SIMBA inaendelea kusuka upya kikosi chake na sasa imeonyesha jeuri ya pesa katika kuwania saini ya winga wa kulia Elie Mpanzu (22), kutoka AS Vita ya DR Congo.
Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kutoa taarifa ya Simba kuwa kwenye mazungumzo na Mpanzu kutaka saini yake na huu ni mwendelezo wa dili hilo lilipofikia.
Jana mastaa wa timu hiyo walianza kuwasili kambini kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kusafiri kwenda mjini Ismailia, Misri kwaajili ya kambi rasmi ya msimu ujao.
Simba imeanza kuja utamu baada ya kukamilisha usajili wa mastaa Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Yusuph Kagoma kutoka Singida, Omary Omary kutoka Mashujaa.
Wengine ni Mzambia Joshua Mutale kutoka Power Dynamos, Mganda Steven Mukwala kutoka Asante Kotoko, MburkinaFaso, Valentino Nouma kutoka Lupopo licha ya kwamba aliyetambulishwa ni Lawi Pekee.
Vilevile Simba inatarajia kutangaza benchi jipya la ufundi ambapo Davids Fadlu na Steven Kompela wote kutoka Afrika Kusini mmojawao atakuwa kocha mkuu wa chama hilo kwa msimu ujao.
Awali Simba ilikutana na ugumu kwenye dili la Mpanzu kutokana na mabosi wa AS Vita kumng’ang’ania Mpanzu na kumuwekea dau nono, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wakamtuma mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyeenda kulainisha dili hilo licha ya kwamba haikuwa rahisi.
Baada ya AS Vita kujua Simba imemfuata hadi Kinshasa, Mpanzu, mabosi wa timu hiyo wakiongozwa na Rais wake, walimuita mchezaji huyo na kukaa naye kikao kizito lakini akachomoa.
Vita ilimuwekea Mpanzu mezani kitita cha pesa zaidi ya Sh400 milioni ili asaini mkataba mpya, lakini winga huyo alikataa kusaini na kuweka wazi anataka kuondoka.
Wakati Vita ikiendelea kumbembeleza Mpanzu, Simba ilimpigia simu na kumueleza ipo tayari kutoa zaidi ya pesa hiyo ili impate na hapo ndipo akatoa masharti yake kuhusu kusaini ambayo kwa kiasi kikubwa yaliafikiwa na vigogo wa Simba.
Viongozi wa Simba wiki hii wanamtumia tiketi ya Ndege Mpanzu na kufika Jumamosi atakuwa amewasili jijini Dar es Salaam kwaajili ya kusaini mkataba wa miaka miwili na rasmi kuwa Mwanamsimbazi.
“AS Vita walimuwekea pesa ndefu ili abaki, ikatubidi nasisi toungeze pesa na ushawishi jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limesaidia na mambo yasipobadilika anaweza akaja Dar es Salaam wiki hii,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba.