani zenye wanafunzi wengi mno chuoni hapo. Nyingine ni sheria niliyoiona ikiwa na wanafunzi wengi. Katika mazingira haya kuna kozi lazima mfundishwe kwenye ukumbi mkubwa kama Nkrumah, ambao hata mwanafunzi wa chuo kingine au mtu baki tu anaweza kuzamia na asijulikane,” anasema na kuongeza:

‘Kuna kozi mpo wanafunzi zaidi ya 200, mhadhiri gani anayeweza kuwajua wote kwa sura? Sasa acha kuzamia mtu akasikiliza mhadhara, hata mtihani katika mazingira hayo mtu anaweza kufanyiwa. Ni suala tu la kukupa namba yangu ya usajili, unaingia unafanya paper (mtihani) maana hata wanafunzi wengine ni vigumu kukustukia.”

Anasema hajui utaratibu ulivyo sasa chuoni hapo kudhibiti watahiniwa kama ni halali ama la, anachokumbuka wakati anasoma, hapakuwa na mfumo wa kuwatambua wanafunzi wanapoingia kwenye chumba cha mtihani.

“Kwa ule utaratibu na ukitazama kozi kama za ualimu sheria au masomo ya sanaa, zilivyo na wanafunzi wengi, uwezekano wa kufanyika udanganyifu ni mkubwa. Open Chuo Kikuu Huria, wamejifunza kwa tukio hili la aibu, nadhani wataweka mifumo imara ya kisasa ya utambuzi. Vyuo vingine navyo vifanye hivyo hasa katika zile kozi zenye idadi kubwa ya wanafunzi,” anaeleza mwalimu huyu huku akishauri matumizi ya teknolojia kutambua wanafunzi wakati wa ufanyaji mitihani.

Maoni ya mwalimu Kheri yanaoana na mtazamo wa mchambuzi wa masuala ya elimu, Adonis Byemelwa anayesema wanafunzi wakiwa wengi na wakatoka katika kampasi tofauti kama ilivyo kwa Chuo Kikuu Huria chenye matawi karibu kila kona ya nchi, ni vigumu hata wanafunzi kujuana na hivyo kushindwa kuwagundua “ wazamiaji”

‘ Mazingira ya vyuo vyetu ni changamoto na huchangia wizi wa mitihani, maana lecturer halls (kumbi za mihadhara), ndio hutumika kama vyumba vya mitihani ambapo unakuta hakuna hata kamera za siri. Ukumbi wa kuingia wanafunzi 300 unakuta wanakaa mpaka 400, huku kukiwa na uhaba wa viti hadi wengine husoma wamesimama,” anaeleza.

Anaongeza: “ Ikitokea hivyo, ukipewa jaribio kwenye mazingira haya, ni rahisi ‘kuunda kijiji’, yaani anayejua zaidi somo fulani hukaa katikati huku pembeni akiwapa majibu walio dhaifu na mitihani huvuja kwa mtindo huo. Anaendelea kusema kuwa vyuo vingi vinaelemewa na wanafunzi kiasi kwamba hadi vifaa havitoshi kufanya practicals (mafunzo kwa vitendo) na pengine wahadhiri hushindwa kusahihisha kundi kubwa la wanafunzi hasa kwa sasa ambapo hawapewi posho.

Kukamatwa kwa watahiniwa hao feki OUT, ni kielelezo cha kuwapo kwa vitendo mbalimbali vya udanganyifu katika taasisi za elimu ya juu nchini.

Udanganyifu ni changamoto kongwe vyuoni ukiwa na sura mbalimbali ndani yake, licha ya ukweli kuwa mamlaka nazo hazijabweteka katika kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo.

Miongoni mwa vitendo hivyo ambavyo aghalabu vimekuwa vikiripotiwa na vyombo vya habari, ni pamoja na wizi wa mitihani, wanafunzi kufanyiwa mazoezi, utafiti na kuandikiwa tasnifu za utafiti.

Katika ripoti ya utafiti wake wa shahada ya uzamili aliouita kwa jina la; The prevalence of academic cheating in Tanzania Universities, Peter Muga, anasema katika utafiti wa vyuo sita alivyovifanyia uchunguzi, amebaini tatizo la udanganyifu wa mitihani linalojumuisha wizi husababishwa na wahadhiri na wanafunzi, huku akivitaja vyuo navyo kuwa moja ya sababu zinazochangia hali hiyo.

Kwa wahadhiri alisema vitendo wanavyovifanya ni pamoja na kuuza mitihani, kuiba mitihani pamoja na kuvujisha kwa wanafunzi.

‘’Examination cheating committed by students include copying from other students, seeking help from fellow students during the exams, sitting closer to academically able students and hiding materials in toilets, anaandika Muga katika dokezo la utafiti huo lililowekwa katika wavuti wa maktaba ya chuo Kikuu cha Dar es Salaam (http://[email protected]).

Tafasiri ya dokezo hilo Muga anasema: ‘’ Udanganyifu wa mitihani unaofanywa na wanafunzi unajumuisha wanafunzi kunakiliana majibu, kusaidiana wakati wa kufanya mitihani kwa wanafunzi dhaifu kukaa karibu na wale wenye uwezo na pia kuficha majibu maliwatoni.’’

Aidha, udanganyifu mkubwa wa kitaaluma ni ule wa ubwakuzi, ambapo mwanafunzi anatumia au kughushi kazi za mwingine hasa katika uandishi wa tasnifu na tazmili.

Ili kukomesha vitendo vya namna hiyo, Profesa Bisanda alisema OUT ipo kwenye maandalizi ya kuwasajili wanafunzi wote kwa alama za vidole, na kumhakiki kila mtahiniwa kwa mashine maalumu za utambuzi wa alama za vidole katika vituo vyote vya mitihani.

Profesa Bisanda alisema OUT kimejijengea sifa kimataifa, kwa kuwa na mfumo madhubuti wa usalama wa mitihani.

“Chuo kimeweza kutumia wataalamu wake wa Tehama, kujenga mfumo wa mitihani, ambao ni vigumu sana mtihani kuvuja. Hata mwalimu anayefundisha somo fulani, hajui wanafunzi wake wataulizwa maswali gani. Anakutana na maswali hayo wanafunzi wakishamaliza kuandika mtihani, na ndipo anaandaa utaratibu wa kuusahihisha,” alisema.

Kwa upande wake, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), kinaeleza kuwa kimekuwa kikitumia njia za kisasa kukabiliana na udanganyifu kwenye kazi za kitaaluma chuoni hapo hasa ripoti za utafiti.

“Tuna software ya ‘Turnitin’ ambayo ina uwezo wa kubaini originality (uhalisia) wa kazi za kitaaluma… na tangu tuanze kuitumia, ni lazima kazi ya mwanafunzi ipitie software hiyo, ili ijulikane kiwango cha uhalisia wa kazi kiasilimia,’’ alisema Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye katika mahojiano aliyofanya na gazeti dada la The Citizen mwaka 2020.

Kwa mujibu wa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Christian Bwaya, wizi wa mitihani katika mfumo wa elimu wa ngazi yoyote ile, huathiri maslahi mapana ya maendeleo ya taifa, hivyo kinapaswa kuchukuliwa kama kitendo cha kuhujumu taifa.

‘’Fikiria itakapofika wakati ambapo mataifa mengine yatakapokuwa na mashaka na wasomi wetu. Sisi wenyewe ndani ya nchi tunahudumiwa na daktari, lakini unamtazama mara mbili mbili na kujiuliza moyoni kama ana sifa,’’ anaeleza.

Aidha, anasema athari kubwa ni kupata watumishi wa kada mbalimbali ambao siyo waadilifu. Hawana maadili kwa sababu wamekulia hivyo katika mfumo huo tangu shule ya msingi.

Kwa upande wake, Byemelwa anasema kuendelea kwa matukio ya udanganyifu vyuoni, ni kuzidi kutengeneza wahitimu feki, na hilo linaweza kuepukika ikiwa Taifa litaacha kuamini katika vyeti na kuweka msisitizo kwenye ujuzi.

 Ingekuwa tuna njia nyingine za upimaji nje ya kuandika kwenye makaratasi, huenda tusingekuwa na haja ya kuiba mitihani. Tunapata ishara kwamba mfumo mzima wa tathimini ya ubora wa wanafunzi wetu nchini ni mibovu, na hakuna miundombinu stahiki ya kusimamia mitihani,’’ anabainisha.

Related Posts