TRC yapokea seti mbili za treni ya kisasa

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) imepokea seti mbili za treni ya kisasa inayotumia nishati ya umeme EMU, (Eletric Multiple Unit) na vichwa vinane vya treni.

Seti hiyo imewasili nchini kutoka Korea ya Kusini. Kwa sasa TRC imeshapokea seti tatu zilizowasili mpaka sasa. Seta ya kwanza iliwasili Aprili 2024.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumanne, Julai 2, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa TRC, Jamila Mbarouk imeeleza Serikali kupitia shirika hilo ilifanya manunuzi ya seti 10 za treni za EMU, zinazotengenezwa na kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini.

Amesema seti moja ya EMU ina jumla ya mabehewa manane yakijumuisha kichwa kimoja mbele na kingine nyuma, ikiwa ina uwezo wa kubeba abiria 589 na kutembea kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa.

Hadi kufika sasa TRC limeshapokea jumla ya mabehewa 65 ya abiria, vichwa 17 vya umeme na seti tatu za EMU.

“Upokeaji wa vifaa vya uendeshaji vya reli ya kiwango cha SGR unaendelea kwa awamu totauti, vifaa vipya vilivyowasili vitaendelea kufanyiwa majaribio kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kuanza kutoa huduma,” amesema Jamila.

Amesema shirika linaendelea na uendeshaji wa awali na uotoaji huduma ya usafiri wa treni za umeme kupitia reli ya kiwango cha kiamataifa kati ya Dar es Salaam na Morogoro, uendeshaji rasmi kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma unaotarajiwa kuanza Julai 25, 2024.

Pia shirika hilo lina mpango wa kuagiza vichwa vya treni vinavyotumia dizeli kwa ajili ya kuvuta treni ya umeme endapo itaharibika katikati ya safari. 

Jamila amesema, hatua hiyo ni muendelezo wa uboreshaji kwenye usafiri huo hapa nchini tangu ulipoanza safari zake rasmi kutoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro Juni 14, 2024.

Related Posts