WAKATI wafanyabiashara nchini wakiweka mgomo wa siku tatu kupinga makadirio makubwa ya kodi na mifumo isiyo rafiki ya ukusanyaji wa kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeandika historia ya ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 ikiwemo kukusanya kiasi cha Sh 27.64 trilioni ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.67 ya lengo la kukusanya Sh 28.30 trilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Hayo yanajiri wakati pia mabalozi wa Marekani, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden, na Ujerumani wakiomba kikao na Serikali ya Tanzania kutokana na wawekezaji wa nchi hizo waliowekeza nchini, wakibambikiwa kodi za kipindi cha miaka 15 iliyopita ppamoja na kufungiwa akaunti na TRA.
Taarifa iliyotolewa na TRA jana na kusainiwa na Kamishna Mkuu, Aphayo Kidata ilisema makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia asilimia 14.50 ikilinganishwa na makusanyo ya Sh 24.14 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya kiasi hicho cha fedha.
“Katika kipindi cha robo mwaka ya nne yaani Aprili hadi Juni mwaka huu, TRA ilikusanya kiasi cha Sh 7.09 trilioni sawa na ufanisi wa asilimia 99.46 ya lengo la kukusanya kiasi cha Sh 7.13 trilioni.
“Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 24 ukilinganisha na kiasi cha Sh 5.72 trilioni kilichokusanywa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023,” amesema.
Aidha, amesema ongezeko hilo la makusanyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 limechagizwa na ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini hususani uzalishaji viwandani na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea nchini kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo.
Pia limetokana na mwitikio mzuri wa walipakodi wengi katika kuwasilisha ritani na kulipa kodio kwa wakati.
“Kuongezeka kwa uhiari wa ulipaji kodi kufuatia maboresho yanayoendelea kufanywa na TRA ikiwemo uboreshaji wa mfumo wa TEHAMA kusogeza uhuduma jirani na walipakodi kwa kuanzisha Divisheni za walipa kodi wadogo na walipa kodi wa kati pamoja na kuendelea kusuluhisha pingamizi za kodi nje ya mahakama.
“Pia kuongezeka kwa uingizwaji wa mizigo toka nje ya nchi kutokana na uboreshwaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini,” amesema.
Kamishna Kidata amesema pamoja na hayo, vitendo vya ukwepaji kodi na kutozingatia sheria vimeendelea kushamiri miongoni mwa makundi mbalimbali ya walipakodi ikiwemo watu binafsi, makampuni ya ndani na yale ya kimataifa.
Amesema TRA itaendelea kuhimiza ulipaji kodi kwa kufuata sheria zilizopo na utekelezaji wake kuzingatia msingi ya utawala bora.
“TRA inaendelea kuhimiza matumizi ya njia ya majadiliano na maridhiano katika kuzuia na kutatua migogoro mbalimbali ya kikodi kwani mara nyingi njia hii immekuwa ikileta matokeo chanya yenye manufaa kwa pande zote,” amesema.