Ukweli kuhusu matumizi ya maji ya bamia

Dar es Salaam. Jamii imekuwa na mtazamo tofauti kuhusu matumizi ya bamia, baadhi wakiamini kwa kutumia maji yake wanaweza kuongeza uteute kwenye magoti.

Mbali ya hao, wapo wanaoamini kwa kutumia maji ya bamia wanaweza kuongeza uteute ukeni.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa kutokana na utajiri wa vitamini na viambata vilivyomo ndani ya bamia, huchangia kuimarisha afya kwa mtumiaji wa mara kwa mara.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Pharmaceutical Biology, nyuzinyuzi za bamia, mbegu na majimaji yake husaidia kuboresha afya ya mtumiaji.

Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Kenedy Nchimbi amesema bamia zina madini ya magnesiamu na kalisiamu ambayo yanahitajika kwenye mifupa.

“Maji ya bamia yana faida na kwa upande wa afya ya mifupa kuna madini ya magnesiamu ambayo ni muhimu, japo hayapatikani kwa wingi. Pia kalisiamu ipo nayo siyo sana. Ila maji hayo yana uwezo mkubwa wa kukinga mwili,” amesema.

Alipoulizwa iwapo bamia zinasaidia kuzalisha uteute kwenye maungio ya mifupa amesema: “Hata makongoro wanasema hivyo, lakini hakuna ukweli, ingawa bamia zina faida nyingi mwilini.”

Akizungumzia maji ya bamia, mkufunzi katika Chuo Kikuu cha INTI International cha nchini Malaysia, Dk Mohd Haizra Hashim anasema husaidia kupunguza matatizo ya mmeng’enyo wa chakula.

“Bamia ina ute mwingi, maji yanayofanana na jeli ambayo husaidia kutuliza njia ya usagaji chakula. Inasaidia kuwezesha choo laini na kuzuia kuvimbiwa,” anasema Dk Mohd.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Isaya Mhando anasema maji ya bamia husaidia kuimarisha ngozi kwa kuwa yana vitamini C.

“Husaidia ngozi zote laini za ndani ya mwili, mfumo wa hewa na uzazi kwa wote mwanaume na mwanamke, siyo kwamba ni dawa lakini inachangia kuimarisha homoni, mzunguko wa mwanamke na kuzalisha ute na kudhibiti ukavu ambao wakati mwingine huja na harufu isiyo nzuri,” amesema Dk Mhando.

Kwa mujibu wa utafiti katika jarida la sayansi ya chakula na teknolojia (Journal of Food Science and Technology) ute kwenye bamia hufanyika kama kilainishi cha asili kwenye utumbo.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Times of India bamia ina vitamini C ambayo husaidia kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuzuia magonjwa mbalimbali.

Utafiti katika jarida la American Journal of Clinical Nutrition uligundua kuwa lishe yenye nyuzinyuzi nyingi, ikijumuisha vyakula kama vile bamia, inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya lehemu, hivyo kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo na kiharusi.

Bamia inaelezwa kuwa chanzo kizuri cha vitamini K na folate. Pia inasaidia kupunguza viwango vya sukari kwenye damu, hivyo kuwa na manufaa kwa watu wenye kisukari.

Bamia pia ina viambato vyenye uwezo wa kupambana na saratani, kama vile antioxidants, ambazo husaidia kuondoa sumu mwilini.

Vitamini A iliyopo kwenye bamia pamoja na beta-carotene ni muhimu kwa afya ya macho.

Related Posts